Unapata taarifa sahihi zisizopotoshwa?

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363

KWA UFUPI

  • Aliondoka jana saa sita mchana na ndege ya ‘Airforce One’ kuelekea Washington kupita Senegal.



Soma kwa makini sentensi zifuatazo na utoe maoni yako. Inawezekana ufafanuzi uliotolewa haukuwa wa wazi, hivyo kutaka kupata maelezo zaidi. Lengo ni kuhakikisha kuwa wasomaji wengi watapata taarifa zilizo sahihi na zisizopotoshwa.

Kwa mfano:“ Kwa maana nzima sasa hatuwezi kusonga mbele kama hatutazalisha walimu wa kutufundishia watoto wetu.”

Mwandishi anatakiwa kuandika kwa kutumia maneno machache na yanayoeleweka. Maneno mengi yasiyoongezea tija katika taarifa yako hayafai.

Kwa mfano, katika maneno manne ya mwanzo ya sentensi hii hayafai kuandikwa. Maneno hayo ni “Kwa maana nzima sasa…” ni ‘blabla’ tu na yanaweza kuondolewa bila kuharibu maana.

“ Aliondoka jana saa sita mchana na ndege ya ‘Airforce One’ kuelekea Washington kupita Senegal.”

Maneno yaliyozoeleka kutumika katika kuelezea muda ni alfajiri, asubuhi, adhuhuri, mchana, alasiri, jioni na usiku. Kipindi cha mchana kinaanzia saa sita hadi saa nane. Saa tisa hadi saa kumi ni alasiri. Kwa usahihi angeandika adhuhuri kama ni saa sita mchana angeandika adhuhuri.

Kwa taarifa iliyotolewa hapo juu ni ‘adhuhuri’ ni neno sahihi badala ya ‘saa sita mchana’.

“ Lohan yuko katika kituo maalumu cha kuacha madawa na anatarajia kumaliza muda wake mwishoni mwa mwezi ujao.”

Baada ya kueleza kwa muda mrefu kuwa neno dawa halina wingi, bado lipo tatizo la kutozingatia misingi ya Kiswahili kwa baadhi ya waandishi wetu. Wamezoea kutumia ‘madawa’ badala ya dawa. Hili ni kosa.

“ Peter Ouma alisema kuwa tukio hilo lilitokea Julai 11.15 usiku katika Kijiji cha Igogo wilayani Igunga.”

Kwa kufafanua zaidi matumizi ya nukta na nuktapacha yanakanganya. Yafaa nieleze kuwa wakati wa kuandika kiasi cha fedha au saa na dakika tunatumia alama ya nukta. Kwa mfano, shilingi 12.50 , saa 12.15. Kwa matumizi ya vipimo tumatumia kilogramu 2.76. Hata hivyo, tunapotenganisha nukta na sekunde, tunatumia nukta mbili na kwa neno moja ni nuktapacha. Kwa mfano saa 12.30:20. Haya ni maelezo ya nyongeza kwa waandishi siyo wa magazeti tu, hata wale waandishi wa makala, vitini na vitabu.

“Watoto hao ambao ni wanafunzi wa darasa la kwanza na la tatu katika shule mbalimbali mjini humo, wamedai wamesimamishwa shule.”

Badala ya kuandiki shule mbalimbali tunatumia shule tofauti.

“Miongoni mwa nchi zilizowahi kuwa na machafuko ya ndani ni nyingi katika Bara la Afrika, huku baadhi zikingali na machafuko hadi leo.”

Matumizi ya ngali na ngeli yanawakanganya waandishi wengi. Unaweza kuepuka na hali hii kwa kutumia zikiwa bado, badala ya zingali. Kwa hiyo sentensi isomeke;

“Miongoni mwa nchi zilizowahi kuwa na machafuko ya ndani nyingi katika Bara la Afrika na baadhi zikiwa bado na machafuko hadi leo.”

“Kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari, muziki huu ulianzishwa mnamo miaka ya 1930 ukiwa na mandhari ya rumba na ukiwa rahisi kuimbwa au kuchezwa na mtu yeyote.”

Mwandishi amechanganya maneno mandhari na mahadhi. Maana ya mandhari ni sura ya mahali aghalabu ardhi panavyoonekana.

Mahadhi ni upandaji na ushukaji wa sauti wakati wa kuimba. Kwa wale wataalamu wa nyimbo linatumika neno ‘rhythm’. Kwa hivyo neno ukiandika mahadhi ya rumba umelitumia neno mahadhi kama ipasavyo.

“Lengo la makala haya ni kuwaasa wanamuziki wawe makini kuulinda muziki huu kuuigiza ulikotoka yaani Kongo.”

Sentensi hii ni sahihi ila kama unataka kuiboresha zaidi ungeweza kuandika, … kuwaasa wanamuziki kuwa makini kuulinda muziki huu…”

“ Rafiki wa karibu wa Kaseja ameitonya Mwananchi jana kuwa kipa huyo kwa sasa yuko nje ya jiji na kwamba anatarajia kuzungumza kuhusu hatima yake Simba Jumapili wiki hii.”

Matumizi ya neno ‘tonya’ yanaweza kueleweka katika lugha ya mazungumzo, lakini halijasanifiwa bado.Kwanza halipo neno tonya katika kamusi zetu. Kwa hiyo tungetumia neno ‘kufahamisha’ au ‘kutanabahisha’.

Tutaendelea na mjadala huu wiki ijayo. Unapata taarifa sahihi zisizopotoshwa? - Makengeza - mwananchi.co.tz

 
huu ni mjadala mzuri sana, nasikitika kuuona umekosa wachangiaji ila mada za ajabu sana zinapata nafasi kule chitchat na jukwaa la mapenzi
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…