#COVID19 Umuhimu wa matumizi ya Barakoa (masks) katika kukinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona

#COVID19 Umuhimu wa matumizi ya Barakoa (masks) katika kukinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona

Status
Not open for further replies.

JamiiTalks

JF Advocacy Team
Joined
Aug 7, 2018
Posts
685
Reaction score
1,124
UTANGULIZI

Barakoa (mask) ni kikinga pua na mdomo na ni nyenzo muhimu inayoweza kutumika kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya vimelea vya maradhi kupitia njia ya hewa. Kuna aina mbalimbali za barakoa ambazo huandaliwa kwa madhumuni tofauti. Zipo aina kuu tatu (3) za barakoa ambazo zinaweza kutumiwa ili kuzuia maambukizi ya vimelea vya maradhi kuenea zaidi au kumkinga mtu asipate maambukizi kutoka kwa watu wengine endapo yupo katika maeneo hatarishi. ya hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya.

Barakoa zinazopendekezwa kutumiwa na wataalamu wa huduma za afya ili waweze kujikinga na kuwakinga wagonjwa na watu wengine ni Barakoa za upasuaji na Barakoa aina ya N95;

1. Barakoa za Upasuaji (Surgical Masks) ni barakoa za kawaida ambazo huvaliwa kwa lengo la la kumkinga mvaaji asisambaze majimaji yanayotoka katika njia ya hewa au mate wakati wa kukohoa au kupiga chafya kwenda kwa watu wengine. Aina hii ya barakoa inaweza kutumiwa na watoa huduma za afya wanaowaona au kuwahudumia wagonjwa wa nje (OPD) na wagonjwa wengine ikiwa ni pamoja na wanajamii wengine

2. Barakoa za N95 (N95 Masks) ni barakoa maalumu ambazo humkinga mtumiaji kuvuta vimelea vya magonjwa ikiwemo aina mbalimbali za virusi (mfano virusi vya Corona) kwa zaidi ya 95%. Barakoa za N95 zinashauriwa kutumiwa zaidi na watoa huduma za afya walio mstari wa mbele katika kuwahudumia wagonjwa wenye magonjwa ya mlipuko kwenye vituo vilivyoainishwa au kuandaliwa kwa ajili ya tiba za wahisiwa na wagonjwa waliothibitika. Hivyo aina hii ya barakoa inahitajika zaidi ndani ya hospitali na vituo vingine vya kutolea huduma za afya

3. Barua za Kitambaa (Cloth Masks) ni barakoa zinazoandaliwa miongoni mwa wanajamii kwa kutumia kitambaa. Inashauriwa barakoa hizi zitengenezwe kwa vitambaa vya pamba, ziwe na matabaka mawili au matatu ili kuziongezea ubora na uwezo wa kukinga na kupunguza uwezekano wa maambukizi kuenea zaidi.

MAKUNDI YA WATU WANAOTAKIWA KUVAA BARAKOA

Endapo mwenendo wa ugonjwa wa mlipuko unaoathiri njia ya hewa umefikia kiwango cha kuenea miongoni mwa wanajamii ni muhimu watu wote ambao wanachangamana na watu wengine na watu wanaoenda au kuingia kwenye mazingira hatarishi waweze kuvaa barakoa ili kujikinga na maambukizi. Makundi haya ni:

•Wahudumu wa afya (Wataalamu wa Afya wanaokutana au kuwahudumia wahisiwa au wagonjwa wa ugonjwa wa mlipuko kama vile Corona (COVI-19)

•Watu waliothibitika kuwa na ugonjwa wa Corona (COVID-19) au watu wenye dalili za maambukizi kwenye njia za hewa kama kikohozi, kupiga chafya au mafua

•Watu wanaomhudumia mgonjwa au wale walio karibu na mtu mwenye dalili za maambukizi kwenye njia ya hewa kama kikohozi, kupiga chafya au mafua

•Watu wote wanapokuwa wameondoka majumbani na kwenda kwenye maeneo yenye kuchangamana na watu wengine, wageni, maeneo yenye mikusanyiko na msongamano mfano katika vyombo vya usafiri, sokoni, nyumba za ibada (msikitini na kanisani) na maeneo ya shughuli nyingine za kijamii au kiuchumi

MATUMIZI SAHIHI NA NAMNA YA KUVAA BARAKOA

Ili kuhakikisha barakoa inakuwa nyenzo muhimu katika kukinga na kupunguza uwezekano wa maambukizi kuenea zaidi ni muhimu itumike kwa kuzingatia kanuni maalumu kabla ya kuvaa, wakati wa kuvaa na kuvua barakoa ikiwa ni pamoja na kuzingatia kanuni za afya katika utupaji wa taka (kuteketeza barakoa zilizotumika) Matumizi ya barakoa bila umakini yanaweza kusababisha kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya Corona.

Ni muhimu hatua zifuatazo zizingatiwe:
• Nawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au vitakasa mikono (sanitizers) kabla ya kuvaa barakoa • Vaa barakoa taratibu na uhakikishe inafunika pua na mdomo. Barakoa ifungwe kwa umakini na kuhakikisha hakuna upenyo kati ya uso na barakoa na kuhakikisha imebana vizuri sehemu ya pua karibu na macho, kwenye mashavu na chini ya kidevu. • Epuka kugusa barakoa ukiwa umeivaa

• Wakati wa kuvua barakoa usiiguse upande wa mbele; ivue kwa kufungua kamba za nyuma na kuitoa kwa kushikiria kamba hizo.

• Baada ya kuvua barakoa hakikishaunanawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au unatumia vitakasa mikono kabla ya kuvaa barakoa. • Barakoa za N95 na Barakoa za Upasuaji (Surgical Masks) zinatakiwa kuvuliwa baada ya masaa 4 hadi 6 na hutakiwi kurudia kuvaa barakoa iliyotumi ka, barakoa inatumiwa mara moja tu na haitakiwi itumiwe n mtu mwingine

• Epuka kurudia kuvaa barakoa za vitambaa (Cloth Masks) baada ya matumizi endapo hazijasafishwa au kutakaswa. Hakikisha unafua barakoa ya kitambaa mara tu baada ya kuivua na ifuliwe kwa maji na sabuni; ianikwe juani na kupigwa pasi kabla ya matumizi kwa siku nyingine.

• Barakoa iliyopata unyevu haitakiwi kuendelea kuvaliwa na ni muhimu ivuliwe maramoja .

• Hakikisha umeiteketeza barakoa baada ya kutumia au umeiweka kwenye sehemu maalumu ya kuhifadhi taka zenye maambukizi.

NAMNA SAHIHI YA KUVAA BARAKOA

• Hakikisha unanawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni au vitakasa mikono kabla ya kuvaa barakoa.

• Hakikisha barakoa yako haina tundu au uwazi wowote.

• Hakikisha upande wenye chuma laini umekaa kwa juu ya pua.

• Upande wa ndani wa barakoa huwa ni mweupe.

• Vaa barakoa yako na uhakikishe sehemu ya chuma laini umeibana vizuri usawa wa pua yako.

• Sawazisha barakoa yako kwa kuivuta mpaka chini ya kidevu chako.

• Usiguse sehemu ya nje ya barakoa ili kuepuka maambukizi ya virusi, na endapo utaigusa kwa bahati mbaya hakikisha unanawa mikono yako kwa sabuni au vitakasa mikono

Chanzo: Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Muongozo wa Kinga na Kuzuia Maambukizi Katika Jamii Dhidi ya Ugonjwa wa Corona
 
Status
Not open for further replies.
Back
Top Bottom