SoC04 Unaonaje Tanzania ikawa hivi baada ya miaka mitano?

SoC04 Unaonaje Tanzania ikawa hivi baada ya miaka mitano?

Tanzania Tuitakayo competition threads

Kashmill

New Member
Joined
Jun 29, 2024
Posts
1
Reaction score
0
TANZANIA NINAYOITAMANI BAADA YA MIAKA MITANO

Kila kitu katika hii dunia lazima kupitia nyakati tatu, wakati uliopita ambao unakuwa kama sehemu ya kurejelea yote tuliofanya nyuma, wakati uliopo ambao kwa asilimia nyingi hujengwa na wakati uliopita na wakati ujao ambao nao hujengwa na kuwa imara kwa wakati uliopo ukiwa na mipango thabiti.

Hakika Kila kitu kinawezekana kwa Tanzania kuwa nchi ya kuigwa katika maendeleo Afrika na duniani, lakini kama ilivyo kesho bora inajengwa na leo yenye mipango madhubuti ambayo ilichochewa na jana kama sehemu ya kurejelea.

Ikumbukwe Mh. Ali Hassan Mwinyi ndie aliyetengeneza na kubadili uchumi wa Tanzania kwa kuangalia mafanikio ya nchi na ya kila mwananchi wakati kabla hajaingia madarakani, huo ni mfano unaonyesha kuwa Mzee Mwinyi alitumia wakati wa jana kama funzo ili kuitengeneza leo, na mpaka leo maamuzi yameisaidia Tanzania kuwa hapa ilipo.

Kwa Sasa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo hazikaukwi midomoni kwa watu duniani kutokana na mikakati yake ya maendeleo katika sekta zote, ambapo Serikali ndio muhimili mkuu wa maendeleo hayo.

Naweza kuizungumzia Tanzania kwenye miaka mitano ijayo nikihusisha na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, na katika kulizungumzia hilo nitaangalia sekta muhimu mno ambazo ndio mihimili ya kila nchi iliyofanikiwa.

Aliwahi kusema Baba wa Taifa, Mwl. Julias Kambarage Nyerere kuwa nchi yetu inapaswa kupambana na maadui watatu, ujinga, umasikini na maradhi, hivyo nitaanza na sekta ya elimu.

Baba wa Taifa ni miongoni mwa watu walioingia katika vitabu vya wengi kutokana na uwezo wake wa kufikiria, Baba wa Taifa alikuja na elimu ya ujamaa na kujitegemea, hii ilikuwa ni miongoni mwa elimu bora sana ambayo ingetiliwa mkazo huenda Tanzania isingekuwa hapa.

Kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, natamani kuiona Tanzania ikiivalia njuga elimu, wanafunzi wasome zaidi kwa vitendo, tusiwe nyuma, kama ni teknolojia watafutwe wataalamu wapelekwe mashuleni, ili mwanafunzi akitoka shule anakuwa ni miongoni mwa watu wanaokuza uchumi wa nchi kutokana na elimu wanayopatiwa shuleni.

Hivyo basi natamani kuona baada ya miaka mitano mtaala wa elimu ya Tanzania umejikita zaidi katika elimu kwa vitendo, kwa elimu hiyo hakika Tanzania itapunguza tatizo la ajira kwa kiasi kikubwa.

Upande wa uchumi ambapo hapa tunapambana na adui wa umasikini, kutokana na sayansi na teknolojia, uchumi katika sehemu zote unategemea sana teknolojia, nchi zilizoendelea mapato yao mengi wanayapata kupitia bidhaa wanazotengeza.

Baba wa Taifa alituachia zaidi ya viwanda elfu moja, lakini hii leo asilimia kubwa ya viwanda hivyo vimekufa, kwahiyo leo iwe sehemu ya kuangalia shida iko wapi, kama sisi ni miongoni mwa nchi tunaozalisha malighafi, je kilichofanya viwanda hivyo kufa ni nini?, je ni ukosefu wa wataalamu wa kuendesha viwanda hivyo? Tukijibu mwaswali hayo na kuyafanyia kazi naamini Tanzania baada ya miaka mitano itakuwa imepiga hatua sana.

Kwa upande wa adui wa mwisho ambae ni maradhi, kwanza naipongeza nchi yangu, kwenye upande wa afya iko vizuri sana, Wizara inayohusika na afya nawapa kongole zenu, natamani kuiona sekta ya baada ya miaka mitano ikitumia zaidi teknolojia ya kisasa ili kuzidi kurahisisha huduma kwa wananchi.

Tanzania mpaka sasa kuna matibabu ambayo awali ilikuwa lazima uende India kwa ajili ya matibabu, lakini leo yetu sio kama jana yetu, magonjwa ya moyo, magonjwa ya figo na magonjwa mengine makubwa yanatibika Tanzania, kwa yale ambayo bado hayawezi kutibiwa Tanzania na matamanio yangu baada ya miaka mitano kuona kila gonjwa linatibika nchini.

Baada ya kuzungumzia maadui hao watatu aliotuachia Baba wa Taifa tupambane nao ambao kwa asilimia kubwa tumepambana nao na tupo sehemu nzuri, naomba nizungumzie kuhusu sekta hizi ambazo pia ni muhimu mno.

Sekta ya kilimo, natamani baada ya miaka mitano Tanzania kwenye upande wa kilimo inaongeza utumiaji wa teknolojia ili kuendana na viwango vya soko la dunia kwa upande wa mazao, teknolojia iyongezeke katika umwagiliaji ili kujihakikishia mda wote mazao, pia teknolojia itumike katika ufugaji ili kuongeza bidhaa zinazotokana na ufugaji.

Sekta ya nishati na miundombinu, hii ni sekta muhimu sana, natamani kuiona Tanzania baada ya miaka mitano ikiwa haina foleni barabarani, Tanzania ambayo tunaweza kukaa mwaka mzima bila umeme kukatika, Tanzania ambayo kujaza mtungi mdogo wa gesi iwe ni elfu nne au elfu tano, naamini Tanzania kwa mabadiliko hayo itanawiri na kuvutia wengi duniani.

Na upande wa siasa, tumeona awapo ya sita ya serikali inayoongozwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amefanya makubwa ambayo hayakutarajiwa kwenye upande wa siasa, kuwaruhusu vyama pinzani kufanya mihadhara ya wazi, kufanya maandamano kwa amani na ulinzi kutoka jeshi la Polisi, ni mambo ya kuvutia mno, kwahiyo natamani mengi yaongezeke na baada ya miaka mitano ijayo natamani vyama viwe vinakaa meza moja ili kushauriana katika kuijenga Tanzania bora.

Hayo ndio matamanio yangu ambayo mabadiliko yake yanaanza sasa, dunia inapitia mabadiliko ya sayansi na teknolojia ambayo yanabadilika kwa kasi mno, kwahiyo natamani kuiona Tanzania baada ya miaka mitano inaendana na kasi hii ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika sekta zote.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom