Shayu
Platinum Member
- May 24, 2011
- 608
- 1,655
Katika mambo ambayo binadamu anatakiwa kulinda ni uhuru wake wa kutoa maoni na jinsi anavyoyaona mambo kwa upande wake.
Uhuru huu ni msingi muhimu sana kwa jamii yeyote huru. Mtu anaweza kuwa na mtizamo na maoni yake binafsi ana uhuru wa kuyatoa hata kama sio maoni ya watu walio wengi.
Kwakuwa ukweli haupimwi na wingi wa watu wanaouamini. Sio mambo yote wanayoamini wengi ni kweli na sahihi.
Historia inatuonyesha kwamba kuna watu walio wachache walikuwa na ukweli walizungumza ukweli lakini walio wengi waliamini tofauti hivyo waliukandamiza huo ukweli na wengine waliuliwa na kuteswa.
Mfano huu uko kwa Socrate, Yesu , Galileo na wengine wengi.
Ni muhimu kuwajenga watu wetu kuwa na fikra za kujitegemea ( Independent thinking ) Mtu awe huru kusema kila anachofikiria na jinsi anavyoona mambo bila kutukanwa wala kukebehiwa. Uhuru wa maoni ndio msingi wa jamii yeyote iliyostaarabika.
Jamii yeyote ambayo inaruhusu maoni yanayopingana ina nafasi kubwa ya kuendelea kuliko ili amabyo hairuhusu na kukandamiza uhuru wa watu wa kufikiri na kutoa maoni yao.
Ni lazima tujenge tabia ya kujisomea na kutafakari na kuruhusu maoni ambayo sio sawa na yetu yawepo. Turuhusu mijadala ya hoja na sio ya ushabiki. Ukweli unapatikana kwenye mijadala kinzani ambayo inaongozwa kwa hoja. Sio hisia tukiongozwa na hisia hatutaweza kufikiri sawa sawa.
Kutafuta ukweli ni moja ya mambo ambayo binadamu anapaswa kufanya jukumu lake la kila siku. Tusipotafuta ukweli jamii yetu itaishi kwenye giza. Mwanga hupatikana kwenye ukweli na ukweli ndio unaodumu. Ukweli unaweza kukandamizwa kwa kipindi kifupi mno lakini mwishowe lazima itainuka.
Watu wenye fikra huru na zinazojitegemea lazima wathaminiwe. Fikra mkumbo hazijawahi kukomboa taifa lolote lile . Watu walioweza kufikiri wenyewe na kutoa maoni yao jinsi wanavyoona hata kama maoni hayo sio ya watu wengi ni watu muhimu sana kwa taifa hili. Kufikiri kutakwama na maendeleo yetu yatadumaa kama hakuna maoni na fikra zinazo kinzana katika kutafuta ukweli.
Na mimi na waambia watu wetu hawapendi kufikiri na kujisomea lakini wanakuwa wa kwanza kujiingiza kwenye mijadala. Tabia hii inatakiwa iishe. Tutafute maarifa na tujiingize kwenye mijadala tukiwa na uhakika na kile tunachokiamini. Tujadiliane kwa mantiki lengo letu liwe kutafuta ukweli ambao utasaidia jamii yetu na taifa letu.
Ubishi wowote ule ambao mwisho wa siku unakuwa hauna faida na wala hauongezi maarifa au ufahamu wetu ni muhimu kuachana nao. Hausaidii, hauna maana. Haumjengi yeyote yule miongoni mwa wanao bishana. Ni muhimu tukaheshimiana katika mijadala yetu yote na kuheshimu utu wa mtu na kujadiliana kwa mantiki tukiongozwa na fikra sio hisia na mihemko..
Mimi binafsi siwezi kukubaliana na kila kitu kama akili yangu haijaona kina mantiki. Siwezi kuwa mnafiki. kila wakati nitaongea ninachoona ni sahihi. Na nitaheshimu maoni ya watu wote wanaonipinga mpaka hapo nitakapo kuja kujua kama kweli mawazo yangu hayakuwa sahihi. Na nikijua hayakuwa sahihi nitakubali ni uungwana kukubali kama ulikusea na hata hivyo katika maisha yetu ya kutafakari kazi yetu ni kutafuta ukweli na tukiujua ukweli tukaukataa tutakuwa wajinga. Ukweli ni kitu ambacho tunapaswa kukikumbatia. Ukweli hutuweka huru.
Kila wakati ongea unachoamini ni ukweli , hata kama uko peke yako. Ukweli hauwi ukweli kwasababu watu wengi wanauamini. Usiogope kuwa na maoni yako binafsi. Usiogope kutoa maoni yako hata kama uko peke yako na wengi hawaamini unachosema. Furahi unapopingwa , katika kila unachopingwa hasa na watu wengi kwakuwa hautakuwa wa kwanza kupingwa. Usikate tamaa na kila unachoamini. Unapopingwa tafakari kama wanaokupinga wanasema ukweli. Usiogope kama kitu unachopigania kwa siku za usoni na kushinda ukikesha kwa kufikiri na kusoma kitakuwa na faida kwa binadamu wote
Ni wajibu wa binadamu kutafuta ukweli na maarifa ili uwakomboe waliowengi ambao bado wanaishi gizani. Elimu ni mwanga.