| Imeandikwa na: Dr.Henry Mayala Jr Mnamo: Mar 29 |
Mojawapo ya tatizo linaloathiri jamii katika nchi nyingi zinazoendelea ikiwemo Tanzania ni magonjwa yanayohusiana na minyoo. Duniani kwa ujumla, takribani watu billion moja wameripotiwa kuwa na uvamizi wa minyoo aina ya helminthes kwenye miili yao.
Minyoo huenezwa kwa njia zipi?
Minyoo huenezwa pale maji au chakula vinapokuwa vimeathiriwa na mayai au mabuu ya minyoo. Hali kadhalika, uwezekano wa kupata minyoo huchangiwa pia na kutonawa mikono kabla ya kula na baada ya kutoka kujisaidia haja kubwa. Aidha watoto wadogo chini ya miaka mitano ambao hupenda kuchezea mchanga au uchafu kwa ujumla na ambao hupendelea pia kunyonya vidole nao pia huambukizwa kwa urahisi. Mambo mengine yanayochangia katika kupata uvamizi wa minyoo ni pamoja na kuishi katika mazingira machafu, kutembea bila viatu (pekupeku) na kula vyakula ambavyo havijaiva au visivyopikwa vizuri (undercooked foods).
Aina za minyoo na madhara yake kwa binadamu
Kuna aina kadhaa za minyoo ambazo, ukiachilia mbali kuwashambulia wanyama wengine kama ngombe, nguruwe, mbuzi na kondoo, humshambulia pia binadamu. Aina hizi ni pamoja na
- Minyoo jamii ya round worms kwa mfano Ascaris lumbricoides ambao husababisha utumbo kuziba (intestinal obstruction) au uambukizi katika kidole tumbo (appendicitis)
- Minyoo jamii ya hook worms kwa mfano Ancylostoma duodenale ambao huishi kwa kunyonya damu kwenye utumbo mdogo na hivyo kusababisha upungufu wa damu mwilini.
- Minyoo jamii ya pin worms au thread worm kwa mfano Enterobius vermicularishusababisha kuwashwa hasa sehemu za haja kubwa kwa sababu ya mcharuko mwili unaotokana na minyoo hii kutoa mayai yao eneo hilo hasa kipindi cha usiku.
- Minyoo jamii ya whip worms kwa mfano Trichuris trichiura husababisha kinyesi kuchanganyika na damu, kupungua uzito, upungufu wa damu na kutoka nje kwa puru (rectal prolapse).
- Minyoo jamii ya tegu (tape worms) kama vile Taenia solium husababisha kifafa pindi wanapovamia ubongo hasa katika hatua ya ukuaji iitwayo cystercosis
Dalili za minyoo ni zipi?
Dalili za kuwepo kwa uvamizi wa minyoo mwilini hutegemea sana aina ya minyoo inayomuathiri mgonjwa. Lakini kwa ujumla, dalili ni pamoja na
- Maumivu ya tumbo
- Kupata choo kigumu sana
- Kuharisha
- Kujisikia mchovu na mlegevu kutokana na kupungukiwa damu
- Kupoteza hamu ya kula
- Tumbo kuwa na gesi na kuhisi limejaa
- Kukohoa na kupiga chafya
- Kwa watoto kusugua meno, kujipinduapindua pamoja na kujikojolea kitandani
- Kichwa kuuma au kupata kifafa kama minyoo (jamii ya taenia solium) ikitaga mayai yake kwenye ubongo
- Kuwashwa, na
- Huathiri ukuaji kwa watoto
Utatambuaje kama umeathiriwa na minyoo?
Vipimo vinavyoweza kusaidia kugundua uvamizi wa minyoo, aina zake na hata madhara yaliyosababishwa na minyoo ni pamoja na:
- Kupima choo kikubwa (Stool examination) kwa ajili ya kuchunguza mayai na mabuu ya minyoo iliyo katika haja kubwa kwa kutumia darubini
- Kupima damu (Complete blood count) huku mkazo zaidi ukiwa kwenye Eosinophil na kiwango cha damu (Hb). Iwapo kuna uvamizi wa minyoo, kiwango cha Eosinophil huwa juu zaidi kuliko kawaida.
- X-ray yaweza kusaidia kuchunguza hatua mojawapo ya ukuaji wa minyoo ya Taenia solium iitwayo cystercosis katika ubongo au paja.
- CT na MRI pia zaweza kurahisisha kugundua na kutambua cyst (vifuko vyenye majimaji) za minyoo aina ya hydatid ambayo huvamia ini, ubongo, figo na sehemu nyingine za mwili.
- Kipimo cha puru (proctoscopy) husaidia kutambua uvamizi wa minyoo aina ya trichiuris trichiura kwenye puru.
Minyoo inatibika?
Bila shaka kabisa, minyoo inatibika. Dawa zifuatazo hutumika katika kutibu minyoo kulingana na aina ya minyoo inayomuathiri mgonjwa
- Mebendazole hutumika kutibu zaidi uvamizi wa minyoo aina ya round worms
- Albendazole yaweza kutibu minyoo aina ya tegu (tape worms) pamoja na hydatid
- Ivermectin hutumika kutibu aina mbalimbali za minyoo
- Ketrax (levamisole) nayo pia ina uwezo wa kutibu aina kadhaa za minyoo
- Piperazzine pia ina uwezo wa kutibu aina nyingine nyingi za minyoo.
Hata hivyo, tunashauri sana matumizi ya dawa hizi hasa kwa watoto, yafanyike mara baada ya kupata ushauri wa daktari na si vinginevyo.
Inawezekana kujinga dhidi ya uvamizi wa minyoo?
Njia za kujikinga na minyoo ni pamoja na
- Kuishi katika mazingira safi.
- Kunawa mikono na sabuni baada ya kutoka msalani na kabla ya kula
- Kukata kucha (kucha ndefu huweza kutunza uchafu)
- Kuwa muangalifu hasa unapokuwa na wanyama kama paka na mbwa
- Kutumia dawa za kuzuia uvamizi (deworming) kila baada ya miezi mitatu au sita
chanzo Fahamu kuhusu Minyoo (Helminthesis) – TanzMED(old) - Afya Kwa Wote