SoC01 Uongozi Bora ni Chachu ya Maendeleo

SoC01 Uongozi Bora ni Chachu ya Maendeleo

Stories of Change - 2021 Competition

Alfredwanka

New Member
Joined
Jul 16, 2021
Posts
2
Reaction score
2
Uongozi ni uhusiano uliopo baina ya pande mbili; upande unaoongoza na upande unaoongozwa (Prof. Rev. Fr. Magesa, 2003). Uhusiano huo unajengwa na imani ya wanaoongozwa kwa kiongozi wao. Wanaoongozwa huwa na imani kwa kiongozi wao kwa sababu ya kutaka kufikia lengo fulani. Hivyo, Uongozi ni dhamana anayopewa mtu na kundi la watu ili kuwafikisha katika hatua au malengo fulani ya pamoja. Matukio yanayotukia ulimwenguni ni kwa sababu ya uongozi. Endapo uongozi utakuwa ni wenye kufuata misingi bora, basi matukio yatakuwa mema na kinyume chake ni sahihi.

Hakuna jamii au jumuiya yoyote ya binadamu isiyokuwa na uongozi. Hivyo, ili kuwepo na uongozi bora, kiongozi hana budi kuzingatia na kuyaishi mambo yafuatayo:

Kujua au kutambua mazingira ya watu anaowaongoza; hii ni kwa sababu, kiongozi akiyaelewa vizuri mazingira itamrahisishia kwa urahisi ni eneo lipi lina uhitaji wa huduma fulani ama upungufu wa jambo fulani na kuona namna ya kuyatatua ama kutafutia ufumbuzi. Vile vile itasaidia kuelewa rasilimali zinazopatikana katika maeneo mbalimbali ili kuona namna gani zitumike kwa ajili ya kuleta tija katika maeneo hayo na taifa kwa ujumla.

Kuwasiliana na watu wake; hii ni kwa sababu, kiongozi akibeza mawasiliano ama kuweka mipaka kati yake na kundi analoliongoza, itamuwia ugumu katika kuzitambua kero, maoni, ushauri na mapendekezo kutoka kwa watu na badala yake hupokea ushauri kutoka katika kundi dogo la watu miongoni mwa watawala ambao wakati mwingine huweza kupindisha kile ambacho kingesemwa moja kwa moja na wanaoongozwa, aidha kwa kulinda nyadhifa zao ama kwa maslahi yao binafsi.

Kubuni mambo mapya na kuyatekeleza; Kiongozi anapaswa kuwa mbunifu katika kuliongoza kundi. Kwa mfano kiongozi anapaswa kubuni sera ambazo pindi zikitekelezwa zitatoa matokeo chanya yenye maslahi kwa taifa. Pia kubuni itikadi au mbinu bora ambazo zikitekelezwa kwa usahihi kama litakavyo kusudio la ubunifu huo, basi jamii inayoongozwa ipige hatua kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

Kuwa kiongozi muwezeshaji na si kiongozi anayedai utii na kuamrisha; hii ni kwa sababu kiongozi ni mtu anayebeba dhamana kubwa katika safari ya kufikia lengo fulani. Hivyo kiongozi anapaswa kurahisisha au kutengeneza mazingira yatakayorahisisha utendaji kazi katika kulifikia lengo kusudiwa kwa kushirikiana na watendaji au wasaidizi wake na kukaa kitako ukiamrisha ama ukihitaji utii kutoka kwa watendaji au wakati mwingine kuogopwa na kundi unaloliongoza.

Kutochukiwa au kudharauliwa; hii ni kwa sababu, uongozi ni dhamana ambayo waongozwaji humbebesha kiongozi kutokana na imani yao kwake. Hivyo, kiongozi hapaswi kukengeuka au kulemaa kwa kwenda kinyume na matarajio au malengo makuu ya kundi analoliongoza. Kwa kufanya hivyo, imani ya waongozwaji dhidi yake itapungua hivyo kuchukiwa au kudharaurika. Hali hii huweza kuleta shida ama ukakasi katika utawala.

Kunena na kutenda; hii ni kwa sababu, maneno peke yake bila matendo, hayana nguvu. Kiongozi anapaswa kutekeleza kwa vitendo jambo alilolizungumza au kuahidi ili kuilinda imani ya anaowaongoza dhidi yake.

Kuleta umoja kati ya makundi mbalimbali katika jamii anayoiongoza; hii ni kwa sababu, katika kila jamii, watu huishi katika makundi madogo madogo ambayo huwa na itikadi na misimamo yao tofauti tofauti. Hivyo, ili kulifikia lengo kuu majumui, kiongozi anao wajibu wa kuyaunganisha makundi hayo ili kuenenda katika hali itakayo saidia kulifikia lengo majumui pasipo mitawanyiko. Kwa mfano, makundi ya wazee na vijana, wanawake na wanaume, vyama mbalimbali, maskini na matajiri n.k.

Baada ya kujadili masuala ambayo utekelezaji wake ukizingatiwa huuweza kuufanya uongozi kuwa bora, sasa tujadili maswala ambayo huweza kumbadili kiongozi kuwa kiongozi bora:

Kiongozi bora anahitaji mafunzo endelevu; hii ni kwa sababu, jamii hupita katika mabadiliko siku hadi siku, hivyo mifumo mbalimbali ya kimaisha na kiutawala hubadilika pia. Hivyo, kiongozi anapaswa kujifunza ili kuja na mbinu mpya zz kiutawala zitakazo muwezesha kuendana na mabadiliko hayo.

Kiongozi bora anahitaji mahusiano na mashauriano kutoka kwa viongozi wengine; hii ni kwa sababu, kiongozi yeyote huwa na watu wa kushirikiana naye katika kuliendesha gurudumu la utawala. Hivyo kundi hilo la viongozi waandamizi wanayo nafasi kubwa katika kumsaidia kiongozi mkuu kulifikia au kutolifikia lengo kuu majumui. Kutokana na uwezekano huo, kiongozi mkuu anapaswa kuwa na mahusiano mazuri pamoja na mashauriano kutoka kwa viongozi wengine ili kulifikia lengo hilo na si kuwa na maamuzi binafsi katika utawala kwani matokeo huwa ya majumui na si binafsi tena.

Kiongozi bora anahitaji tafakari binafsi; hii ni kwa sababu, kiongozi bora hutoa nafasi ya kushauriana kupokea maoni na ushauri kutoka kwa wasaidizi au kundi analoliongoza. Hivyo, kiongozi anapaswa kuwa na muda wa kutosha ili kutafakari na kuchambua kwa kina taarifa za mapokeo kabla ya kutoa tamko au kufanya maamuzi. Hii ni kwa sababu katika kundi la watu wengi hila, fitina, chuki pamoja na wivu ni vitu visivyoepukika, hivyo bila tafakuri pevu kiongozi anaweza kufanyamaamuzi yenye kuumiza upande mmoja na kupendelea upande mwingine.

Kiongozi bora anapaswa kuwa mfano wa kuigwa; hapa kiongozi anapaswa kuisimamia imani waliyonayo waongozwaji dhidi yake kwa kutimiza wajibu wake katika namna inayofaa na kukubalika. Halii hii iende sambamba kwa vitendo na maneno huku vitendo visivyo rafiki katika kulifikia lengo vikiepukwa. Kwa kufanya hivyo, viongozi wasaidizi pamoja na umma unaoongozwa utahamasika kujibidisha kwa bidii kutokana na ari kubwa wanayoipata kutoka kwa kiongozi mkuu.

Kiongozi bora awe na ushawishi; hii ni kutokana uwajibikaji unaotakiwa ambao unadhihirishwa na kiongozi mkuu katika nafasi yake. Iwapo utendaji kazi ama uwajibikaji unaridhisha basi utatumika kama nyenzo muhimu ya kuushawishi umma unaoongozwa kuwajibika katika nafasi yake. Lakini mambo huwa kinyume kama kiongozi hatawajibika katika nafasi yake hivyo kupoteza nguvu ya ushawishi katika jamii.

Hivyo tunaweza kusema kuwa, kuwa kiongozi bora au kutokuwa kiongozi bora ni matokeo ya mtu binafsi kulingana na mbinu, itikadi pamoja na misimamo aliyojiwekea mwenyewe. Kwani, kiongozi bora ni yule anayeambatana na madaraka (Marko 1: 21-28), madaraka halisi na si uwezo wa kutumia nguvu bali ushawishi. Katika hali hii nuru ya maendeleo huonekana katika kundi la waongozwa. Lakini kiongozi asiye bora yeye hutumia madaraka ambayo si halisi kwa hutawaliwa na matumizi ya nguvu na si ushawishi. Katika hali hii misingi ya maendeleo katika jamii, hubakia katika giza.


Marejeleo.

Biblia Takatifuu

Magesa, L & Nthamburi, Z. Democracy and reconciliation: a challenge for African Christianity. Nairobi: 2003.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom