SoC04 Ukasuku wa matabibu katika tasnia ya Afya dhidi ya magonjwa sugu na ya kuambukiza; Suluhisho mbadala katika ujenzi wa Tanzania mpya

SoC04 Ukasuku wa matabibu katika tasnia ya Afya dhidi ya magonjwa sugu na ya kuambukiza; Suluhisho mbadala katika ujenzi wa Tanzania mpya

Tanzania Tuitakayo competition threads
Joined
Jun 17, 2024
Posts
12
Reaction score
14
TANBIHI: Nimetumia neno "tabibu" nikimaanisha wataalamu wote wa afya, wanasayansi na wote wanaohusika katika mlolongo mzima wa tasnia ya afya nchini.

Neno "tabibu" linaweza kuwa na maana finyu katika Kamusi, lakini kwa madhumuni ya bandiko hili, neno "tabibu" litumie tafsiri niliyoitoa hapo juu.

Bandiko hili limechochewa na mfuatano wa matukio yaliyothibitisha jinsi ambavyo matabibu wetu wamesinzia na kuzubaa katika kujenga misingi imara ya huduma za afya ambazo taifa lina umiliki nazo, lina utambuzi nazo, lina ubunifu nazo na limejihakikishia usalama wake katika nyakati za dharura na nyakati zisizo za dharura.

Matukio yafuatayo yanathibitisha ukasuku katika tasnia ya afya:-

1. Kukosekana kwa tiba ya kudumu dhidi ya maradhi sugu au tafiti mbadala kuhusu maradhi hayo:-

Maradhi sugu kama vile Kisukari, saratani, na Virusi vya Ukimwi, yameendelea kuwa tishio kubwa huku yakigharimu maisha ya watu wetu mamia kwa maelfu.

Wataalamu wetu wa afya wamejikita kwa kiasi kikubwa katika kuegemea na kutegemea tafiti za wazungu ambazo zimepigilia msumari wa mwisho katika magonjwa hayo kuwa hayawezi kutibika kwa namna yoyote ile. Tafiti hizi za wazungu zimechimba mizizi mirefu mpaka kwenye mitaala ya shule za kitabibu na katika vitabu vyote ambavyo wataalamu wetu wa afya hutumia kujifunza elimu hiyo.

Kwa sababu hii, wataalamu wetu wa afya na watabibu wameendelea kusoma tafiti hizi za wazungu na vitabu vyao kwa kukariri pasipo kufikiri nje ya boksi. Katika miaka 63 ya uhuru wa taifa baada ya kupata mamia na maelfu ya wataalamu wa afya, hakuna tafiti zozote za kisayansi ambazo wamezifanya kuchunguza, kuthibitisha, au kupinga tafiti zilizofanywa na wazungu kuhusu magonjwa sugu yasiyotibika.

Tafiti za wazungu kuhusu magonjwa sugu tajwa hapo juu zimeendelea kutawala tasnia ya afya nchini kama msahafu uliopigwa muhuri wa moto usiofutika wala kutenguliwa kwa namna iwayo yoyote.

2. Matumizi ya madawa na chanjo zilizotoka nje ya nchi yasiyo na ubora au uhakiki wa usalama wake:-

Kutokana na kuwa makasuku wa tafiti za wazungu, tumeendelea kwa kiasi kikubwa kutegemea madawa yao. Viwanda vya ndani vilivyopo nchini kama vile "shellys" havina uwezo wa kuzalisha madawa toshelevu au stahiki kutokana na utaalamu duni, rasilimali hafifu na teknolojia isiyokidhi viwango.

Pamoja na uwepo wa taasisi za udhibiti wa ubora wa madawa nchini kama vile TMDA bado madawa yasiyo na ubora nchini yameendelea kuingia na kuwadhuru watu wetu. Madawa kama vile 'Quinine' na 'Chloroquine' ambayo baadaye yaligundulika kusababisha madhara makubwa kama vile uziwi wa kudumu yaliingizwa nchini na kuthibitishwa na TMDA.

Je, usalama wa taifa waweza kuwa mashakani? TAFAKARI.

3. Kushindwa kudhibiti magonjwa ya milipuko au "pandemics":-

Mwaka 2020 mpaka mwaka 2021, ilithibitika palipo shaka kwamba, Tanzania hatukuwa na utaalamu wa kupambana na gonjwa la corona. Hapakuwa na tiba yoyote madhubuti ya kisayansi katika kutibu walioathirika au kuwakinga wale walio katika hatari ya maambukizi. Mpaka pale wazungu walipotuletea chanjo zao ndipo na sisi tukakurupuka kuzikumbatia kwa kasi. Huu ni ukasuku, kuvamia vamia na kuigiliza bila kuwajibika sisi wenyewe.

Endapo wazungu wakashindwa kutuletea madawa au chanjo katika magonjwa ya dharura na ya milipuko, ni wazi taifa litateketea na kuangamia lote. Hapatakuwa na watu wa kutuokoa, maana tuliowakabidhi dhamana hawana uwezo wala nyenzo. Tujitafakari.


3. Mitaala na kanuni za kitabibu isiyoruhusu ufikiri nje ya boksi:-

Mitaala iliyoandaliwa kwa ajili ya wanafunzi wa utabibu na wale wa masomo ya sayansi pamoja na kanuni zake zote ni BAPA isiyoweza kunyumbulika ili kumruhusu daktari au mwanasayansi kufikiri kwa upeo mpana nje ya yale aliyofundishwa darasani au nje ya miongozo yake ya kutoa tiba au kazi zingine za kitabibu.

Watabibu wamezungukwa na kanuni nyingi za kisheria pamoja na bodi za kitaaluma kama vile 'Baraza la Madaktari la Tanganyika', 'Baraza la Wafamasia' na vyombo vingine vya udhibiti ambavyo vinamfanya daktari kuwa kasuku badala ya mbunifu. Tabibu haruhusiwi kutoa tiba nje ya miongozo hata kama mazingira husika hayafai kutumia miongozo hiyo la sivyo anafutiwa leseni ya utabibu.

Hii si kusema miongozo ni mibaya, la hasha, miongozo ni nyenzo muhimu isipokuwa pawepo na fursa ambayo matabibu wataruhusiwa kujenga ubunifu katika kazi zao ili kuwawezesha kuleta utofauti pale ambapo hakuna majawabu sahihi ndani ya miongozo iliyowekwa.

NINI KIFANYIKE:

Yafuatayo nashauri yachukuliwe hatua na kufanyiwa kazi:-

1. Kutengwa kwa bajeti maalumu na toshelezi katika kuendesha tafiti za kisayansi za kweli na zenye dhamira ya dhati:-

Natoa changamoto kwa wizara ya afya kuja mikakati madhubuti na endelevu katika kufanya tafiti za kila mwaka dhidi ya magonjwa yote hususani magonjwa sugu yasiyotibika.

Bajeti inayotolewa sasa kwa ajili ya tafiti si bajeti inayokidhi au kuonesha kuwa tuna nia ya dhati. Wizara haijaonesha mahali popote kuwa itaenda kuendesha tafiti dhidi magonjwa yanayosemekana kuwa 'hayana tiba". Nashauri wizara kutenga bajeti maalumu na kuja na mikakati madhubuti.

2. Kutoa motisha kwa ugunduzi na ubunifu wa tiba za magonjwa:-

Motisha ya kifedha au bakshishi ni nyenzo madhubuti katika kuwainua na kuwaibua watu binafsi, taasisi, na wanasayansi ili wahamasike kuja na majawabu ya magonjwa yanayotusumbua. Kuwatambua na kuwahamasisha inaweza kuwa mojawapo ya njia muhimu. Tuitumie.

3. Kuimarisha uwezo na meno ya NIMR:-

NIMR ni mojawapo ya taasisi za tiba asili nchini yenye mamlaka ya kisheria na ya kitabibu katika kutoa tiba mbadala na za asili. Kwa bahati mbaya taasisi hii ni butu na haitiliwi maanani, hata bajeti yake haizingitiwi ipasavyo. Ni muhimu na lazima kujenga uwezo wa NIMR ili ufanisi wake na tija yake ionekane katika kutoa suluhisho la magonjwa sugu.


3. Kujenga uwezo wa viwanda vya madawa nchini:-

Viwanda vya ndani vya madawa kama vile "shellys" havina uwezo wa kisayansi na kiteknolojia kuweza kushindana na viwanda vya mataifa ya nje. Jambo hili linasababisha kubweteka kwa wataalamu wetu wa ndani na badala yake wamegeuka kuwa madalali wa madawa na chanjo kutoka nchi zingine.

Serikali ione ulazima na wajibu wa kuwawezesha wataalamu wetu kifedha na kiteknolojia ili waweze kuwajibika kikamilifu.

Matabibu na wanasayansi nchini ni uti wa mgongo wa afya za watanzania. Wao ni chumvi ya taifa!

Je, chumvi ikiharibika itatiwa nini ili ikolee? TUTAFAKARI.

Wasaalam!
 
Upvote 3
Ndugu mwandishi naheshimu maoni yako lakini ningekushauri uifuatilie vizuri kabla hujaandika
Hivi unajua kwamba ni Tanzania pekee ambapo mgonjwa wa marbug amepona? Na ametibiwa na wataalamu wazawa wa kitanzania?
Kwa nn unakuwa na mtazamo hasi tu kwa wataalamu wetu?
Kwani hao wazungu wenye pesa za utafiti wameweza kuitibu saratani? Unafikiri wao na wataalamu wa saratani wa kitanzania wamelala?
 
Back
Top Bottom