SoC02 Umuhimu wa kuwepo, kusimamiwa na kutekelezwa kwa programu za stadi za maisha kwa watoto na vijana katika jamii

SoC02 Umuhimu wa kuwepo, kusimamiwa na kutekelezwa kwa programu za stadi za maisha kwa watoto na vijana katika jamii

Stories of Change - 2022 Competition

Tonytz

Senior Member
Joined
Jul 18, 2022
Posts
159
Reaction score
1,142
UTANGULIZI

Stadi za maisha maisha ni maaifa yanayotarajiwa kumsaidia mtu kuishi vema. (Nukuu kutoka Wikipedia)
Program ya stadi za maisha ni mkabala kabambe wa kubadilisha tabia unaotilia mkazo juu ya uendelezaji wa stadi zinazohitajika kwa maisha kama vile mawasiliano, utoaji wa maamuzi, kufikiria, kuhimili matendo, utetezi wa haki, ujenzi wa kujiheshimu, kukataa shinikizo rika na stadi za mahusiano. Pia kuongeza uwezo kwa wasichana na kuwapa maadili mapya wavulana. (Nukuu kutoka PEACE CORPS- Mwongozo wa Stadi za Maisha, 2001 ).

Maisha ni muambatano wa muda pamoja na matukio, hivyo ni muhimu kufahamu kuwa muda unavyozidi kwenda ndipo kiumbe hai kinapopata nafasi ya kupita katika matukio mbalimbali yaliyo mazuri na mabaya, ambayo yote huhitaji hekima na maarifa katika kuyapitia hususani yaliyo mabaya. (Nukuu kutoka Wikipedia).

Katika andiko hili nitajikita zaidi katika kuelezea vitendo(tabia) vinavyoonesha kutokuwepo kwa kuhimizwa na kutekelezwa kwa program za stadi za maisha katika jamii na athari zake, kanuni za kubadili tabia kulingana na program za stadi za maisha, umuhimu wa kuwepo na kutekelezwa kwa programu za stadi za maisha katika jamii na mwisho nitatoa hitimisho. Jambo la kuzingatia pia ni kuwa katika kujadili hayo nitajikita zaidi katika kuhusianisha program za stadi za maisha kwa watoto pamoja na vijana.

Mtoto au kijana anaweza kujifunza stadi za maisha nyumbani kwa kuiga vitu au tabia zinazotendwa na wanafamilia kama vile wazazi wake au Ndugu wanaomzunguka. Watoto na vijana huweza kujifunza stadi za maisha shuleni kutokana na mafunzo kutoka kwa walimu mfano hujifunzaji wa somo la stadi za kazi. Pia mtoto na kijana anaweza kupata elimu ya stadi za maisha katika taasisi za kidini kutokana na mafundisho yao kwa kuhimiza kuishi kwa upendo, kufanya kazi kwa bidii, makatazo, pamoja na kuenenda kwa hekima.

Pia katika jamii inayotuzunguka, mtoto au kijana anaweza kujifunza stadi za maisha kwa kujifunza stadi mbalimbali za maisha kama vile stadi za ujasiriamali.
Screenshot_20220828-172817_1.jpg

(Picha kutoka mtandaoni)
TABIA AU VITENDO VINAVYOONESHA KUTOKUWEPO, KUTOTILIWA MKAZO KWA PROGRAMU ZA STADI ZA MAISHA KATIKA JAMII ZETU HASA TANZANIA.
IMG_20220831_200358_079.jpg

(Picha kutoka mtandaoni-UTV, habàri,31/8/2022)
Katika jamii zetu nyingi za Kiafrika, kumekuwepo na vitendo ambavyo vinaonesha dhahiri kuwa yawezekana hakuna programu za stadi za maisha ama kama zipo basi hazitiliwi mkazo kwa namna yoyote ile. Hapa tuangazie macho baadhi ya vitendo au matukio ambayo kimsingi hayana tija kwa Taifa; viwango vya maongezeko ya virusi vya UKIMWI kwa baadhi ya mikoa hapa nchini kwetu, uenezwaji wa makusudi wa magonjwa ya ngono, kuwapo na mimba zisizotarajiwa, kukithiri kwa matukio ya utoaji wa mimba, vijana kuacha shule kutokana na kupata mimba, kujikita katika ulevi uliokithiri kama njia ya kuondoa msongo wa mawazo, kushiriki kwenye michezo ya kamali(gambling), utumiaji wa madawa ya kulevya kwa vijana na watu wazima, unyoaji wa nywele kwa mitindo isiyo ya staa mbele za watu, kuvaa mavazi yasio na staa mbele za wengine, kushiriki mapenzi kinyume na maumbile, kushiriki mapenzi ya jinsia moja, ulawiti kwa watoto, kurekodi na kupiga picha za utupu, uwepo wa makundi ya vijana waharifu mijini hujulikana kama Panya Rod. Vitendo hivyo na vingine vinavyofanana navyo nadhani kila mmoja anachukizwa navyo. Tujiulize kwa nini katika karne hii vimetawala sana na kuharibu vijana wengi na watoto wetu?

Watoto na vijana wengi huingia katika matukio magumu ya kimaisha kwa kukosa stadi za maisha; ambazo ni stadi binafsi, za kijamii, na stadi za maamuzi sahihi. Matokeo yake hupelekea vijana wawe ni watu wa lawama na kuishi maisha magumu na wasiyoyatarijia katika maisha yao.


Binafsi siwezi kusema nani alaumiwe lakini msomaji utakuwa na la kusemea kwenye hilo. Kikubwa ninachokiona na ninachokiamini katika magumu hayo au matukio hayo ni TABIA. Ni wazi kuwa kwenye jamii kila mtu ana tabia yake yawezekana ikawa nzuri au mbaya ambayo humwendesha mtu kwenye kile anachoamini.

Kwa mfano mtu anapokuwa na stadi binafsi humsaidia kujitambua, kutambua mahitaji na kuweka malengo katika maisha. Lakini sia ajabu kwa karne ya sasa kijana kuishi bila malengo hata kama ni msomi. Stadi binafsi ni muhimu sana kwa mstakabali wa maisha ya mtu mmoja mmoja. Wahenga walisema Wema ni Akiba. Vijana hatujatambua hili jambo kwa kuwa hatuna stadi za kijamii. Hii inajidhihirisha kwa kuishi maisha ya kibinafsi na kuwa na mawasiliano mabaya na kushindwa kuishi vizuri na watu ambao pengine ndiyo wa kutuinua. Yatupasa kubadili tabia na mienendo yetu watoto kwa vijana.

Screenshot_20220829-123149_1.jpg
Screenshot_20220829-123149_1.jpg

(picha kutoka mtandaoni)
KANUNI ZA KUBADILI TABIA

Kwa jinsi dunia ilivyobadilika yatupasa kubadili tabia na mienendo yetu. Ni kweli kubadili mwenendo na tabia iliyozoeleka ni vigumu, lakini tunaweza kubadili tabia na mienendo kwa kuzingatia baadhi ya kanuni zifuatazo za kiutekelezwaji;
Screenshot_20220829-121539_1.jpg

(Picha: kutoka mtandaoini- chapisho la peace corps)
  • Utoaji wa taarifa zinazoeleweka kwa urahisi na zenye kuwafaa wahusika unaowafikia. Taarifa zenye utata na ugumu kwenye kueleweka kuhusu kundi Fulani kunaweza kufanya kusiwe na utekelezaji wa stadi za maisha na kutobadili tabia za mtoto au kijana.
  • Kuwafunza watoto na vijana stadi za kujihusisha na tabia zinazokubalika. Kwa kuwapa mifano ya watu wanaoonesha tabia njema na mafanikio yao.
  • Kutoa au kutangaza tabia mbalimbali zinazoweza kupunguza hatari hasa katika maambukizi ya magonjwa ya zinaa, ili kulinda na kuokoa afya ya kijana na mtoto.
  • Kuacha kutoa ujumbe au matamko ya kutisha kwa watoto na vijana. Huweza kuwajengea woga na hivyo kuishi kwa hofu na mashaka na kushindwa kufikia malengo yao.
UMUHIMU WA PROGRAMU ZA STADI ZA MAISHA KATIKA JAMII.

  • Zinasaidia kujenga umahiri makini, kwani wahusika katika program hizo wanajifunza aina mbalimbali za kupambana na hali ngumu, kwa kufunzwa mbinu za kijasiriamali.
  • Hufanya washiriki kujadili tabia zifaazo katika jamii na kupuka sizizofaa.
  • Kuongezeka kwa afya ya akili na mwili, tabia ya kijamii na kupungua kwa shida za kijamii na tabia ya kujiharibu.
  • Humfanya mtoto na kijana kuishi maisha aliyoyatarajia na yenye malengo
  • Huepusha woga na ujikanaji
  • Hujenga hali ya uvumbuzi, ubunifu, utambuzi na umakini wa kiutendaji
Screenshot_20220829-122334_1.jpg

( Picha kutoka mtandaoni)

HITIMISHO.
Program za stadi za maisha ni kielezo chema cha kutokomeza umasikini, tabia mbaya, kwa kuongeza ujuzi wa kijamii, kihisia na kufikiri. Hivyo uwepo wake, itawasaidia watoto na vijana wa sasa kufikia malengo yao kwa kuimarisha uwezo wao ili kukidhi mahitaji ya jamii ya sasa na kufanikiwa. Serikali iweke mipango mkakati katika taasisi zake hasa katika elimu kuhakisha kunakuwa na utekelezwaji wa stadi hizo ili kupunguza wimbi la matukio mabaya.
 

Attachments

  • Screenshot_20220829-121249_1.jpg
    Screenshot_20220829-121249_1.jpg
    21.2 KB · Views: 13
  • Screenshot_20220829-121841_1.jpg
    Screenshot_20220829-121841_1.jpg
    36 KB · Views: 13
  • Screenshot_20220829-123941_1.jpg
    Screenshot_20220829-123941_1.jpg
    27.7 KB · Views: 11
Upvote 93
Back
Top Bottom