Unaujua mtego wa wauaji wa ndoto zako katika maisha?

Unaujua mtego wa wauaji wa ndoto zako katika maisha?

mwakavuta

Member
Joined
Sep 22, 2020
Posts
99
Reaction score
306
Je ni biashara gani ulikusudia kuifanya lakini ukaahirisha kwa sababu kuna mtu alikuambia haifai kufanya na ukaua ndoto zako milele? Watu wengi wanakutana na wauaji wa ndoto kila siku na bahati mbaya sana ni wachache wanaofanikiwa kuwakwepa na kuendelea kufanya kazi ndoto zao.

Umepata wazo la biashara linalokuvutia lakini hauna Imani nalo? Au una mashaka jinsi ya kulitekeleza? Hauko peke yako kila mtu aliyefanya maamuzi ya kuanzisha biashara alipitia mtihani huu vilevile kila mtu aliyekuwa na wazo la kuanzisha biashara akashindwa kulitekeleza alikwamishwa na mtihani huu kwa sababu hakufanikiwa kufaulu ili atekeleze ndoto zake.

Mtihani ambao unaamua mtu atekeleze wazo Fulani la biashara au jambo lolote lile unatokana na hisia za mashaka na wasiwasi wa kutofanikiwa au kutokukubalika na watu wanomzunguka kutoka ndani kabisa kwa mtu mwenyewe kuhusu aina ya biashara anayokusudia kuitekeleza. Mtihani huu una maswali makuu yafuatayo;

  • Hivi hii biashara ni halali?
  • Nitaweza kuifanya?
  • Ni nani ninayemfahamu aliyefanikiwa kwa kufanya ninachokusudia kukifanya?
  • Watu wanaonizunguka watanifikiriaje nikifanya biashara ya aina hii?
  • Je nina maarifa ya kutosha kufanya biashara hii?
  • Vipi kama nikifanya biashara hii nisifanikiwe? Nitaweza kurudisha gharama zangu?
Maswali kama haya na mengine mengi ndiyo yanayozunguka kwenye akili za watu wengi wakati wanapofikiria kufanya jambo fulani hasa linalohusu biashara na uchumi wao. Sio kosa kujiuliza maswali haya, ni mtihani ambao unatokiana na asili ya kimaumbile ya mwanadamu (nature of human being) kutafuta usalama kabla ya kufanya jambo lolote. Mtihani huu unapatikana katika kila jambo ambalo mwanadamu anataka kulifanya iwe ni kuanza mahusiano, kuanzisha familia, biashara, safari, kusoma, kujenga nyumba na mengine mengi ambayo mtu anataka kuyafanya. Kinachokuwa tofauti ni lugha ya maswali ndiyo hubadilika kutoka na jambo au tukio linalotaka ulifanyie maamuzi lakini yote yanalenga kuhakikisha kuwa maamuzi atakayochukua mtu husika yatamfanya awe salama kwenye jambo lenyewe na mitazamo ya watu wanaomzunguka.

Bahati mbaya sana ni kwamba ni mara chache sana watu wanafanikiwa kujibu maswali ya mtihani huu wao wenyewe, hivyo hujikuta wakiangukia kwenye mtego wa kutafuta majibu kutoka kwa watu wengine ambao bila kujua watu hao hugeuka kuwa wauaji wa ndoto zao (dream killers) ama kwa kukusudia au kwa sababu na wao hawajui majibu ya maswali hayo kwa usahihi. Ni watu wachache sana wanapata majibu kutoka kwa watu wengine ambayo yatawaruhusu kuendelea na kutekeleza mpango wao. Mara nyingi watu wanaotoa msaada wa kujibu maswali haya hugeuka kuwa wauaji wa ndoto za wengine kwa sababu zifuatazo.

  • Hawajui kwa undani kuhusu biashara au jambo husika walilouzwa,
  • Hawapendi kufanya biashara au jambo husika hivyo huzuia wengine wasifanye pia,
  • Waliwahi kufanya biashara au jambo husika na wakashindwa kutokana na madhaifu yao binafsi hivyo, hudhani kuwa madhaifu yaliyowasabisha wao wakashindwa yatawafanya na wengine washindwe pia.
  • Hawahitaji kuona watu wengine wakifanikiwa kupitia biashara au jambo husika.
  • Hawataki waonekane kuwa wameshindwa kutoa majibu ya maswali wanayoulizwa na wengine. N.k
Kutokana na mamlaka tunayowapa watu hawa tunajikuta tunashindwa kukataa maamuzi wanayotuamulia bila kujali mambo kama hayo niliyotaja hapo juu na mengine mengine mengi. Nini kinafuata? Ndoto zako huishia hapo kwa sababu kuna mtu amekuambia kuwa usifanye sio jambo au biashara nzuri.

Naomba nisinukuliwe vibaya, sipingi kuomba ushauri kwa watu wengine kuhusu jambo unalotaka kufanya iwe biashara au jambo lolote lile lakini, ni vyema kujitahidi kutaka majibu ya maswali hayo mwenyewe (uyajibu mwenyewe kadri ya uwezo wako), pale unaposhindwa kupata majibu husika ndipo utafute majibu kwa watu wengine kwa kuzingatia vigezo muhimu ambavyo vitakufanya usiangukie kwenye mtego wa wauaji wa ndoto zako, baadhi ya vigezo hivyo ni;

  • Je, mtu huyo ana nia ya dhati ya kukuona unafanikiwa?
  • Je, mtu huyo ana uzoefu au maarifa ya kutosha kuhusu biashara au jambo husika unalotaka kumuuliza?
  • Je, mtu huyo ana mtazamo chanya kuhusu jambo au biashara husika?
  • Je, kama mtu huyo hajui kuhusu unachomuuliza anaweza kukuelekeza kwa mtu sahihi ambaye anaweza kukusaidia kwa usahihi kupata majibu ya maswali yako?
Kwa kuzingatia vigezo hivi unaweza kuepukana na mtego wa waua ndoto zako na ukaanza safari mpya ya kufikia malengo kama utaamua kutafuta majibu sahihi kutoka kwa watu sahihi na mitazamo sahihi. Mwandishi mmoja wa vitabu alisema kuwa, “kila mtu yupo hatua sita kutoka kufahamiana na watu wote ulimwenguni”. Inawezekanaje? Kwa kutaka kuhusiana na rafiki wa rafiki zetu na rafiki wa marafiki zao, kadri utakavyojitahidi kutaka kujua zaidi kutoka kwa jamaa na rafiki watakaokuwa tayari kukutambulisha kwa watu wanaowafahamu ambao wana uelewa mpana zaidi ni rahisi sana kuwa salama na mtego wa wawindaji na wauaji wa ndoto zako. Kumbuka hakuna jambo ambalo halina majibu katika ulimwengu ni kwamba hatufanikiwi kukutana na watu wanaojua majibu ya maswali yetu.

Usiue ndoto zako kwa sababu hazikukubaliwa na mtu uliyemuomba majibu ya mswali yanayohusu biashara au jambo lolote ulilokusudia kulifanya. Kumbuka kuwa wewe ndiye mtu sahihi zaidi wa kujibu maswali yanayotakana na ndoto zako. Unapokutana na watu wanaokuzuia kuanza kufanya biashara au jambo lolote wakati mwingine ni kwa sababu hawana taswira halisi ya maono yako yako hivyo watakupa majibu yanayotokana na ufinyu wa taswira waliyonayo kuhusu maono yako. Hivyo ni vyema kujibu mtihani huo mwenyewe kwa sababu wewe peke yako ndiye unayejua uzuri na fahari ya maono yako.

Naomba tutumie uzi huu kuuliza na kupata majibu sahihi yua maswali yetu kutoka kwa members wenzetu ambapo naamini kwa jamii forum hakuna swali lisilo na majibu sahihi, huu ni ulimwengu wetu.

KUMBUKA! Unapoelekeza mawazo yako kuona ubaya wa kitu utaupata hata kama jambo au kitu hicho sio kibaya. Jitahidi kuwa na mtazamo sahihi na chanya kila siku.
 
Hakika umenena vyema...

Kama uwezo unao, nia unayo na sababu unayo chukua hatua tenda...
 
Back
Top Bottom