Ukweli kuhusu ndoto usingizini.

badshah

Member
Joined
Mar 16, 2013
Posts
51
Reaction score
32
Fikra za mtu huendelea kuzunguka katika ubongo kila siku kutokana na aliyoyaona, kuyasikia na mengineyo. Na kuna fikra ambazo hujitengeneza zenyewe katika akili ya mwanadamu, na hii inatokana na hamu ya kitu, furaha, huzuni, wasiwasi, hofu, uwoga n.k.

Kumbuka kuwa ile hali ya ubongo kuwa inaegemea sana katika kufikiria kitu fulani basi huleta athari sana hata unapokuwa usingizini, unaweza kuwa unafikiria sana matokeo ya mtihani, basi hata unapokuwa umelala unaona taswira halisi ya matokeo ya mitihani aidha umefaulu au umefeli.

Vilevile sio kwamba taswira hizi tunazoziona usingizini lazima ziwe ni za mawazo yetu yaliyojaa akilini, hapana, huenda ukawaza hata kitu kimoja tu na ukaacha kukifikiria lakini kutokana na kwamba kilishakaa ndani ya ubongo basi inaweza ikatokea siku moja ukaona taswira yake halisi ndani ya usingizi, na wengi huamka na kushangaa, “Ah! Mbona leo nimeota hivi?” na kumbe alishasahau kuwa aliwahi kufikiria juu ya suala hilo aliloliota lakini kwakuwa halikuwahi kudumu akilini mwake basi alilisahau.

Sio kila jambo ulilolisahau basi hufutika ndani ya ubongo hapana, kusahau huko kunatokana na kupatikana mengi ya muhimu na mazito yaliyoziba jambo ambalo umelisahau.

Na ndiyo maana utaona watu wakipata tabu sana juu ya ndoto zao, na wengine huangaika sana kupata ufumbuzi wa jambo waliloliota, kumbe ni fikra zao za kila siku zimewafanya waone taswira hizo ndani ya usingizi. Mfano unaweza kupishana na mwanamke ukamuona mzuri sana, kisha baada ya hapo ukaamua kupotezea ile hali. Na baada ya masiku kadhaa unaweza kumuona usingizini katika mazingira tofauti na yale uliyomuona mwanzo, sasa kama ulimsahau ndio hapo unapoanza kujiuliza huyu ni nani?!! Na mara unaweza kufikiria vibaya, “Au Jini?!!” na hapo unaanza kuhangaika kwa wataalamu. Tuwe makini na fikra zetu.

Inajulikana sana kwa dini zote kuwa wale manabii na mitume walikuwa wakipata ndoto za ukweli ambazo zinaleta maana fulani katika maisha waliyokuwa nayo, lakini hao ni watakatifu waliochaguliwa na mungu na hivyo huoteshwa kwa mafunzo kadhaa katika uongofu wao na watu wao. Na pia wapo ambao wana ujuzi wa kutafsiri ndoto lakini wengi huwa ni waongo au wanaongeza chumvi katika jambo hilo kwa maslahi yao binafsi.

Na pia ijulikane kuwa hakuna tafsiri ya aina moja ya ndoto, kwa mfano “ukiota nyoka basi ujue kuna adui yako hapo” hapa inategemea, je kama wewe ni muoga sana wa kiumbe huyu na siku hiyo ukahisi, au hata ukamuona mdudu huyu na ikakufanya hali hii uote je? Hapo kuna adui yako? Na muradi uliozungumziwa hapa adui sio adui huyu nyoka bali ni adui mwanadamu. Huo ni mfano tu nilioueleza. Hivyo unaweza usiwe na adui hata mmoja lakini ukaota kuhusu huyu nyoka. Haya ni matokeo ya mzunguko wa kumbukumbu ndani ya ubongo.

Sasa hebu tujiulize mimi na wewe leo hii, una fikra ngapi zilizokuzunguka akilini? Na mangapi unayakumbuka na mangapi umeyasahau? Na pia umeshawahi kugundua au kuona hali fulani ambayo inakufanya ukumbuke kwamba, kuna siku hali hiyo ilishawahi kutokea ingawa hupati picha kamili? Basi hizo ndizo kazi za ubongo, ubongo hautupi kumbukumbu hata iwe ndogo kiasi cha punje ya mchele. Ukisahau leo basi ujue ipo siku utakumbuka tu hata kama ni usingizini.

Kule kukumbuka jambo tulilosahau hali ya kuwa tumelala ndiyo humfanya mtu ashikwe na wasiwasi kwanini ameota jambo hilo. Kumbukumbu ya jambo ndani ya usingizi huja kwa mfumo wa taswira halisi.

Napenda sana kuwashauri vijana, ndugu zangu kuwa, tukijifunza kukabiliana na fikra mbaya akilini mwetu, kutatusaidiana kuepukana na wasiwasi, hofu, shida na matatizo yanayotuzunguka, hivyo tuepuke sana kufikiria mambo yasiyotufurahisha na tujitahidi sana kufikiria upande chanya (positive thinking). Tukijaa na fikra nzuri pia tutapata ndoto nzuri na kufurahi, lakini ukijawa na fikra mbaya basi hata ndoto zako nyingi zitakuwa mbaya na kukupa hofu sana katika maisha yako.

kwa makala nyingi zenye kuelimisha na kuburudisha tembelea Staryte - Education, Entertainment & Development - Elimu, Burudani na Maendeleo
 
Binafsi haipiti mwezi bila kuota nikiwa angani napaa, jambo ambalo sijawahi kaa nikalifikiria
 
Ndoto zingine huwa ni tamu balaa.Kwa mfano zilee zinazotufanya tufue mashuka!
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…