Nilifika katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi, Dar es Salaam, nikapata nafasi ya kuzungumza na Wanawake wajasiriamali wanaofanya kazi katika eneo hilo.
Wanawake hawa, wanaojishughulisha kama mamalishe, Wabeba mizigo, makarani na wauzaji wa vinywaji, walinishirikisha changamoto nyingi zinazohatarisha maisha yao binafsi na biashara zao.
Katika mazungumzo yangu nao, wengi walielezea jinsi unyanyasaji wa kijinsia na rushwa ya ngono zilivyo changamoto kubwa katika shughuli zao za kila siku.
Mwanamke mmoja, ambaye ni mamalishe, alinieleza mara kwa mara hulazimishwa kukubali matakwa ya baadhi ya wasimamizi wa kituo au kupoteza nafasi yake ya kufanya biashara.
Namnukuu “Nilijaribu kupinga mara ya kwanza, lakini nikakosa kibali cha kuendesha biashara yangu kwa siku kadhaa," alieleza kwa uchungu.
Hali hii inaathiri sana maendeleo yao ya kiuchumi. Biashara ambazo tayari ni changamoto kwa sababu ya ushindani mkubwa zinakumbana na vikwazo zaidi kutokana na vitendo hivyo vya unyanyasaji.
Wanawake wengi wanasema badala ya kuzingatia kuboresha huduma zao, hulazimika kutumia muda mwingi kufikiria jinsi ya kukabiliana na mazingira haya yasiyo rafiki. Niliweza kushuhudia mazingira magumu wanayokutana nayo.
Baadhi ya Mamalishe walieleza kuwa wanapokataa kushiriki vitendo vya rushwa ya ngono, wanatishiwa kufukuzwa au kunyimwa fursa ya kuuza katika maeneo yenye wateja wengi.
"Hali hii inatufanya kuishi kwa hofu kila siku," aliongeza mmoja wao.
Wengine walieleza wamefikiria kuacha biashara zao, lakini kutokana na ukosefu wa fursa mbadala za ajira, wanalazimika kuvumilia hali hizi mbaya.
Nilipozungumza na viongozi wa kituo, walikiri kuwepo kwa changamoto hizo lakini walidai wanashughulikia suala hilo. Hata hivyo, hakuna hatua thabiti zilizotajwa, na hali inaonekana kuendelea kuzorota.
Wajibu wa viongozi katika kuhakikisha mazingira salama ya kazi hauwezi kupuuzwa. Wanawake wanasema kuwa mara nyingi viongozi hawa hutetea vitendo vya unyanyasaji kwa kusema kuwa ni sehemu ya changamoto za maisha, hali inayovunja moyo.
Wajasiriamali hawa hawakabiliwi tu na changamoto za unyanyasaji wa kijinsia bali pia dharau na unyanyapaa. Baadhi ya abiria na wafanyakazi wa mabasi huchukulia kazi zao kama zisizo na thamani, hali inayowafanya wapoteze ujasiri na ari ya kuendelea na biashara zao.
Hili ni tatizo la kisaikolojia ambalo linawaathiri vibaya wanawake hawa.
Upande wa mamlaka na mashirika ya kijamii, juhudi bado ni za kiwango cha chini. Wanawake hawa wanahitaji msaada wa dhati ili kuondokana na hali hii ya unyanyasaji na kuwezeshwa kufanya biashara zao kwa heshima na usalama.
Mashirika yanayojihusisha na masuala ya kijinsia yanaweza kushirikiana na viongozi wa kituo kutoa elimu ya haki za binadamu na kusisitiza umuhimu wa uwajibikaji katika maeneo ya kazi.
Kwa mujibu wa maoni niliyokusanya, wanawake wa Kituo cha Mabasi cha Magufuli wanahitaji zaidi ya ahadi.
Wanahitaji hatua za haraka, kama kuanzishwa kwa mifumo ya kisheria inayolinda haki zao na kuhakikisha uwajibikaji wa wale wanaohusika na vitendo hivi vya unyanyasaji.
Mfumo wa wazi wa kupokea na kushughulikia malalamiko pia ni muhimu, kwani wengi wa waathiriwa hawajui wapi pa kupeleka shida zao.
Ni wazi kwamba hali hii si tatizo la wanawake wa Magufuli pekee, bali ni sehemu ya changamoto kubwa inayowakabili wanawake wajasiriamali katika maeneo mengi.
Hivyo, ni muhimu kuanzisha mjadala wa kitaifa kuhusu usawa wa kijinsia na mazingira salama ya kazi kwa kila mmoja.
Kufanikisha hili, mamlaka za serikali zinapaswa kushirikiana na mashirika binafsi na ya kijamii, kuhakikisha kuwa sheria zinatungwa na kutekelezwa kwa manufaa ya wote.
Natoa wito kwa mamlaka husika, mashirika ya kijamii, na wadau wengine kuungana kuhakikisha kuwa wanawake hawa wanapata fursa sawa za kufanya kazi kwa heshima na uhuru.
Ni wakati wa kuacha kufumbia macho tatizo hili na kuchukua hatua stahiki kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo. Wanawake hawa ni kiini cha uchumi wa eneo hili, na ustawi wao ni faida kwa jamii nzima.
Ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa wanawake hawa wanapata mazingira bora ya kazi yanayolinda heshima yao, biashara zao, na utu wao.