Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Kuna taarifa za kustusha kuhusiana na upatikanaji wa damu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH). Hali ni mbaya. Inaelezwa kuwa hivi sasa, hospitali hiyo ambayo ni ya rufaa ya taifa imekuwa na uhaba mkubwa wa damu na hivyo kutishia uhai wa wagonjwa wengi wenye kuhitaji huduma ya kuongezewa damu.
Msemaji wa hospitali hiyo alikaririwa na gazeti hili jana akikiri kuwapo kwa tatizo hilo, akieleza kuwa kati ya chupa 100 zinazohitajiwa kuwapo kila uchao ili kukidhi mahitaji ya wagonjwa, wao wamekuwa na chupa kati ya 50 hadi 65 tu. Matokeo yake, mara zote wamekuwa wakitoa damu hiyo kwa wagonjwa wa dharura tu.
Hali hiyo ya ukosefu wa damu ilithibitishwa vilevile na Meneja wa Taifa wa Mpango wa Damu Salama, aliyesema kuwa mwamko wa wananchi kuchangia damu umekuwa mdogo na hivyo, wao hujikuta wakiwa na chupa 160,000 tu badala ya 450,000 zinazohitajika kukidhi mahitaji.
Hakika, taarifa hii siyo njema hata kidogo. Ni janga kubwa kwa taifa. Hii inatokana na ukweli kuwa hospitali ya Muhimbili, ndiyo kubwa kuliko zote nchini. Inapaswa kuwa kimbilio la Watanzania wote pindi panapokuwa na ulazima wa rufaa kwa mgonjwa aliyeshindwa kutibiwa katika hospitali nyingine kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za ukosefu wa vifaa tiba vya kisasa, dawa na hata madaktari bingwa wenye uzoefu wa kutosha kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Kutokana na ukubwa wake, na umuhimu wake kwa kila Mtanzania, hospitali hii ya umma haitazamiwi hata kidogo kukutwa ikiwa na matatizo ya kukosa vifaa tiba vya msingi vya hospitali ya hadhi yake, kukosa watalaamu au dawa za msingi. Ni kwa kutambua hilo, ndipo nasi tunapoona kuwa tatizo hili la damu ni la kufedhehesha kwa kiasi kikubwa.
NIPASHE tunachukulia kuwa tatizo hili ni la aibu na fedheha kutokana na ukweli kwamba damu ipo na upo uwezekano wa kuipata kwa wingi kutoka kwa Watanzania wenyewe. Jambo pekee linalotakiwa kufanywa ni kuendesha kampeni endelevu za kuhamasisha umma ili ujitolee kuchangia damu pasi.
Madai kwamba umma haujahamasika hayapaswi kupewa nafasi ya kuhalalisha hali mbaya iliyopo Muhimbili na kwenye hospitali nyingine nchini. Bali, ni dalili kwamba kuna baadhi ya watu waliopewa dhamana ya kusimamia jambo hili bado hawajawajibika ipasavyo.
Ikumbukwe, uhai wa kila Mtanzania ni muhimu kuliko maelezo ya aina yoyote ya kutetea kuwapo kwa hali mbaya ya upatikanaji wa damu. Tunaamini kwamba damu ipo, na wachangiaji wanaweza kuwapo wengi kuliko hata malengo ya benki za damu za taasisi zetu. Isipokuwa, jambo muhimu ni kuhakikisha kwamba kampeni za kuhamasisha umma zinakuwa endelevu. Ubunifu pia unahitajika katika kuhakikisha kwamba watu wote wenye sifa ya kuchangia damju wanafikiwa na mwitikio wao mara zote unakuwa chanya.
Hatuamini kwamba uhamasishaji katika kuchangia damu unafanyika vizuri. Mathalan, idadi ya vyuo vikuu vilivyopo nchini peke yake, ambavyo sasa ni zaidi ya 50, vinatosha kuwa chanzo kizuri cha upatikanaji wa damu.
Zipo pia taasisi nyingine za elimu ya juu zaidi ya mamia zinazoweza kuwa sehemu muhimu ya uchangiaji wa damu, achilia mbali vyuo vya ufundi stadi (Veta), shule za sekondari na kambi za majeshi yetu. Taasisi za dini ni muhimu pia kushirikishwa katika kampeni hii. Masheikh, maaskofu na wachungaji ni watu muhimu, wenye umati mkubwa wa waumini nyuma yao. Hawa wakishirikishwa vizuri, wanaweza kuwa kiungo muhimu cha kusaidia upatikananji wa damu kutoka kwa mamilioni ya Watanzania.
Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, pamoja na Watanzania wote, ni lazima sasa kufuta kabisa hisia za kusubiri ufadhili hata katika jambo muhimu na lililo ndani ya uwezo wetu kama hili la kuhamasisha umma kuchangia damu. Ni kwa sababu tukiingia katika mtego wa kusubiri ufadhili, tutashindwa kuwakoa wapendwa wetu wenye kuhitaji damu. Na sisi wenyewe tutaendelea kujiweka katika hatari ya kupoteza maisha kwani kila mmoja, katika muda usiojulikana, anaweza kuhitaji damu ili kuokoa maisha yake.
Isitoshe, ni aibu kupoteza watu wetu kwa sababu ya kukosa damu ambayo hatuiagizi kutoka nje bali tunayo wenyewe miilini mwetu. Tujiepushe na fedheha hii.
CHANZO: NIPASHE