SoC01 Umasikini chanzo cha maswaibu

SoC01 Umasikini chanzo cha maswaibu

Stories of Change - 2021 Competition

Gunguk baksa

New Member
Joined
Aug 20, 2021
Posts
1
Reaction score
1
UMASIKINI CHANZO CHA MASWAIBU.

Tarehe 21/07/2021 usiku wa sikukuu ya Eid-el-Hajj, ambapo baada ya shamra shamra za mchana katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam. Mnamo saa tano usiku tukiwa tunarejea nyumbani tukaona gari imenasa kwenye mchanga na watu wakifanya jitihada za kulinasua. Tukaomba kuwasaidia kuwanasua na hilo lilikuwa wazo la ndugu yangu hivyo niliafiki, nikaenda kuzungumza na watu walioko pale.

Ajabu ni kwamba nilivyokwenda kuwaeleza hawakutaka msaada na wakaona kama nimekwenda kuwaharibia ‘dili lao’, hivyo tukaamua kuzunguka lile eneo kwa njia nyingine na kutokea mbele ya lile gari. Baada ya kufika mbele ndugu yangu akaniambia tuwasaidie wale watu la sivyo watakesha pale, mara hii tukaafikiana kuwa yule mwenye gari awalipe wale waliokuwa wakijaribu kumnasua na sisi tutamsaidia.

Baada ya kurudi na kuongea wenye gari (mtu na mkewe) ambapo mume alikuwa amelewa kiasi chake akakubali wazo letu na kuwaeleza kisha tukaanza kumsaidia. Wakati ndugu yangu amebaki kwenye gari ili avute hii gari iliyonasa, huku kwenye gari alipanda moja ya watu waliokuwa wakisaidia, kwa kigezo kuwa mwenye gari anaweza kukimbia bila kuwalipa. Gari ikaanza kuvutwa na ikafanikiwa kutoka na hapa ndo kiini kikuu cha hadithi.

Kijana aliyekuwepo kwenye lile gari alikanyaga breki, wakati tunafanya jitihada za kutoa kamba tukamtaka arudishe gari nyuma, ghalfa akaipeleka mbele na kugonga gari yetu. Tulishangaa alichofanya alisimamisha gari na tukamtaka ashuke akasema yeye gari hajui vizuri baada ya kumuuliza kama alikuwa anajua, kuthibitisha hilo alishuka na kuacha gia kwenye ‘D- drive’ wakati tunaongea ghafla gari tulioinasua ikaanza kusogea yenyewe nilifungua mlango haraka nikaingia na kusimamisha gari ambayo ilikuwa inaenda kugonga ukuta wa nyumba iliyokuwa jirani.

Hapa ikathibitika kuwa yule kijana hakuwa na ujuzi na alichokua akifanya. Tuliamua kumuonya kutorudia tena na kuondoka mara moja. Katika kisa hiki kuna aina tatu za umaskini nilizojifunza;

UMASKINI WA MALI

Huu ni umaskini ambao haujifichi hata kidogo, sababu unahusisha vitu vinvyoonekana. Eneo ambalo tulikuta gari imenasa, ni limezungukwa na nyumba (mabanda) za mabati na vyoo vya nje. Hivyo umasikini wa fedha ulipelekea wakazi wa pale kuiliona gari kama fursa ya kujipatia chochote kitu bila kujali jambo lolote.

Vile vile ni umaskini huu wa mali uliopelekea msaada wetu kuonekana kama ubaya, shauri ya kwamba msaada hutolewa bila mtoaji kutarajia malipo yoyote kutoka kwa mpokeaji.

Mwisho, umasikini huu ulipelekea kijana mdogo tu kung’ang’nia kuendesha gari ya watu kwa kuwa ndiyo fursa aliyoipata huku, akilinda mwenye gari asiondoke na kushindwa kulipa pesa yao, ambayo ukiilinganisha na hasara ambazo alitaka kuzisababisha zingetosha labda kumnunulia maji ya kunywa chupa kadhaa tu.

Wakati naandika makala hii niliacha kuandika na kuanza kuangalia pambano la masumbwi katika kipindi maarufu cha televisheni ‘Usiku wa Vitasa’. Katika mchezo wa masumbwi huwa kuna watu wanaomsindikiza bondia mbali ya kocha pamoja na daktari wake. Kwa rejesta iliyoenea hivi sasa, watu hawa wanaitwa “chawa”. Chawa huwa na kazi ya kutetea maslahi ya bosi wao tu. Kuna tukio lilikuwa linajirudia rudia, kwamba kila pambano likiisha chawa wanaingia ulingoni, sasa idadi yao ni nyingi kuliko idadi ya watu wanaotakiwa kuingia ulingoni. Jambo hili lilipamba moto baada ya kuisha pambano kubwa la usiku baada ya mshindi kutangazwa kwenye watu wakaanza kugombania kuingia ulongoni ili kumbeba bondia wao. Jambo hili linapelekea kuleta aina ya pili ya umaskini.

UMASKINI WA KIFIKRA.

Wengi wetu umaskini tunaupima katika vitu vinavyoonekana, lakini pia tunazungukwa na upungufu wa vitu visivyoonekana. Katika tukio la gari kunasa, kitendo cha yule kijana na wenzake kulazimisha kuendesha gari kinaonyesha jinsi gani walishindwa kulinganisha walichotaka kufanya na athari zake.Umaskini huu unatokana na kwamba ima akili zetu hazili chakula cha kutosha yaani taarifa zinazoingia akilini mwetu hazitusaidii kupata fikra mpya na chanya zinazoweza kutusaidia kusogea mbele zaidi.

Asilimia kubwa ya ushauri tunaochukua ni ushauri unaotoka kwa watu ambao tunamudu kuzungumza nao au tunapenda yale wanayoyasema na sababu ya tatu kukosa kabisa mtu/watu wa kutushauri na hii linatokana na mazingira ambayo mhusika anakuwepo. Labda huenda kuna sababu nyingine lakini hizo tatu ndio kuu kabisa, hivyo kupelekea ukosefu wa chakula kitakachoisaidia akili kuwa tanuri la fikra chanya zinazomsogeza mtu kutoka sehemu moja au nyingine.

Umaskini huu wa kifikra unatupelekea kukosa muelekeo wa maisha au jinsi gani ya kuendesha maisha yetu, hili nalo linatufanya tusijue nani wa kumuomba aina gani ya ushauri, hatimae kukosa ushauri na fikra zinazohitajika. Janga hili linaweza kutibika iwapo kwanza tutaanza kuzilisha akili zetu chakula kilicho bora, yaani kusoma, kusikiliza, kuangalia, kushiriki vitu ambavyo ni vya msingi.

Mizani iliyotumika ni kwamba vitu vinavyomjenga mtu bila kupoteza heshima yake binafsi wala ya mwengine. Leo hii kuna maudhui mengi tunayopokea hasa hasa kupitia njia za mawasiliano, asilimia kubwa ya maudhui haya hayatujengi kifikra sana sana yanatufurahisha tu. Sio vibaya kupata wasaa wa kufurahi bali hii furaha isije kwa gharama kubwa inayoweza kupelekea kupoteza mambo muhimu.

Hivyo ni muhimu sana tukajenga utamaduni wa kupenda kujifunza mambo mapya yanayoweza kutujenga kifikra na kukuza upeo wa kufikiri. Vilevile tuchuje maudhui ambayo tunafuatilia mitandaoni ambako tunaweza kupata mawazo mazuri ya kutusaidia. Leo hii kupitia vipindi vya redioni au televisheni mara chache sana unaweza kukuta kipindi kinanyesha stadi za maisha au elimu ya fedha au hata umuhimu wa mazingira tu, haya ni maudhui ambayo huenda yangesaidia mtazamo na fikra zetu kwenye mambo mengi kuwa nzuri. Mwisho ningependa kumalizia na suala zima la afya ya akili.

Hili ni janga amabalo bado hatujalipa umuhimu wa kutosha kutokana na kutoonekana moja kwa moja madhara ya uwepo wake. Kuna uwezekano mkubwa wengi wetu tunahitaji msaada wa afya za akili zetu, hili linatokana na baadhi ya vitendo ambavyo tunavifanya ima wazi au kwa kujificha. Kuna haja kubwa sana ya kuelimishana kuhusu umuhimu wa afya ya akili na vipi tunaweza kujihifadhi na magonjwa au sababu zinazopelekea kuathirkika na ugonjwa akili.

UMASIKINI WA MAONO.

Fikra na maono ni mambo yanayokaribiana sana na uhusiano uliopo baina ya vitu viwili hivi ni mkubwa. Uwepo wa fikra nzuri unaweza kupelekea uwepo wa maono mazuri na kinyume chake ni sahihi. Japo kuna uwezekano wa kuwepo kwa fikra nzuri na lakini ukakosa maono ya kuzitumia fikra hizo kufika mbali.

Wakati nataka kuandika sehemu hii ya makala, nilikumbwa na shughuli za ghafla hivyo sikuendelea.

Huenda ulikuwa ni wasaa wa baraka katika kificho “blessing in disguise”, kwa sababu kulizuka habari ya mchezaji wa tenisi wa Uingereza aitwaye “Emma Raducanu” mwenye umri wa miaka 18 ambaye ameweza kushinda mashindano makubwa ya US Open jijini Newyork mwaka huu.

Nilipoona jina lake sana katika kurasa za mitandaoni nikaona nimtafute ili niweze kujua binti huyu ni nani. Emma binti wa miaka 18 kabla ya kucheza tenisi alipitia michezo minne kabla ya kufika kwenye tenisi mchezo wake wa tano na ambao leo hii umemjengea umaarufu mkubwa.

Kwa mujibu wa tovuti ya “nationworld.com” Emma anatoka katika familia nzuri tu inayojiweza yenye mchanganyiko wa asili tofauti, yenye baba mwenye asili ya Romania na mama mwenye asili ya Uchina. Yeye amefanikiwa kumaliza shule sekondari akibobea hisabati na uchumi huko Uingereza.

Maono ya wazazi wake waliona ajikite zaidi kwenye michezo kwani toka mdogo amekuwa ni mpenzi sana wa michezo. Hivyo wazazi wake walitumia fedha na rasilimali nyingi tu kumjaribisha katika michezo mbali mbali mpaka aliponesha uwezo kwenye tenisi na akasajiliwa kwenye shule ya tenisi huko huko Uingereza. Hili tukio limesababisha nibadilishe maono yangu kwenye suala la michezo au uchumi wa michezo.

Uwekezaji katika michezo hata katika ngazi ya familia moja moja bado ni mdogo sana. Wakati habari ya Emma Raducanu ikiendelea kuishangaza dunia, kuna kijana wa kitanzania aitwaye Barka Seif Mpanda mwenye umri wa miaka 7 anayetoka katika familia chache zinazoona uwekezaji kwenye kipaji alichonacho mtoto ni muhimu. Inaweza kuwa kuna changamoto katika mfumo au uchache wa vioo vya kuakisi mafanikio ya vipaji nchini, lakini mambo hayo hayaondoi uhalisia kwamba maono ya wengi wetu yamekusanyika sehemu moja.

Kijana Barka Seif yuko nchini uholanzi kwenda shule ya mpira ya klabu kongwe nchini humo ya Ajax inayotambulika kuzalisha vipaji vizuri katika ulimwengu wa soka. Hadithi ya Emma wa Uingereza na Barka wa Tanzania zinafanana pale ambapo wazazi wao wameamua kuwekeza katika vipaji vya watoto wao zaidi kuliko kufuata tu utaratibu wa maisha.

Umasikini huu wa maono, wa kushindwa kuona kwamba huu utaratibu wa shule mpaka chuo kikuu kwa sasa unakumbwa na changamoto kadhaa kama uwepo wa deni kubwa pale kijana anapomaliza masomo ya chuo, uwepo wa wahitimu wengi kuliko fursa chache za ajira, uwepo wa wahitimu wengi wasioweza kuleta tija.

Hivyochangamoto hizi ambazo watu mmoja mmoja na lakini pia nchi kiujumla imeshindwa kwa na maono ya kuangalia jinsi gani tunaweza kutatua changamoto mbali na utaratibu wa kawaida tu. Ndiyo maana kila kila kiongozi anaposimama siku ya mahafali ya taasisi yoyote ya kielimu kuna maneno yanafanana kwenye hotuba zao ‘niwapongeze wahitimu kwa kumaliza masomo yao, ninawahusia mtumie elimu zenu kujiajiri na msitegemee kaujirirwa’ haya ni maneno maarufu sana katika mahafali mengi tu.

Hivyo umasikini huu umetukumba katika nyanja mbalimbali katika nchi hivyo kupelekea kuchelewa maendeleo ya familia moja moja mpaka nchi kiujumla.


HITIMISHO.

Jambo la muhimu katika maisha yetu ya kila siku ni kujifanyia tathmini na kukubali kujifunza na ili tuweze kutoka katika aina mbalimbali za umasikini.


Mwandishi:
Gunguk baksa.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom