Unamjua ''Bamanga'' Katika Historia ya Uhuru na Mapinduzi ya Zanzibar?

Unamjua ''Bamanga'' Katika Historia ya Uhuru na Mapinduzi ya Zanzibar?

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
UNAMJUA ''BAMANGA'' AHMED SAID KHARUSI KATIKA HISTORIA YA UHURU WA ZANZIBAR?
Leo nimeletewa picha ya Ahmed Said Kharusi maarufu, ''Bamanga.''

Maktaba yangu ya picha imepambwa sasa na picha mbili za mzalendo huyu ambae hatajwi katika historia ya Zanzibar.

Nimemtaja Ahmed Rashaad Ali mara nyingi sana katika makala zangu zinazohusu historia ya uhuru na mapinduzi ya Zanzibar.

Ahmed Rashaad halikadhalika na yeye pia hatajwi popote katika historia ya Tanzania.

(Nilikuwa nikiliandika jina lake ''Rashad'' lakini hivi karibuni mwanae amenishahihisha na kunieleza kuwa jina la baba yake ni ''Rashaad.'')

Ahmed Rashaad alikuwa baba yangu na alinipenda sana.

Alipofariki mama aliwaambia wanae, ''Mpigieni simu Mohamed mwambieni baba yake amefariki.''

Nilikuwa nafanya kazi Tanga.

Nilikuja Dar es Salaam kuwahi mazishi ya baba yangu.

Mzee Ahmed Rashaad alinisomesha historia ya Zanzibar na ya Tanganyika na kunieleza mengi ya ndani ambayo mengine nimeyaeleza na mengine bado sijayasema.

Ahmed Rashaad alikuwa rafiki ya Abdul Sykes toka udogo wao wako shule ya msingi katika miaka ya 1930.

Mzee Rashaad anasema alifahamiana na Abdul Sykes 1936 jengo la Arab Association na wote walikwenda pale wakiwa wameongozana na wajomba zao.

Ilikuwa wakati wa ''Sports,'' ambapo Wazanzibar wanakuja Dar es Salaam na mwaka unaofatia jamaa kutoka Dar es Salaam wanakwenda Zanzibar kwa ajili ya michezo.

Sports imedumu hadi hivi sasa.
Jina la Bamanga kwa mara ya kwanza nimelisikia kutoka kwa Mzee Rashaad.

Kwa miaka mingi sana nilikuwa najaribu kumshawishi Mzee Rashad tuandike maisha yake lakini akawa anakataa.

Ahmed Rashaad alikukuwapo na Abdul Sykes siku Abdul alipokutana na Jomo Kenyatta na viongozi wenzake wa Kenya African Union (KAU) Nairobi mwaka wa 1950.

Kisa hiki nimekieleza mara nyingi naamini wengi wanakifahamu.

Sikuchoka kumshawishi Ahmed Rashaad kuwa tukae kitako tuandike maisha yake.

Siku moja bila kutegemea Mzee Rashad alinikubalia.

Sikumwambia tuanze siku fulani.
Nilimuomba tuanze hapo hapo.

Mzee Rashad alianza na kisa cha yeye na rafiki yake Ahmed Said Abdullah Kharusi maarufu kwa jina la Bamanga walipoamua kuanzisha chama walichokiita Haki za Binadamu (HK).

Chama hiki baadhi ya Wazanzibari walikiita ''Chama Cha Wendawazimu,'' sababu ikiwa ni chama kilichokuwa kimeanzishwa na vijana machachari.

Siku ile tuliandika sura moja ya kitabu iliyokuwa na mvuto wa pekee kwani vijana hawa walifanya jambo ambalo halikupata kufanyika Zanzibar jambo ambalo lilisababisha hofu mji mzima.

Ahmed Rashaad na Bamanga walimwaga makaratasi ya uchochezi dhidi ya serikali na palikuwa na onyo kwa serikali.

Vyombo vya usalama vikaingia kazini.

Bamanga na sahib yake Rashaad walikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la ''sedition.''

Kesi hii ilivutia hisia za wengi kwani vijana wote wawili walioshitakiwa walikuwa wanatoka nyumba kubwa za watawala.

Imekuwaje watoto hawa wa viongozi wanafanya jambo kama lile la kushawishi watu wafanye uasi dhidi ya serikali inayoongozwa na wazee wao?

Kosa lilikuwa kubwa na lililobeba adhabu kubwa vilevile.

Hakimu Mdahoma alikuwa akiogopewa kwani hakuwa mtu wa mchezo na yeye ndiye aliyekuwa akisikiliza kesi hii.

Mashahidi walipatikana baada ya uchunguzi na ushahidi ulikuwa umekamilika barabara.

Zanzibar yote ilihamia mahakamani watu wamejazana kuja kusikiliza kesi.

Ahmed Rashaad alikuwa mtangazaji maarufu wa Sauti ya Unguja na Bamanga mwanamasumbwi aliyekuwa akitisha wapinzani wake.

Wale vijana wawili mbele ya Hakimu Mdahoma walikuwa watoto waliocheza na wanae udogoni na wote akiwajua vyema.

Lakini kwa mara ya kwanza katika historia ya mahakama Zanzibar licha ya kuwa na ushahidi uliokamilika mashahidi wote walibadili kauli zao mahakamani walipoanza kuhojiwa na Mwendesha Mashtaka.

Mzee Rashaad alikuwa mzungumzaji hodari akipenda ku-dramatise mambo.

Utapenda akihadithia, "trial scene," yaani yale yaliyotokea pale mahakamani vipi yule Mwendesha Mashtaka," aliyeingia mahakamani kwa mbwembwe ghafla alivyokuja kulowa.

Kila ninapoifikiria kesi hii namkumbuka mwalimu wangu wa fasihi Miss Menez alipokuwa akitusomesha, ''The Merchant of Venice,'' tumefika pale Shylock yuko mahakamani anadai ratili yake moja ya nyama aikate kutoka kwenye mwili wa Bassanio.

Mwalimu wangu huyu Miss Menez bingwa wa lugha ya Kiingereza kama alivyokuwa Mzee Rashaad alikuwa hodari wa ''dramatics.''

Kesi ilikuwa ya kufungua na kufunga Shylock Myahudi Mla Riba alikuwa anasubiri kupewa haki yake.

Hakimu Mdahoma na yeye alikuwa anasubiri kutoa hukumu yake.

Jana yake Mzee Rashaad anasema mashahidi walitembelewa na wakwezi kutoka shamba wote wamevaa ala zenye visu vikali na virefu.

Wakwezi hawa walikuja pia mahakamani siku ya kesi kama wasikilizaji na wale mashahidi waliwaona.

Hapo ndipo ushahidi wote ulipovurugika.
Huwa nikifika hapa naikumbuka ''scene'' moja katika ''The Godfather II,''

Mwendesha Mashtaka alipomleta shahidi wake aliyeamini kuwa ushahidi wake utamtia Don Michael Corleone hatiani na huo kuwa mwisho wa ujambazi wake.

Shahidi huyu alipomwona mmoja wa jamaa zake kutoka Cicily yuko pale mahakamani hapo hapo akabadili kauli yake na kuvuruga ushahidi wote uliokuwa umekamilika.

Ushahidi aliokuwanao Hakimu Mdahoma ulikuwa umemwagiwa maji baridi.

Hakimu Mdahoma katika kufuta kesi ile alikuwa kajaa ghadhabu na akasema kuwa mashahidi wametishwa.

Kwa hakika na bila shaka yoyote kisa cha wazalendo hawa wawili Bamanga na Ahmed Rashaad ni kisa cha kusisimua katika historia ya Zanzibar na historia ya Mapinduzi yalikuja kutokea miaka 12 baadae.

Hatukupata kukaa kitako tena kuendelea na kitabu chetu kwani Mzee Rashad alilazwa hospitali na kufariki muda mfupi akiwa kaniachia sura moja tu ya kitabu cha maisha yake tulichokusudia.

Sikuweza kuchapa kitabu chenye sura moja tu.

Nilipokuja kutafsiri kitabu cha Abdul Sykes mwaka wa 2002 kwa Kiswahili niliamua kuwaongeza Ahmed Rashaad Ali na Ahmed Said Kharusi (Bamanga) ndani ya tafsiri hii.

PICHA:
1. Bamanga
2. Ferej Abadi
3. Yusuf
4. Eddy Mbaraka
5. Naji
6. Turhan Ali Mdogo
7. Saleh Hassan Sheikh
8. Jabir
9. Saleh Ba Saleh
10. Mahfudh Salim

Picha ya pili wa pili waliosimama ni Bamanga.

1664128440715.png
1664128481572.png
1664128518923.png
1664128549620.png
 
Back
Top Bottom