Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,809
- 15,421
Kifo hakina muda wala siku, hakina saa wala dakika. Kifo hakina mahali wala eneo, bali hutokea popote. Leo hii unaweza kudhani utafia Tanzania, ukajikuta umefia kwenye misitu ya Amazon. Hata hivyo, inaelezwa hivi sasa kwamba, kwa baadhi ya hali au mazingira, mtu anaweza kujua atakufa lini.
Watu wenye kiharusi waliolazwa mwishoni mwa wiki kwa mfano, inaelezwa kuwa, wana uwezekano mkubwa zaidi wa kufariki dunia kuliko wale ambao wamelazwa katikati ya wiki. Najua unaweza kusita kukubaliana na kauli kama hii, lakini kwa bahati mbaya siyo kauli yangu. Hii ni kwa mujibu wa utafiti toka Canada. Utafiti huo uliwafuatilia watu waliokufa kutokana na ugonjwa wa kupooza katika hospitali 606 za nchini Canada toka Aprili 2003 hadi Machi 2004. Lakini, pia hata katika nchi changa imeonekaa kuwa kiharuisi kikali kinachomtokea mtu siku za wikiendi huuwa zaidi kuliko kikitokea siku za kawaida za wiki.
Baada ya kuchukua vigezo vingine ikiwa ni pamoja na umri, jinsia, magonjwa mengine, na mambo yafananayo na hayo, waliopata kiharusi na kulazwa mwishoni mwa wiki walikuwa na uwezekano mkubwa wa kufa kwa asilimia 13 kuliko wale ambao walilazwa katikati ya wiki. Utafiti hauoneshi kwa uhakika kwa nini vifo vya waliopata kiharusi, vinaongezeka mwishoni mwa wiki. Lakini watafiti, ikiwa ni pamoja na Gustavo Saposnik, wa Chuo Kikuu cha Toronto, Canada katika kitengo kinachojihusisha na matatizo ya kiharusi, walitoa maoni kwamba idadi ya madaktari na wauguzi mwishoni mwa wiki ni ndogo na hivyo kuwa na huduma hafifu.
Upungufu wa rasilimali, ujuzi, na huduma bora kwa wagonjwa mwishoni mwa wiki unajionesha wenyewe kwa kusababisha vifo vingi. Hivi ndivyo watafiti hao wanavyosema. Lakini, kwa nchi zinazoendelea, jambo au mambo kama haya ndiyo yanaweza kutazamwa kama tatizo kubwa kiasi hicho. Inaonesha kuwa, katika nchi changa, mtu anapopigwa na kiharusi kikali siku ya wikiendi, anakuwa kwenye nafasi kubwa zaidi ya kufariki ukilinganisha na yule ambaye, amepigwa na kiharusi hicho siku za kawaida za wiki. Kwa nchi changa kama Tanzania, huenda hili la hospitali kuwa shaghalabaghala siku za wikiendi linaweza kuwa na nguvu. Kwa nchi tajiri inatia mashaka.
Lakini, huenda pia ni kwa sababu, wakati wa wikiendi, watu wengi huwa kwenye nafasi ya kujiumiza zaidi kimawazo, kutokana na kupungukiwa na kazi, ambazo huwa zinawafanya wawe bize, hivyo kutowaza sana na kupalilia kiharusi. Ukweli ni kwamba, mtu akipigwa na kiharusi Jumamosi au Jumapili, hasa Jumapili, uwezekano wa kufa ni mkubwa kuliko kama angepigwa siku nyingine. Lakini, ukweli mkubwa zaidi ni kuwa, haijafahamika hasa ni kwa nini. Sababu mbili zilizotolewa hazikidhi kuelezea mazingira ya jambo hili. Kiharusi ni ugonjwa wa tatu nchini Marekani unaosababisha vifo, ukiuwa zaidi ya watu 150,000 kwa mwaka. Kiasi cha watu 700,000 Marekani hupata kiharusi kwa mwaka – ni kama pigo moja katika kila sekunde 45, kwa mujibu wa Chama cha Kiharusi cha Marekani.
Hakuna takwimu toshelevu kwa tatizo hilo hapa nchini, lakini limekuwa likikua kwa kasi kubwa sana. Kiharusi hutokeaje? Hutokea hivi: Mshipa upelekao damu kwenye ubongo hupasuka. Damu ikishakauka inazuia damu isitiririke kwenda kwenye ubongo. Kuna sababu nyingi ni kwa nini mishipa ya damu inaweza kupasuka. Vifo vitokanavyo na kiharusi vinaonekana kuwa juu zaidi mwishoni mwa wiki kuliko katikati ya wiki (Asilimia 8.5 ya wagonjwa wanaolazwa mwishoni mwa wiki wanakufa, ikilinganishwa na asilimia 7.4 ya wale wanaolazwa katikati ya wiki).
Dalili za kuonesha kwamba mtu anakabiliwa na kiharusi, kwa maana yuko karibu kukumbwa nacho, ni:
Kwanza, udhaifu wa mwili wa ghafla au kuhisi ganzi usoni, kwenye mkono, au mguu upande mmoja wa mwili.
Pili, kutoona vizuri kwa ghafla, kupungukiwa nguvu, kuyumba utembeapo, mwili kutohisi kitu hata baada ya kuguswa, sauti kukauka, au kupungua kwa uwezo wa kuelewa kauli zinazotolewa na mtu mwingine.
Tatu, maluweluwe ya ghafla kwenye macho, hasahasa kwenye jicho moja.
Nne, kuyumbayumba kwa ghafla, wakati mwingine ikiandamana na kutapika, hali ya kichefuchefu, homa , kwikwi, au shida katika kumeza.
Tano, kuumwa kichwa vibaya na kwa ghafla bila chanzo kingine chochote , ikifuatiwa kwa haraka na kupotelewa fahamu.
Sita, kupotelewa na fahamu kwa kipindi kifupi. Pia kizunguzungu kisichoelezeka au kuanguka kwa ghafla.
Yeyote atakayeziona dalili hizo au akimwona mwenzie akionesha dalili hizo hana budi kutafuta msaada mara moja kuliko kusubiri kuona dalili hizo zinaondoka zenyewe. Dalili hizi hata hivyo, si kila wakati zinaonesha kwamba mtu anakaribia kupigwa na kiharusi, lakini hatari za kusubiri kujua chanzo chake ni nini, ni kubwa mno kwani kwa kufanya hivyo unaweza kupoteza maisha ya jamaa yako au ya mtu wako wa karibu.