Montserrat
JF-Expert Member
- Sep 9, 2011
- 10,938
- 14,745
Katika hali ya kawaida, kila mtu mwenye kipato lazima kwa njia moja au nyingine ajikute analipa kodi. Kodi inaweza kulipwa kupitia manunuzi/matumizi, mshahara, biashara, au uwekezaji.Kwa utangulizi huo ni wazi kwamba karibia kila mtu lazima anaswe na mtego wa kodi. Ni kwa sababu hiyo naona umuhimu wa kila mtu kujua sheria na kanuni zinazotumiwa kutoza kodi.Pengine tujiulize kodi ni nini? Kodi ni tozo la lazima kwa mujibu wa sheria ambapo Serikali huwatoza watu mbalimbali, makampuni na taasisi. Kodi inalipwa kwa pesa sio bidhaa. Nisingependa kueleza kwanini tunalipa kodi, kwa sababu maelezo yake yanatolewa kila mara na viongozi mbalimbali pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Kumekuwepo na changamoto nyingi zinazohusu maswala ya kodi. Nyingi kati ya hizo zinasababishwa na uelewa mdogo walionao wadau wa kodi.
Nani ni mdau wa kodi? Kutokana na maelezo ya awali, jibu ni wazi; ni mtu yeyote au taasisi ambayo inafanya manunuzi/biashara/uwekezaji au ina kipato chochote kutokana na ajira hapa nchini.
Mataifa yaliyoendeleza elimu ya kodi imepewa msisitizo, kila mtu anahamasika kuelewa maswala ya kodi kwa sababu hakuna jinsi atajikuta halipi kodi. Wengi unawakuta wana uelewa sawa au zaidi ya maafisa wa kodi. Kuepuka misuguano na malumbano, uelewa na sheria za kodi ni muhimu kwa kila mtu; angalau tu zile kodi/ushuru/tozo ambazo panga pangua utakutana nazo katika shughuli zako.
Unapoanzisha shughuli yoyote, miongoni mwa mambo ya msingi kuyaelewa ipasavyo ni maswala ya kodi katika eneo hilo. Soma maandiko, kutana na wataalamu wa kodi wakupe ushauri katika hilo eneo kabla hujafanya maamuzi ya kufanya au kutofanya shughuli/mradi huo. Utaonekana mtu wa ajabu unaletewa makadirio/bill halafu utetezi wako unakuwa nilikuwa sijui kama napaswa kulipa hiyo kodi/tozo
Ipo changamoto kwamba sheria zetu zipo kwenye lugha ya kiingereza. Serikali makini inayojua uhalisia wa watu wake inatakiwa iwe na seti mbili za sheria za kodi; moja kwa kiswahili na nyingine kwa kiingereza. Hiki ni kilio cha muda mrefu ikiwa ni pamoja TRA kuwaandika walipakodi barua za kiingereza, wakati wanajua kabisa kwamba wanaye muandikia barua ya kiingereza hajui lugha hiyo. Hiki kitu hakijakaa sawa, ili andiko langu liwe na mafanikio, ningeomba hiki kilio kipate jibu.
Kumekuwepo na lawama nyingi kwa watumishi wa Mamlaka ya Mapato kuhusu kuwabambikia walipakodi kodi kubwa ili kutengeneza mazingira ya kudai rushwa. Sina uhakika na madai haya na si nia andiko hili kujua ukweli wake. Kinachoonekana hapa ni uelewa mdogo wa maswala ya kodi. Kujua kama umebambikiwa kodi kubwa au la unahitaji uwe na uelewa wa kutafsri kwa usahihi sheria za kodi. Mlipakodi ana haki ya kupinga makadirio ya kodi kama ana ushahidi kwamba makadirio aliyopewa hayakufuata matakwa ya kifungu fulani cha sheria ya kodi husika. Taratibu za kupinga makadirio zimeelezwa wazi kwenye Sheria za kupinga makadirio ya kodi (Tax Revenue Appeal Act) pamoja na Sheria za Usimamizi wa Kodi (TAA). Hata hivyo, Mamlaka ya Mapato inawajibika kumuelimisha mlipakodi taratibu na muda wa kuwasilisha pingamizi lake, sio kuviziana kama inavyokuwa mara nyingi.
Lengo la andiko hili ni kutaka Watanzania wajibidiishe kuyaelewa mambo muhimu ya kikodi yanayogusa kazi/biashara/uwekezaji wao. Tusipende kuwa taifa la kulalamika tu bila kujua sheria zinatutaka nini. Tukiweza kuwa na uelewa huo, basi tutakuwa tumefaulu kuondoa moja ya kero tulizonazo katika maisha yetu ya kila siku.
Zipo aina nyingi ya kodi, kwa mfano zile zinazosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania:
Kodi ya kampuni/Kodi ya Mapato kwa watu binafsi
Ushuru wa Forodha,
Ushuru wa bidhaa, zikiwemo na hizi za kwenye miamala ya simu
Ushuru wa mafuta (Petroleum Levy) - Tzs 313 kwa lita
Ushuru wa mafuta ya Taa, Dizeli na Petroli (Fuel Levy) - Tzs 50 kwa lita
Tozo ya kuendeleza Reli – 1.5% ya CIF
Ushuru wa Stempu
Kodi ya Ongezeko la Thamani
Kodi ya majengo na mabango
Ushuru wa bidhaa ziendazo nje (Export Tax) – Ngozi
Tozo ya Korosho zisizobanguliwa (Export Levy)
Ada ya mchakato wa forodha (Processing fee) – 0.6% ya FOB
Kodi ya kuendeleza utalii
PAYE
Ada za huduma ya Bandari
Kodi kwenye michezo ya kubahatisha
Kodi ya zuio, ikiwemo pato litokanalo na kuuza rasilimali
Tozo ya kuendeleza ufundi stadi – 4% kwa malipo yote aliyolipa mwajiri kwa wafanyakazi; kwa waajiriwa ≥10
Ada ya usajili, Kuhamisha umiliki wa vyombo vya moto na Leseni za udereva
Ushuru wa huduma za Viwanja vya Ndege, nakadhalika nakadhalika
Kama kawaida ukishindwa kufuata sheria, lazima utakutana na kadhia ya kupewa adhabu na riba ya kuchelewesha serikali kupata kilicho chake. Hizi adhabu na riba mara zote zinaathiri mtaji wako. Wapo wengi wanatozwa adhabu na riba kwa sababu ya kukosa elimu ya kodi, wakati unaweza kupata elimu ya kodi bila gharama yoyote.
Si nia yangu kwa sasa kufafanua jinsi gani kila aina kodi inavyokokotolewa, bali kukuhamasisha kusoma sheria na kanuni za kodi (zipo kwenye mtandao wa TRA - www.tra.go.tz), kuongea na watalaamu wa kodi, kuhudhuria semina zitolewazo na Mamlaka ya Mapato kuhusu kodi mbalimbali, kusoma hukumu za maswala ya kikodi ambazo baadhi zipo kwenye mtandao wa Mamlaka ya Mapato Tanzania. Ukifanikiwa kufanya hivyo, taratibu utajikuta umekuwa mbobezi wa masuala ya kikodi bila kuingia darasani; sambamba na hilo hakuna mtu atakubabaisha au kukubambikia kodi.
Kumbuka zoezi la kujifunza ni endelevu, na sheria zetu za kodi zinabadilika mara kwa mara.
Tutumie vizuri simu/tablet/computer zetu kupata elimu sio kwenye umbea, pisi kali au majungu.
Upvote
1