SoC02 Ule Ufunguo umekwishapotea!

SoC02 Ule Ufunguo umekwishapotea!

Stories of Change - 2022 Competition

Clement Robert

New Member
Joined
Sep 8, 2022
Posts
3
Reaction score
2
Elimu ni uwezo wa mtu kumudu mazingira yake, elimu isiyomsaidia mtu kufanya hivyo ni mufilisi, sawa na ngombe anayepeleka ulimi wake puani kisha kuurudisha tena kinywani. Shaban Robert aliandika hivyo katika kitabu chake cha kusadikika, huenda aliandika hivyo sababu aliona watu waliokuwa na elimu kubwa kisha wakaangukia kwenye mambo ya kushusha thamani ya kisomo chao, au labda Shaban Robert aliandika hivyo sababu alijua itafika mahala watu hawatapaswa kijificha chini ya kivuli cha elimu na kuyafanya ya ajabu huku wakijigamba kwa maneno ya sisi ni wasomi hatupangiwi cha kufanya

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO iliyotolewa mwaka 2019. Ajira za viwango duni ni moja ya changamoto kubwa katika soko la ajira huku mamilioni ya watu wakilazimika kukubali mazingira duni ya kazi

Ripoti ya ILO inaendelea kwa kusema cha kusikitisha ni kuwa mtu mmoja kati ya watano walio chini ya umri wa miaka 25 hawana ajira, hawajasoma au kupokea mafunzo na hivyo kuhatarisha mustakabali wao wa ajira.

Haifiki kale lakini huenda huko zamani cheti peke yake ilikuwa ni sababu ya mtu kutambulika kama msomi, haikuwa kwa nguvu ila wasomi wa kweli walizalishwa kipindiki hicho, watu waliitaka elimu kwa jasho na damu, vijana wa enzi hizo walitafuta elimu kwa udi na uvumba Sijui, labda sababu wataalamu walikuwa wachache ndiyo maana elimu ilikuwa bora zaidi yenye wahitimu wenye nia za dhati, au labda kipindi hicho hakukua na pisi kali zenye nywele nyeupe kichwani hivyo kila mmoja akamanika zaidi kumshika elimu na asimuache aende zake

Pengine si changamoto tu za kazi, je vijana wenyewe wanajiandaa vipi na vita dhidi ya ukosefu wake, Uwapo ndani ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania nenda kusi rudi kasi watu wenye uchumi mdogo zaidi ni vijana, vijana ambao damu zao zinachemka , akili bado nyepesi kufikiri, miili yao haina uchovu wa mifupa au misuli ya paja, vijana wanaoshindana kuchapisha maneno yenye karaha na aibu mitandaoni kwa lengo la kjifurahisha na kuongeza wafuasi katika kurasa zao ili wajigambe wanapoketi kwenye vijiwe vya mpira

Kwasasa vijana wa vyuoni ni hodari wa kuabudu kuliko wazee wa zamani, Kijana wa chuo akiamka asubuhi anawasha data kwenye simu janja na kuchapisha mtandaoni Alhamdulillah au Ahsante Yesu nimeiona siku nyingine mbele kidogo atamalizia na emoji ya shukrani kisha anazima data na kuendelea kuuchapa usingizi Kwani hujawahi kuktana na chapisho mtandaoni linakuhimiza kupenda like picha kama kweli ni muumini wa dini fulani? Na hapo ndipo ibada ya wanavyuo imetamatika Hapo ndipo yalipoishia mawazo ya mtu tunayeamini atatumia elimu yake kuhamasisha watu waende kuabudu kwenye nyumba za ibada ili kuepuka anasa za hapa na pale

Valentine Mbuke ni mchungaji wa kanisa la Beacon Mission Christianity Center (BMCC) tawi la Mwanza, anaeleza namna ambavyo wanafunzi hukwepa ibada za kanisa kwa kisingizio cha kazi nyingi za chuo huku wakifurika kwa wingi kunapokaribia kipindi cha mitihani ya kumaliza muhula

"Wanajihidi kuja lakini wengine wanakuja Zaidi kwenye kipindi cha mitihani kwasababu waamini zaidi Mungu atawasaidia, wanakuwa ni wakrito wa jina sababu hawajaweka Imani kubwa, wao Imani yao ni ya juu juu tu na wengine wanakuja kwa misukumo ya wazazi ila wengine wapo na tunashiriki nao katika maombi"

Sina maana ya kuaminisha kila mmoja kwamba sasahivi watu hawasomi, lakini nina ushahidi juu ya lawama nyingi nilizozisikia kwenye makongamano mbalimbali pale ambapo waajiri wanalalamikia vyuo, kwa kushindwa kutoa wataalamu watakaokidhi mahitaji kuendana na kasi ya sayansi na teknolojia

Huenda waajiri wana haki ya kukosoa moja kwa moja vyuo vinavyotoa mafunzo ya taaluma hizo, lakini je anayestahili kupokea lawama hizi ni mhadhiri anayetimiza majukumu na kusubiri mshahara uingie mwisho wa mwezi akafurahi na familia yake? Ama Serikali inayopanga mitaala ya kumuandaa mwanafunzi kusubiri ajira na wakati huo huo ikimuhimiza kujiajiri amalizapo masomo yake? Ama mzazi anayelipa pesa na asifuatilie nini kinafanywa huko chuoni na mtoto wake au mtoto anayebadili rangi za nywele baada ya kukutana na marafiki wapya na asikumbuke nini kilimpleka chuoni akasimama kidedea kutmiza wajibu wake..?

Lilian Kabura ambaye ni mtaalamu na mhadhiri wa masuala ya kijamii chuo kikuu cha mtakatifu Agustino SAUT amezitaka taasisi zinazojihusisha kutoa elimu ya juu zikutane na wadau kabla ya kuanzisha program ili kila mmoja aeleze mahitaji yake

“Kabla ya kuanzisha program mbalimbali ni vyema kufanya makutano na waajiri (watu wanaohitaji wataaluma sababu wao ndiyo wanaowapokea kwenye taasisi zao ili chuo kikianzisha kisimamie misingi na kujidhatiti kwenye ubora wa wahitimu, kusiwepo tena na malalmiko kutoka kwa waajiri

Sanjari na yote huruma ni kwamba mwenye kuni atakula vilivyoiva na mwenye pesa atakula vitamu kwa maana hata hao wachache wanaosoma kwa machungu ya kula raka moja bado wanapohitimu masomo yao wanakuta ofisi zote zimejaa, tena sio zimejaa wasomi zaidi au kama wao, huko watakuta muajiri kamuweka mtoto wa mamaake mdogo mapokezi, mtoto wa shangazi mhasibu, mtu wa mahusiano ya umma na masoko ni mtoto wa dada yake, na dada anayefanya usafi alikubali kutoa rushwa ya ngono akapewa nafasi kama ngekewa... Wewe bado unaita elimu ni ufunguo wa maisha! Maisha gani? Au elimu ipi hiyo?

Ila bado huwezi jua umuhimu wa makalio mpaka moja litakapopata jipu, kama ambavyo baadhi ya vyombo vya habari vinafungwiwa na kupigwa faini kila uchao sababu wa waandishi/watangazaji wake kufanya mambo yaliyo nje ya miiko ya taaluma,siku moja tutapata hata Rais wa kupendekezwa sababu ana undugu na viongozi wa Tume ya uchaguzi ya taifa au Rais aliyepita ni Mjomba wake Hii elimu ambayo ipo mahututi kitandani na tunaipa kisogo kana kwamba hatutambui matokeo yake yatakuwa majuto ni mjukuu Anayepata fursa ya kusoma hasomi kweli, Anayesoma anatumia shaghalabaghala elimu yake Na anayemiliki kampuni anapachika ndugu zake ofisini na kuacha wataaluma wa kweli wakichomwa na jua mitaani
Tubadilike.

Kijana uliyepata nafasi ya kusoma soma ukielewa ajira zipo ila yakupasa kujiandaa endapo mambo yatakuwa tofauti. Taasisi za elimu tukemee rushwa ili tuzalishe wasomi wa kujenga sio kubomoa taifa. Serikali iongeze mikakati mbalimbali ya kutanua wigo wa fursa kwa vijana, huenda kupitia wawekezaji au miradi yake mbalimbali ili kauli ya Elimu ni ufunguo wa maisha isiwe mfu

Mtayarishaji wa Makala haya ni Clement Robert. Naweka nukta hapa
+255 752 451 278 / +255 784 808 070
 
Upvote 3
Back
Top Bottom