Umuhimu wa kumbukumbu na nyaraka za Sykes katika kuijua historia ya Mwalimu Nyerere, TAA na TANU (2)

Umuhimu wa kumbukumbu na nyaraka za Sykes katika kuijua historia ya Mwalimu Nyerere, TAA na TANU (2)

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
UMUHIMU WA KUMBUKUMBU NA NYARAKA ZA SYKES KATIKA KUIJUA HISTORIA YA MWALIMU NYERERE, TAA NA TANU (2)

Ndani ya nyaraka hizi nikasoma historia ya Kasella Bantu katika ujana wake akiwa masomoni Afrika Kusini na akaanza kazi huko.

Namsoma Kasella Bantu akiwa kijana mdogo aliyeajiriwa akagombana na Mzungu jina lake Hugh Tracey na Tracey akaandika barua mbaya dhidi ya Kasella Bantu iliyosababisha kufukuzwa kazi.

Kasella Bantu alirudi Tanganyika na akaajiriwa na Tanganyika Broadcasting Corpration (TBC) na hapo akagombana tena na Mzungu mwingine aliyewatukana Waafrika kwa kuwaita wajinga. Kasella Bantu aliandika barua ya kujitetea (Kasella Bantu kwa kwa Honourable Chief Secretary 27 April 1954).

Lakini barua hii haikumsaidia kitu kwani Chief Secretary alikuwa na taarifa ya iliyoandikwa Afrika Kusini na Hugh Tracey.

Ikaonekana kama Kasella Bantu ni Mwafrika mkorofi kwa hiyo akafukuzwa kazi kuwaonyesha Waafrika kuwa hailipi kuonyesha ‘’jeuri’’ na ‘’ukaidi’’ kwa Wazungu.

Katika nyaraka hizi nikasoma mengi ya Mwalimu Nyerere lakini hayakuwa katika hali ile ya kusisimua kama mathalan haya niliyoeleza katika historia ya Kasella Bantu ya kupambana uso kwa uso na wakoloni.

Mwalimu yeye alikuwa na ya kwake .ambayo yatagusa fikra zako kwa namna ya pekee kabisa.

Haya ni kutokana na uandishi wake hodari, umahiri wa lugha ya Kiingereza na upangaji wake wa hoja.

Ilikuwa katika nyaraka hizi ndipo mimi kwa mara yangu ya kwanza ukitoa kuiona sahihi ya Nyerere kwenye noti ndipo nilipoiona katika karatasi ya kawaida.

Nilikuwa mfano wa yule ‘’mkulima mwenye shamba aliyechimba chini akapata almasi.’’

Katika mikono yangu nilikuwa na hazina kubwa sana na nikamuuliza Ally Sykes kwa nini hizi nyaraka hawapi, Nyaraka za Taifa (Tanzania National Archives) kwa ajili ya kutunzwa na kuhifadhiwa kwa faida ya taifa zima na kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Mtafiti yeyote atakaebahatika kuziona nyaraka hizi lazima atapigwa na butwaa.

Kuna barua iliyoandikwa mwezi Agosti 1954 na Zuberi Mtemvu kwa penseli akimwandikia Ally Sykes inayohusu mazungumzo ambayo Mtemvu alifanya na Nyerere wakimzungunza yeye.

Walichozungumza Mtemvu na Nyerere juu ya Ally Sykes ni barua yake ya uhamisho kwenda Korogwe majuma mawili tu baada ya TANU kuundwa.

Waingereza walikuwa wanamuadhibu Ally Sykes kwa kuwa mmoja wa waasisi wa TANU.

Katika barua ile Mtemvu alimfahamisha Ally Sykes kuhusu mwanachama mpya aliyempata.

Huyu alikuwa Ali Mwinyi Tambwe, Katibu wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika.

Huyu Ally Mwinyi Tambwe atakuja kufanya mambo makubwa sana katika historia ya Tanganyika na Zanzibar na atakuja kuwa karibu sana na Nyerere wakati wa kudai uhuru na baada akimtumia kama mshauri wake mkubwa katika siasa za Zanzibar.

Si haya tu Ali Mwinyi Tambwe atahusika pia katika mipango ya mapinduzi Zanzibar.

Lakini kubwa na la kushangaza ambalo Nyerere hakujua, si Abdul wala Ally Sykes, wala Mtemvu ni kuwa Ally Mwinyi Tambwe alikuwa kachero wa Waingereza ndani ya TANU.

Kwa miaka mingi hii ilibakia kuwa siri na kama ilijulikana labda aliyekuja kujua ni Julius Nyerere tena baada ya uhuru lakini wengine wote hawakulijua hili.

Kwa Mtemvu kumleta Ali Mwinyi katika TANU alikuwa anamfungulia mlango kicheche kuingia ndani ya banda la kuku. Kuna matukio matatu ambayo yalitokea kwa Rashid Ali Meli, Ally Sykes na Iddi Faiz Mafungo ambayo yalikuwa katika siri kubwa ndani ya TANU lakini Waingereza walipata taarifa na wakachukua hatua kujaribu kuyazuia yasifanikiwe.

Bahati nzuri wazalendo hawa wote waliweza kunusurika na mitego waliyowekewa na makachero wa Special Branch.

Iddi Faizi alikamatwa Turiani akashushwa ndani ya basi akitokea Tanga akidhaniwa ana fedha amepokea kutoka Tanga kwa Mwalimu Kihere kwa ajili ya safari ya kwanza ya Nyerere UNO Februari, 1955.

Rashid Ali Meli yeye alikuwa ametoa fedha katika sefu yake akiwa Mtunza Fedha wa Dar es Salaam Municipal Council kuikopesha TANU kwa ajili ya safari ya Nyerere UNO na akavamiwa na wakaguzi ofisini kwake siku ya pili tu.

Imechukua miaka 57 kumtambua yule aliyekuwa akivujisha siri za TANU kwa Waingereza.

Kuna barua ya Mtemvu aliyoandika kwa penseli akimwandikia Ally Sykes, Mtemvu anaeleza safari yake ya Morogoro yeye na Nyerere.

Hii ilikuwa safari ya kwanza ya Nyerere kama Rais wa TANU kusafiri nje ya mipaka ya Dar es Salaam Agosti 1954.

Mtemvu Mtemvu alimshawishi baba yake Mzee Mmanga Mwinshehe azungumze na wazee wenzake Morogoro ili yeye na Nyerere waende Morogoro kuzungumzanao kuhusu TANU na harakati za kudai uhuru.

Mazungumzo haya hayakuzaa matunda kwani wazee wa Morogoro hawakuonyesha hamu ya kujiunga na TANU.

Mtemvu na Nyerere wakarudi Dar es Salaam mikono mitupu. Katika barua hii Mtemvu anamfahamisha Ally Sykes kuwa amefanya mazungumzo na Nyerere na wamefikia kuamini kuwa Ally kwa uhamisho ule wa Korogwe akishaondoka Dar es Salaam asitegemee kamwe kama Waingereza watamrudisha tena Dar es Salaam.

Nafasi haitoshi kabisa ni ndogo kwangu mimi kukueleza msomaji wangu yote yaliyomo katika hizi nyaraka zilizosheheni mengi katika historia ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na historia ya TANU na historia ya wazalendo wengi wengine ambao baadhi hata majina yao hayajasikika popote juu ya kuwa walifanya makubwa katika kupigania uhuru wa Tanganyika kwa hali na mali.

Wazalendo kama Iddi Faiz Mafungo, Rashid Sisso, Juma Selemani maarufu akijulikana kwa jina la Juma Mlevi, Shaaban Gonga kijana mshairi aliyetunga mashairi ya kumsifu Nyerere na TANU, Robert Makange, Rashid Ali Meli, Shariff Abdallah Attas na mkewe Bi, Chiku bint Said Kisusa na watoto wao Mwalimu Sakina na Mwalimu Fatina, Tatu bint Mzee, Hawa bint Maftah akina mama ambao waliingiza nyimbo za lelemama katika mikutano ya TANU ya mwanzo Mnazi Mmoja, nyimbo ambazo zilihamasisha wananchi kusimama imara nyuma ya Nyerere wakaijenga haiba yake ikawa kubwa na nzito kumwezesha Nyerere kuwaunganisha Watanganyika wote kuwa kitu kimoja na kujiona wao ni taifa badala ya makabila mado 2go madogo.

Majina ya wazalendo hawa ni mengi sana lakini juu ya wingi wao taifa lina wajibu ya kuwaadhimisha na kuwaenzi pamoja na Mwalimu Nyerere.

NYERERE NA ALLY SYKES.JPG

Mwalimu Nyerere na Ally Sykes 1958

ABDULWAHID SYKES NA NYERERE ARNAUTOGLO HALL SAFARI YA PILU YA NYERERE UNO 1957.jpg

Kulia ni Lawi Sijaona, Abdul Sykes, Julius Nyerere, Dossa Aziz 1957,

ROBERT MAKANGE.JPG

Robert Makange

SHARIFF ABDALLAH ATTAS.jpg

Shariff Abdallah Attas

TATU BITI MZEE.JPG

Kulia Bi. Tatu bint Mzee, Bi. Titi Mohamed, kushoto Bi. Chiku bint Said Kisusa (mke wa Shariff Attas) na Mwalimu Nyerere​
 
Historia tamu na yenye kufunza, nimejifunza jambo.
 
Back
Top Bottom