SoC01 Umasikini katika nchi zinazoendelea ni wa kujitakia

SoC01 Umasikini katika nchi zinazoendelea ni wa kujitakia

Stories of Change - 2021 Competition

DustBin

JF-Expert Member
Joined
Jun 3, 2021
Posts
609
Reaction score
604
Maendeleo na umasikini ni vitu vinavyoelekeana kwa kukinzana. Kupiga hatua kimaendelea kunadidimiza na kuuzika umasikini. Na umasikini unamfanya mtu asiendelee katika Nyanja yeyote ile. Tunapoambiwa kuna nchi za daraja la tatu nchi zinazoendelea ni kwamba zinaendelea kujikwamua kutoka katika dimbwi la umasikini. Kama yalivyo maendeleo, umasikini pia hua kwa mtu mmoja mmoja na hata kwa kiwango cha nchi/taifa kwa ujumla wake. Ukweli usiopendeza kusemwa ni kwamba nchi zinazoendelea ni nchi masikini ingawa wenyewe au imezoeleka kuita nchi zinazoendelea ili kuficha ule unaoitwa umasikini. Hata hivyo nchi nyingi ambazo kwa asilimia kubwa ni nchi zinazopatikana katika bara la Afrika zinakumbwa na umasikini wa kujitakia.

Kwa hali ya kawaida nchi hizo hazikutakiwa kuwa katika kundi la nchi masikini kwa sababu zifuatazo;-

  1. Idadi toshelezi ya watu
    Miongoni mwa sababu zinazotajwa kuchochea umasikini ni wingi wa watu ambao ukilinganisha na rasilimali zilizopo hazitoshi kuwakidhi watu wote. Ukizichunguza nchi nyingi zinazoendelea utagundua zina idadi toshelezi (ya wastani) ya watu hasa ukilinganisha na rasilimali ardhi ambayo ndio kigezo kikubwa kitumikacho katika kupima wingi wa watu katika eneo husika.

  2. Wingi wa mali ya asili na vito vya thamani
    Nchi hizi zina hazina ya mali ya asili ya kutosha sana. Vitu kama madini ya thamani, wanyama pori na misitu mikubwa ya kuvutia, milima yenye kila aina ya vivutio, hali ya hewa safi, uoto wa asili, vyanzo vya kudumu vya maji kama bahari, maziwa na mito mikubwa.

  3. Amani na utulivu
    Kukosa utulivu, usalama na amani katika nchi hupelekea kurudi nyuma katika kupiga hatua za kimaendeleo. Kwa miaka ya millennia ya pili nchi zinazoendelea hasa za kiafrika hali ya usalama imehakikishwa na kufanya watu waishi kwa amani na utulivu. Sio kama hakuna migogoro na machafuko kwa asilimia zote la hasha! Machafuko na migogoro ipo ila kwa kiwango kisicho athiri harakati za kimaendeleo.

  4. Shirikisho na jumuiya za kikanda
    Nchi nyingi leo hii zimejiunga na kuunda jumuiya za pamoja kwa ajili ya masilahi fulani. Pamoja na mambo mengine jumuiya hizo zinaweka kipaumbele suala la kuhakikisha usalama katika ukanda wao. Lakini pia kushirikiana katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo kama vile biashara na uchukuzi, teknolojia na mawasiliano.
Pamoja na uwepo wa hayo niliyoyataja na mengine ambayo sijayaorodhesha bado nchi hizo zinasifika kwa umasikini. Na ndio maana nikasema umasikini huu ni wa kujitakia.

Mambo yafuatayo ni ishara ya kuonesha kuwa umasikini wa nchi zinazoendelea ni wa kujitakia;-

  1. Uvivu wa kutojishugulisha
    Ria wengi wa nchi hizo wanasifika kwa kubweteka na kutojishugulisha katika shuguli za kujikwamua kutoka katika umasikini. Kwa mfano utakuta mtu anaishi katika maeneo ya kijijini lakini akashindwa hata kusafisha eneo la nyumba yake kiasi unafika kwake unakuta nyumba imezungukwa kwa vichaka visivyohimilika na yeye anaona kwake ni kawaida. Na kubweteka huku wakati mwingine huletwa na ile tabia ya kuona baba ana vitu nitavirithi, hivyo ukamkuta kijana hajishugulishi eti kwa kuwa wazazi wake wana mali.

  2. Viongozi wasiowajibika
    Viongozi wengi katika nchi hizi wamegubikwa na uchu wa madaraka na lengo lao kubwa ni kujinufaisha na kujitajirisha kwa kutumia rasilimali za taifa. Na ndio maana viongozi hao hawana mipango au sera za kimaendeleo kwa ajili ya nchi zao. Na hata pale linapokuja suala la kimaendeleo ya nchi wanapoona kuwa jambo hilo halina maslahi binafsi kwao hulikana jambo hilo na kulipinga kwa gharama zote.
    Viongozi wengi sio wabunifu, hawataki kujichosha kufikiria kwa ajili ya nchi zao, ule moyo wa kujitoa kwa ajili ya jamii kwa viongozi wengi haupo.
    Bali utakuta baadhi yao wakitumika na mataifa makubwa kuhujumu rasilimali za nchi zao kwa kujinufaisha wao wenyewe.
    Kubwa zaidi unakuta kwenye nchi hizi viongozi wanaochaguliwa hawana uwezo wa kuongoza, aidha kwa kupata madaraka kwa njia za haramu kama rushwa na mfano wake au kwa kuteuliwa kutokana na sababu zingine tofauti na vigezo ainishi vya kupata kiongozi bora.

  3. Kukosa kujiamini na kutojikubali
    Huu ni ugonjwa unaozikumba nchi nyingi zinazoitwa nchi zinazoendelea. Wameshajiwekea katika mawazo yao kwamba wao ni nchi masikini na huko kuna nchi tajiri hivyo vyovyote iwavyo hawawezi kuwa kama hao wanaoitwa nchi tajiri. Hivyo maisha yao hutegemea misaada kutoka kwa wahisani na nchi tajiri, hata wakipanga bajeti zao huweka kabisa na asilimia kadhaa fedha zake ni za misaada. Kwa maana hupanga bajeti kwa fedha wasizokua nazo wakitaraji misaada kutoka nchi tajiri. Na ndio maana nchi tajiri hutumia misaada hiyo kupora rasilimali kwenye nchi masikini kwa ajili ya maslahi yao ya kimaendeleo.

  4. Tabia ya kuiga hata visivyokua na maslahi kutoka katika mataifa makubwa
    Ukichunguza mambo mengi ambayo ndio misingi ya kimaendeleo katika nchi hizi huiga kutoka kwa nchi za daraja la kwanza. Ukiangalia mifumo ya elimu imenakiliwa kutoka huko, sera na mbinu za kimaendeleo zinachukuliwa kutoka katika nchi hizo, kubwa zaidi utakuta hata katiba za nchi hizo ambazo ndio msingi mama wa sheria zote za nchi zimenakiliwa tu kutoka katika nchi hizo.
    Mbali na hayo kuna baadhi ya mambo yanaigwa hata hayana msingi katika kuisaidia nchi kupiga hatua kimaendeleo. Utakuta kila kinachofanywa katika nchi za daraja la kwanza hata bila kuchunguza wao wanafanya hivyo kwa mantiki gani mambo hayo huletwa kwenye nchi za daraja la tatu na kutekelezwa, mwisho wa siku umasikini unaendelea.

  5. Wivu wa kijinga na roho mbaya
    Raia wengi katika nchi hizi zinazoendelea wanasumbuliwa na wivu wa kijinga, asione mwenzie amefanikiwa basi ataanza kumchukia na kumfanyia vitimbi na kumsemanga. Hatakio kuona mwenzie anapiga hatua kimaendeleo, hasa tabia hii inapokua sugu mpaka kwa viongozi jambo huwa na athari kubwa zaidi.

  6. Kukosa mipango na dira ya maendeleo ya taifa
    Nchi nyingi zinazoendelea hazina mipango madhubuti yenye mikakati imara ya kimaendeleo. Na hili hutokana na kukosa dira ya wapi nchi inataka kwenda au kufika. Rasilimali zipo lakini zinashindwa kutumiwa ipasavyo kwa kupanga mikakati endelevu juu ya matumizi bora ya rasilimali hizo kwa maendeleo ya taifa.


HITIMISHO

Umasikini ni jambo la kujitakia, unahitajika utayari tu wa mhusika kujiikwamua kutoka katika janga hilo hasa pale ambapo sababu za kujikwamua zipo. Wito kwa nchi zinazoendelea, endapo zitaendelea kuridhika na hali walizonazo umasikini hauwezi kwisha daima.

Kuna haja kubwa ya kufanya mabadiliko ya kiuongozi na kiutawala katika nchi nyingi zinazoendelea ili kuchochea maendeleo. Kuna hitajio la kuwa na viongozi wa aina fulani ya udikteta ili kuweka mazingira sawa kwa raia na kuwafanya wawajibike katika kujiletea maendeleo wao wenyewe kwa kujishugulisha.

DustBin
 
Upvote 0
Back
Top Bottom