- Source #1
- View Source #1
- Source #2
- View Source #2
Wakuu,
Nimekuja na swali hili baada ya jamaa mmoja kusema jambo hili sio la kweli, lakini mimi pia nimeshawahi sikia hii, bi mkubwa alituhadisia kuna ndugu yao mmoja aling'atwa na mbwa mwishowe alipokaribia kwenda kwenye ulimwengu mwingine alikuwa akibweka kama mbwa. Naamini hata wewe unayesoma hapa umeshawahi kusikia kuhusu hili.
Je, suala hili ni kweli au stori tu za mtaani wataalamu wa JamiiCheck?
Nimekuja na swali hili baada ya jamaa mmoja kusema jambo hili sio la kweli, lakini mimi pia nimeshawahi sikia hii, bi mkubwa alituhadisia kuna ndugu yao mmoja aling'atwa na mbwa mwishowe alipokaribia kwenda kwenye ulimwengu mwingine alikuwa akibweka kama mbwa. Naamini hata wewe unayesoma hapa umeshawahi kusikia kuhusu hili.
Je, suala hili ni kweli au stori tu za mtaani wataalamu wa JamiiCheck?
- Tunachokijua
- Mbwa ni mnyama wa familia ya Canidae, aina moja ya mbwa mwitu ambaye amefugwa na binadamu kwa maelfu ya miaka kwa kazi, ulinzi, michezo, na kama mnyama wa kufugwa. Mbwa wana tofauti za ukubwa, rangi, umbo, na tabia, na wamekuwa marafiki wa karibu wa binadamu kwa muda mrefu. Wana uwezo mkubwa wa kujifunza na kuelewa maelekezo ya binadamu na wanaweza kushiriki katika shughuli mbalimbali kama vile uwindaji, kutafuta watu, na kuwa pamoja na familia kama wanyama wa kufugwa.
Pamoja na uzuri wa mnyama huyu kwa binadamu, Mbwa huweza kukabiliwa na magonjwa mbalimbali ambayo ni hatari kwake na ni hatari kwa binadamu. Miongoni mwa magonjwa hatari zaidi kwa binadamu ni pamoja na kichaa cha mbwa.
kichaa cha mbwa ni ugonjwa wa kuambukiza unaoathiri mfumo wa kati wa fahamu yaani ubongo na Ugwe mgongo na kupelekea kupooza, kupoteza fahamu au kifo. Ugonjwa huu ni hatari na husabishwa na virusi Rabies. Vijidudu hivi vinapatikana katika mate au damu ya binadamu na wanyama wengine kama mbwa, mbweha, paka, popo n.k.
Kumekuwa na hoja katika jamii inayodai kuwa ikitokea binadamu ameng'atwa na mbwa mwenye kichaa huathirika na kubadilika kufikia kiwango cha kuanza kubweka kama mbwa.
Je, ni kweli uking'atwa na mbwa mwenye kichaa utabweka kama mbwa?
JamiiCheck imepitia vyanzo mbalimbali ikiwamo Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (CDC) na Tovuti ya Abiteafya.com ambapo zote zinaelezea athari ya virusi vya kichaa cha mbwa kwa binadamu. Vyanzo vyote kwa ujumla vinafafanua namna virus vya kichaa cha mbwa vinavyoathiri mfumo wa mwili wa binadamu hasa eneo ubongo na kumfanya awe na mwenendo tofauti wa kimatendo pamoja kutoa sauti zisizo za kawaida.
Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (CDC) wanaeleza hatua kwa hatua za mtu aliyeng'atwa na kuingiwa na virusi vya mbwa kichaa huonesha dalili na mpaka mwisho kuonesha tabia zisizo za kawaida. Wakifafanua kwa kina jambo hili CDC wanasema:
Baada ya virusi vya kichaa cha mbwa kuingia kwnye mwili wa binadamu hukimbilia kwenye ubongo kabla ya kuonesha dalili za kwanza. Muda huu unaweza kudumu kuanzia wiki mpaka mwezi kutegemea na umbali wa jeraha na ubongo. Dalili za kwanza za kichaa zinaweza kuwa homa, kupata udhaifu au kutokujisikia vizuri, maumivu ya kichwa. Dalili hizi zinaweza kudumu kwa siku kadhaa. Kisha dalili hizi hukua na kuathiri ubongo wa mgonjwa. Halii hii hupelekea kuibuka kwa hali ya wasiwasi na mgonjwa kuanza kuchanganyikiwa. Kadiri ugonjwa unavyoendelea, mtu anaweza kupata wazimu, tabia isiyo ya kawaida, ndoto za mchana, hydrophobia (hali ya kuogopa maji), na kushindwa kulala. Kipindi cha ugonjwa kinaishia kawaida baada ya siku 2 hadi 10 ugonjwa huu kwa kiwango kikubwa unaua, mpaka sasa kuna kesi zisizozidi 20 za watu kupona baada ya kuugua. Pamoja na kuwa andiko la CDC linabainisha namna virusi vya kichaa cha mbwa kinavyoweza kumfanya mgonjwa kuwa na tabia zisizo kawaida lakini andiko haliweki bayana ikiwa tabia hizo zinajumuisha mgonjwa kubweka kama mbwa.
Kwa upande wao AbiteAfya.com wanadokeza kwa ufupi kuhusu kuwepo kwa dalili ya mtu aliyeingiwa na virusi hivi kubweka kama mbwa. Katika andiko hilo wanasema:
Wengi wetu dalili ambayo huwa tunaijua ya kichaa cha mbwa ni ile hali ya kubweka kama mbwa lakini hatujui kwamba hiyo ni dalili ya baadaye kabisa.Kichaa cha Mbwa (Rabies) ni ugonjwa ambao huwa hauzungumziwi sana lakini naweza kusema ni jinamizi lililonyamaza. Sifa yake kuu ni hii Ukishapata dalili za kichaa cha mbwa ndio basi tena, hakuna dawa! Ni ugonjwa unaoua kwa asilimia 100, lakini cha ajabu ni ugonjwa unaoweza kuzuiliwa (prevention) kwa asilimia 100 pia. Hadi sasa ni watu 20 tu, dunia nzima, walioripotiwa kupona baada ya kuambukizwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa, na mmoja wapo ni mwanadada anayeitwa Jeanna Giesse (35).Makala hii imetaja tu kuhusu kuwepo dalili ya aliyeshambuliwa na mbwa kichaa kubweka lakini haijaingia kwa kina kama dalili hii hutokea kwa kila muathirika au la. Lakini inatusaidia kutupa mwanga kwamba suala hili linajitokeza kwa baadhi ya waathirika. Hata hivyo mawazo yaliyotolewa na makala hii yanafanana na mawazo yaliyoandika katika gazeti la Punch ambao wao wanadai baadhi ya vipo baadhi ya visa vya wagonjwa walioshambuliwa na mbwa kuonekana wanabweka kama mbwa.
Kwa upande wao tovuti ya The Economic Times wanakanusha virusi vya kichaa cha mbwa kumsababishia muathirika kubweka. Wanaeleza namna virusi hivyo vinavyoathiri ubongo na sauti ya mtu. Ktika kufafanua jambo hili wanasema:
Virusi vya kichaa cha mbwa (rabies) havimfanyi muathirika kubweka. Hata hivyo, inaweza kuathiri neva na kuleta dalili mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wasiwasi na kuchanganyikiwa, na utoaji wa sauti zisizo za kawaida. Dalili hizi ni sehemu ya maendeleo ya ugonjwa na sio sifa ambayo inajitokeza kwa kila muathirika.JamiiCheck imezungumza na Dkt. Jofrey Josia, Mtaalamu wa Mifugo Kutoka Goba, Veterinary clinic ambaye ameeleza kuwa si kweli kuwa mtu akipata kichaa cha mbwa huwa anabweka bali kutokana na mfumo wa neva za fahamu kuwa umeshaathirika na virusi basi mtu huyo anakuwa hawezi kutamka maneno yanayoeleweka, anakuwa anatoa sauti zisizoeleweka na hali hiyo watu huichukulia kama kubweka lakini si kweli kwamba mtu huyo anabweka kama mbwa.
"Mtu aking'atwa na mbwa ambaye ana kichaa, kinachotokea cha kwanza ni wale virusi kwa sababu kichaa ni ugonjwa wa virusi, wanaingia kwenye mwili wa mwanadamu ukishaingia unaanza kusambaa taratibu kupitia kwenye neva mpaka pale unapofika kwenye ubongo.
Sasa sisi tunaanza kuona dalili za kichaa mpaka pale unapokuwa umefika kwenye ubongo, kwa maana ya mfumo mzima wa fahamu kwa maana wanapenda kushambulia mfumo mzima wa fahamu.
Sasa wakishafika kwenye mfumo wa fahamu ndio tunaanza kuziona zile dalili ambazo mara nyingi, dalili moja wapo ni hallucination, hallucination ni ile hali ya kuhisi kama umeitwa lakini hujaitwa au unahisi kama mtu kakugusa lakini hajakugusa.
Ambazo hizo dalili wakati mwingine huwa zinatokea kwa mbwa, Sasa wakati mwingine unakuta mtu anatamka maneno ambayo yanakuwa hayaeleweki kwa sababu kunakuwa hakuna muunganiko wa ubongo, ubongo unakuwa hauko katika uwiano mzuri, umeshashambuliwa na kuathirika.
Wakati mwingine anakuwa anatamka maneno ambayo yanakuwa hayaeleweki, sasa ile ndio watu wanaiita kama kubweka lakini kimsingi wanakuwa hawabweki, lakini wanakuwa wanatoa sauti ambazo hazieleweki kwa sababu hawezi kutamka neno vizuri kwa kuwa mfumo wa ubongo umeshaathirika na hicho ndicho kinachotokea.
Je, Inachukua muda gani kuonesha dalili za kichaa tangu alipong'atwa?
Dkt. Jofrey Josia anaeleza, Inatokana na vitu vingi. Cha kwanza inategemea na eneo alipong'atwa, uking'atwa mguuni wale virusi wanasafiri taratibu hivyo watachukua muda mrefu kufika kwenye ubongo.
Uking'atwa shingoni wale virusi watasafiri haraka kwa sababu shingo iko karibu na ubongo.
Kwa hiyo inategemea umeng'atwa wapi, ndio maana kuna watu wanang'atwa mpaka walishasahau kabisa kama waling'atwa na mbwa ndipo wanakuja kupata dalili za kichaa.
Cha pili, ni kiwango cha virusi waliongia kwenye mwili wako.
Aina ya virusi waliongia kwa sababu virusi wapo wa aina tofauti tofauti wa kutoka maeneo tofauti tofauti.
Kinga ya mtu mwenyewe binafsi, kinga ya mwili wako inapambana kiasi gani hizo ndio sababu zinaweza kufanya uoneshe dalili kwa muda gani mapema au kwa kuchelewa zaidi".
Je, Mtu akifikia hatua ya kuonesha dalili anaweza kupona?
Dkt. Jofrey Josia anaeleza, Hapana, mtu akishaonesha dalili za kichaa hawezi kupona, kwa sababu virusi wanakuwa wameshaenda mpaka kwenye ubongo na anakuwa hawezi tena kupona.
Tunachokifanya mtu akiwa ameng'atwa na mbwa mwenye kichaa huwa tunampatia chanjo haraka sana, ile chanjo ya kichaa cha mbwa na hiyo inatakiwa apatiwe muda mfupi baada ya kuwa ameng'atwa siku ya kwanza siku ya 3, siku ya 5, siku ya 14 na siku a 90
Kwa hiyo anapata chanjo ya kichaa kwa ajili ya kuzuia wale virusi wasiingie mwilini.
Cha pili, kuosha kidonda kwa maji na sabuni yanayotiririka, lakini atatakiwa kutia dawa pale na taratibu nyingine za kimatibabu kulingana na ushauri wa daktari
Iwapo mtu ameng'atwa na mbwa mwenye kichaa na amechelewa kupata chanjo na wale virusi wakasambaa wakafika mpaka kwenye ubongo, hakuna namna mtu huyo anaweza kupona"
Vipi kuhusu paka uliyemzungumzia naye anapata virusi kama wanaopatikana kwa mbwa?
Ndio, paka anapata virusi, sema mara nyingi kitabia paka hashambulii kama mbwa ndio maana siyo maarufu sana, lakini paka naye anapata virusi na anaumwa na hiyo iko kitaalam kabisa, kimsingi wanyama wote wanapata kichaa ila ni kichaa cha mbwa na yuko maarufu kwa kuwa wanyama wengine hawana tabia ya kung'ata na hawako karibu na binadamu kiasi cha kumng'ata kama mbwa na hawashambulii sana kama mbwa na hawako karibu sana kumng'ata au kumsababishia madhara.
Hivyo kama una paka tunakushauri umchanje kuzuia kichaa
Kulingana na majibu ya daktari na tafiti mbalimbali Jamiicheck imejiridhisha kuwa taarifa za mtu aliyepata kichaa cha mbwa kubweka hazina ukweli wowote.