Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho (Taaluma na Tafiti), Profesa Jo, Do Hyun amewaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa, chuo kiko tayari kuanza masomo na kwamba sasa kiko katika harakati za kusajili wanafunzi wenye sifa zinazotakiwa na kuongeza kuwa, kwa kuanzia, chuo hicho kitachukua wanafunzi 120, ambapo kila moja ya kozi hizo mbili itachukua wanafunzi 60.
Amesema chuo hakitasajili wanafunzi kwa misingi ya dini zao, bali sifa za kitaaluma na kuongeza kwa mwaka wa masomo unaoanza, chuo kitatoa ufadhili kwa wanafunzi 53 na watarajiwa wa ufadhili huo watatakiwa kuwa na vigezo vilivyowekwa. Ufadhili huo umewekwa katika makundi ya aina mbalimbali.
Akielezea zaidi, amesema wanafunzi katika chuo hicho watapata fursa ya mafunzo kwa vitendo kwa muda wa miezi sita nje ya nchi na kwamba hiyo itasaidia kuwajengea mtazamo mpya wa dunia, kujifunza zaidi kivitendo pamoja na kujenga mtandao kwa faida yao na nchi kwa ujumla.