Masaburi kumrithi Kimbisa Dar es Salaam
Imeandikwa na Oscar Job; Tarehe: 16th December 2010 @ 06:13
NYOTA ya Umeya wa Jiji la Dar es Salaam imemwangazia Diwani wa Kata ya Kivukoni katika Manispaa ya Ilala, Didas Masaburi, baada ya jana kushinda katika kinyang'anyiro cha nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kutokana na uchache wa viti vya udiwani vya vyama vya Upinzani ukilinganisha na vile vya madiwani wa Chama Cha Mapinduzi, ni dhahiri kuwa Mbunge huyo wa Bunge la Afrika Mashariki ndiye atakayekuwa mrithi wa Adam Kimbisa aliyeongoza Dar es Salaam kwa miaka mitano iliyopita.
Kimsingi, Masaburi ndiye Meya mpya wa Dar es Salaam kwani katika Jiji la Dar es Salaam, CCM inavyo viti 111 wakati wapinzani wana viti 14 tu. Kati ya hivyo, Ilala wanacho kimoja, Temeke viwili na Kinondoni 11.
Madiwani hao wa vyama vyote kesho watapiga kura kumchagua Meya wa Jiji. Masaburi alichaguliwa na Baraza la Madiwani la CCM la Jiji la Dar es Salaam jana kuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, kwa kuwashinda wagombea wenzake wawili, Tarimba Abbas na Hashimu Saggaf kwenye uchaguzi uliofanyika kwenye Ukumbi wa Karimjee.
Masaburi alishinda kwa kupata kura 61 kati ya kura 111 zilizopigwa na wajumbe wote huku Tarimba anayetokea Kata ya Hananasif katika Manispaa ya Kinondoni, akipata kura 33 na Saggaf aliyewahi kuwa Mbunge wa Dodoma Mjini na sasa Diwani wa Mchafukoge, aliambulia kura 17.
Awali, kabla ya kutangaza matokeo hayo, Msimamizi wa uchaguzi huo, Ritta Mlaki, aliwataka wajumbe na wagombea wote kutulia wakati wa kuyatangaza matokeo hayo huku akisisitizia ushindi uliopatikana hapo ni wa huru na kuwa wagombea wamepigiwa kura kutokana na namna wanavyokubalika na wajumbe.
Aidha, aliwapongeza wajumbe wote kwa kufanikisha uchaguzi huo katika hali ya utulivu na amani huku pia akisifia demokrasia iliyokomaa ndani ya chama hicho tawala kwa kuzingatia kuwa hakuna kura hata moja iliyoharibika katika uchaguzi huo.
Baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, baadhi ya wajumbe waliokuwemo katika ukumbi huo, walishangilia kwa nderemo huku mke wa mshindi huyo, Janet Masaburi aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, akiangua kilio sambamba na kupiga magoti na kumwomba Mungu.
Masaburi aliahidi kushirikiana na wenzake kumaliza kero mbalimbali za wakazi wa Jiji na kuwataka madiwani wenzake kuvunja kambi ndani ya CCM ili kusimama kama kitu kimoja kwa maslahi ya chama hicho.
Aidha, katika uchaguzi huo uliofanyika katika ngazi za Manispaa zote tatu za Jiji la Dar es Salaam, Temeke, Kinondoni na Ilala, pia matokeo yaliyotolewa yaliangusha nderemo kwa baadhi ya wajumbe.
Katika Manispaa ya Ilala, Diwani wa Jangwani na Meya wa siku nyingi wa Ilala, Abuu Jumaa alikula mwereka kwa kijana mdogo, Diwani wa Kata ya Gongo la Mboto, Jerry Silaa baada ya kushindwa kwa kura 25 dhidi ya zake 10. Silaa alikuwa Naibu wa Jumaa katika Baraza la Madiwani lililopita.
Mgombea mwingine, Salumu Bisalala kutoka Kata ya Kariakoo aliambulia kura mbili. Nafasi ya Naibu Meya ilikwenda kwa Eli Kessy kutoka Kata ya Kisutu aliyepata kura 20 na kuwashinda wenzake, Abdulkadiri Salum ‘Masamaki' aliyepata kura 11 na Mtumwa Mohamed aliyepata kura tano.
Kwa upande wa Temeke, Maabad Hoja alichaguliwa kuwania nafasi ya umeya wa Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam, kwa tiketi ya CCM.
Hoja alitangazwa jana katika uchaguzi uliofanyika katika Ukumbi wa Manispaa hiyo, baada ya kuwashinda wagombea wengine wawili.
Wakati Hoja akitangazwa kuwa mgombea mteule wa nafasi hiyo, wajumbe walimteua Aisha Mpanjila kuwania nafasi ya unaibu meya wa manispaa hiyo.
Akitangaza matokeo Katibu wa CCM Wilaya ya Temeke, Saad Kusilawe, alisema kura zilizopigwa katika nafasi ya umeya ni 39 na kwamba hakuna zilizoharibika; na katika hizo, Hoja alipata kura 30 huku akiwaacha Michael Mwakasindile aliyepata sita na Zena Mgaya kura tatu.
Kwa nafasi ya unaibu meya, wajumbe walikuwa 39 na hakuna kura iliyoharibika ambapo Mpanjila aliteuliwa baada ya kupata kura 34, huku Abdallah Chaurembo akipata tatu na Muhidini Sanya mbili.