Ukipendwa kwa pesa, utaachwa kwa kuzikosa

Ukipendwa kwa pesa, utaachwa kwa kuzikosa

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Joined
Nov 22, 2012
Posts
1,985
Reaction score
1,286
Katu hapandi Farasi, yule mzoea Punda,
Mpenda kwenda kasi, mwendo pole humshinda,
Amezoweshwa fenesi, doriani lamshinda,
Sitokalifisha nafsi, nafanya ninayopenda,
Loo! Nina wasiwasi, kwa mambo yanavyo kwenda.

Moyo una wasiwasi, akili i'njia panda,
Huyu mja Ibilisi, ni jini msaka tenda,
Kila siku alhamisi, kwake siku huganda,
Si kuna siku nyepesi, na za kukaza mkanda?
kuna siku za mafurusi, na za mifuko kukonda.

Hili jua la utosi, kila mja humtenda,
Hata mwenye ukwasi, pia laweza mponda,
Ya jini kuhama rasi, mkiti anapo konda,
Mwayaiga pasi wasi, ya majini mwayatenda,
Kwa tindo na bisibisi, mioyo mnaitinda.

Sina hofu sina wasi, tena nenda mwana kwenda,
Kitu changu kimepasi, hakiyumbi kimedinda,
Hupati tena nafasi, dagaa zangu kutanda,
Umeshakuwa unyasi, nyoka alonipa donda,
Nimestuka kirahisi, we endelea kutanda.

Wengi wapo kifurusi, hawana kitu kupenda,
Huu wangu msindusi, natafuta pa kupanda,
Asojali mafurusi, ndo nitakaye mpenda,
Mwenye kujali nafsi, mafurusi kuyaponda,
Mapenzi ya wasiwasi, wallahi ni kama donda.

Niko na pepo za kusi, ni mbali ninapo kwenda,
Mapenzi ya wasiwasi, naona yamenishinda,
Wenye kupendwa wakwasi, shida nzito huzishinda,
Sina kazi na ofisi, yakwangu yananishinda,
Mkono wangu mwepesi, yu wapi wa kunipenda?

Nipe pombe ya kiasi, nipate ipiga funda,
Na miraa ya Ramisi, kwa ubani naifunda,
Initoe wasiwasi, hata kipoe kidonda,
Niupate na wepesi, wa kumkabili nyonda,
Hivi ni kitu rahisi, kutamka "nakupenda"?


Njano5.
0762845394
 
Back
Top Bottom