Ungemnunia Mangwea, kazi yake ingekupa tabasamu

Ungemnunia Mangwea, kazi yake ingekupa tabasamu

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Joined
Apr 29, 2016
Posts
20,743
Reaction score
25,564
APRILI 8, 2012, ilikuwa Pasaka. Wakati huo nilikuwa Mhariri Mwandamizi wa magazeti ya Global Publishers LTD, vilevile Mratibu Mkuu wa Matukio wa kampuni. Na kwa nafasi hiyo, pia nilikuwa Mwandaaji Mkuu wa matukio kwenye ukumbi wa Dar Live, uliopo Mbagala Zakhem.

Kipindi hicho, Dar Live utaratibu wetu ulikuwa mzigo kwa mzigo, back-to-back. Kila Jumapili ya wiki tulikuwa na maonesho makubwa ya burudani. Hata hivyo, sikukuu zilikuwa na uzito zaidi.

Sasa, Pasaka 2012, kwa uzito wake wa kisikukuu, iliipendeza kamati yetu ya maandalizi kuwasaini wanamuziki; Juacali (Kenya), Sir Nature na Ngwair kuwa waburudishaji wakuu. Kulikuwa na wasindikizaji wengine.

Kuelekea makubaliano ya Pasaka 2012; Juacali tulimsaini kupitia kampuni ya wakala wa wasanii ya Unity Entertainment ya AY. Nature mkataba wake na Dar Live ulikuwa wa mwaka mzima. Ikabidi nifanye mazungumzo na Ngwair.

Nilipomwambia Ngwair kuhusu nia yetu ya kutaka kufanya naye kazi Dar Live, aliniambia mazungumzo yote yafanywe na aliyekuwa meneja wake, Tippo, Mkurugenzi wa Zizzou Fashion.

Nilipowasiliana na Zizzou na kumweleza alichokisema Ngwair kuwa yeye ndiye asimamie mazungumzo ya kibiashara, alicheka.

Akaniuliza: “Kila siku anachukua pesa za shoo bila kunishirikisha, hii ndio ameona ipitie kwangu?” Nikamjibu kuwa labda ndio aliamua kubadilika. Tukazungumza, tukakubaliana na kusaini mkataba.

Siku ya shoo, mchana, Tippo akanijulisha kuwa Ngwair alikuwa Mwanza kikazi na hiyo kazi angemaliza saa 3 usiku. Ahadi ikawa, baada ya hiyo kazi ya Mwanza, angechukua ndege mpaka Julius Nyerere International Airport, kisha angekwea mkebe mpaka Dar Live.

Matarajio yakawa mpaka saa 5:00 usiku, Ngwair angekuwa ameshafika.

Jioni ya shoo, Dar Live ikawa imeshafurika. Kila mara nikawa na wasiwasi kuhusu Ngwair. Unajua mambo ya shoo, watu wanamfuata msanii wanayemtaka. Tulishamtangaza Ngwair, kama asingefika, waliohudhuria kwa sababu yake, tungewaambia nini? Vipi wangeamua kufanya vurugu na kuharibu mali?

Kwa kupima uzito, jinsi nilivyopanga ratiba ya awali, ilikuwa Ngwair angeanza, halafu Nature, kisha Juacali angefunga. Ngwair alifanya ratiba ibadilike. Nature akaanza, Juacali akafuata. Ngwair angefunga.

Muda ukawa unayoyoma, mpaka Nature akiwa na timu yake ya Wanaume Halisi, walipopanda jukwaani, Ngwair alikuwa hajapanda ndege Mwanza. Uzuri, Tippo alikuwepo Dar Live. Kila mara nikawa namuuliza, hakuwa na majibu yenye kunyooka.

Kwa mwenye kunifahamu, anaelewa kuwa kama jambo ninalolitaka likiwa haliendi sawa ni kwa kiasi gani huwa ‘napanic’ haraka. Hivyo, chelewa ya Ngwair ilinifanya nipanic.

Sasa, panic zangu nikazielekeza kwa Tippo. Kila mara nikawa namuuliza Ngwair alipofika. Unamuuliza sasa hivi, anakujibu yupo njiani anakwenda Airport Mwanza, baada ya dakika tano, unamuuliza tena. Nilimsumbua sana Tippo. Kuna wakati nilimlaumu kwa kitendo cha kumkabidhi pesa zote Ngwair. Tippo naye kama alipanic, akanijibu, ikiwa Ngwair asingetokea angerejesha pesa.

Baada ya jibu hilo la Tippo, sikumuuliza tena. Nilijua kakasirika. Jukwaani shoo ilikuwa inaendelea. Juacali alikuwa anapiga kazi na alielekea kumaliza. Ngwair hayupo. Tungewafanya nini wana-Dar Live waliofurika?

Watu walikuwa wengi sana. Juacali aliposhuka, ikaonekana mashabiki bado walikuwa na kiu ya burudani. Aliyekuwa bosi wangu, Eric Shigongo, akaniambia lazima tufanye kitu ili kuwafanya wana-Dar Live waendelee kuburudika.

Uzuri wa siku hiyo, Juacali alisindikizwa Dar Live na Fid Q, AY na MwanaFA. Ni kwa sababu AY ndiye alikuwa wakala wa Juacali. Na kwa vile FA na Fid Q ni marafiki wa AY, sikushangaa wao kuwepo.

Mimi na Shigongo tukajadili; tuzungumze na mwanamuziki gani haraka ili awafanye wana-Dar Live waendelee kufurahia siku? AY, FA au Fid Q? Je, nani angekuwa tayari? Kura zikamuangukia Fid Q.

Nikamvuta chemba Fid. Akanijibu alikuwa tayari kwa kazi, apewe pesa ili kieleweke. Tukajadili. Mfukoni nilikuwa na kiasi, nikamhesabia. Nikamwambia kinachobaki aibuke ofisini (Bamaga wakati huo), achukue na asaini. Tukakubaliana.

Nikamwita DJ wetu Dar Live wakati huo. marehemu DJ Juce ili apange shoo na Fid. Muda bila kuchelewa, Fid alikuwa jukwaani. Watu waliamka. The Swagger Don yupo jukwaani, unategemea nini?

Fid akiwa anaendelea kuifanya hadhira ifurahie wakati mzuri ndani ya Dar Live, nikapewa taarifa kuwa Ngwair amefika. Eti na mimi nikawa nimemnunia Ngwair kwa kuchelewa. Tippo akaniambia “haya mtu wako huyo hapo.” Sikutaka hata kumtazama usoni Ngwair. Uzuri hata yeye Ngwair hakuwa na shobo na mimi.

Nilimwambia DJ achukue instrumentals za Ngwair na maelekezo ili kazi ifanyike. Fid aliposhuka, Ngwair alipanda. Hali ya hewa ikabadilika.

Ngoma baada ya ngoma, Ngwair akaifanya Dar Live iwe kama hakukuwa na mwanamuziki mwingine kabla yake. Utadhani jukwaa alilopanda, hakupita Nature, Juacali na Fid Q muda mchache kabla.

Ngwair aliichukua shoo, akaimeza. Akamfanya kila aliyekuwa jukwaani aimbe naye wimbo kwa wimbo. Mikasi ambayo ni collabo la wengi lakini hakumhitaji Mchizi Mox, Mkoloni, Rah P wala P Funk. Hadhira aliyoiburudisha iliziba mapengo yote, kisha, ikawa bonge la burudani.

Aliniudhi ndio, akanipandisha presha kwa alivyochelewa. Hata hivyo, burudani ambayo Ngwair alikuwa anaishusha Dar Live ilikuwa si ya kununiwa. Nikawa natabasamu. Nachekacheka. Tippo aliniona nilivyokuwa natabasamu, akasogea, akaniuliza “vipi bado una hasira?” Nikamtazama, nikacheka. Tukacheka.

Ngwair aliposhuka jukwaani, nilikuwa mtiifu mno kwa kazi yake. Sikufungua kinywa kumlaumu. Hata tulipokutana siku nyingine baada ya hapo sikufungua mdomo kumlaumu. Alininyamazisha.

Aliniudhi kwa nidhamu yake ya kutozingatia ratiba, lakini kazi yake ilinijaza tabasamu. Siku haikuharibika. Ilikuwa tamu sana. Nilirudi nyumbani nikitabasamu. Kesho yake niliingia ofisini nikitabasamu.

Ni miaka nane tangu tukio hilo. Jana ilitimia miaka saba tangu Ngwair aliporejea kwa Mungu. Siku nyingine nitaeleza lingine kuhusu kumbukumbu yangu na Ngwair. Kwa leo ni hii.

Endelea kupumzika kwa amani The Freestyle King. We miss you, Albert.


Credit: Luqman Maloto

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom