JE, NI KWELI YESU ALIKUFA JUU YA MSALABA?
Ikiwa kuna mambo ambayo yamekuwa yakileta utata katika ulimwengu wa Dini mbalimbali ni pamoja na kuhusiana na kifo cha Yesu Kristo juu ya msalaba ,inawezekana hata wewe ni miongoni mwa watu walio wahi kusikia habari hizi katika Midahalo ya Dini, sehemu mbalimbali au tumewahi kuwasikia baadhi ya Wahadhili wa Dini wakijadili juu ya suala hili, hata inawezekana wewe ndugu yangu unayesoma somo hili ni miongoni mwa watu ambao hawaamini suala la kifo cha Nabii Issa juu ya msalaba . Bila shaka mwenyezi Mungu ni mwingi wa Rehema kwa waja wake na hivyo yeye atatueleza kupitia vitabu, upi ni ukweli juu ya mada hii, Maana vitabu vinasema.
ASH-SHUURA 42:10 Na mkihitilafiana katika jambo lolote( rejeeni kitabu cha mwenyezi Mungu na hadithi za mtume ….).
YUNUS 10:94 Na kama unayo shaka juu ya haya tuliyokuteremshia, basi waulize wale wasomao vitabu kabla yako(Mayahudi na Manasara wale waliosilimu).
AALI-ALAA 87:18,19 Hakika haya (mnayoambiwa humu katika Qurani ) yamo katika vitabu vilivyotangulia, Vitabu vya Ibrahimu na Musa (na wengineo)
Mtume anaambiwa ikiwa ana shaka juu ya jambo lolote ndani ya Qurani Tukufu, basi awaulize wasomao vitabu kabla yake, hawa si wengine bali ni Mayahudi na Wakristo(manasara). Kwa hiyo ikiwa kuna utata wa mada yoyote ndani ya Qurani inabidi turejee kwenye Biblia Takatifu. Na miongoni mwa mashaka kwa ndugu zangu Waislamu ni pamoja na mada inayohusu kifo cha Nabii Issa.
Hivyo basi, mada hii itachunguzwa kupitia vitabu viwili yaani QURANI TUKUFU na BIBLIA TAKATUFU, tutachunguza ukweli ni upi kuhusiana na kifo cha Yesu?: Mambo tutakayoyachambua ni kama ifuatavyo:
1. Je, manabii wa kale walitabiri kuhusu kifo cha Yesu?
2. Je Yesu mwenyewe alitabiri kuhusu kifo chake?
3. Je, Quran Tukufu inasemaje kuhusu kifo cha Yesu?
4. Chimbuko la kupinga kufa na kufufuka kwa Yesu limetoka wapi?
Je, manabii wa kale walitabiri kifo cha Yesu?
Luka 24:44 Kisha [Yesu] akawaambia, hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na Manabii, na Zaburi.
Kwa mujibu wa Biblia Takatifu, baada ya Yesu kufufuka aliwatokea baadhi ya wafuasi wake, na ndipo anawaambia kwamba habari za yeye kufa na kufufuka zimeandikwa katika Torati ya Musa, Manabii na katika Zaburi ya nabii Daudi.
Je ni kweli Musa,na manabii wengine na Zaburi(Daudi) walitabiri juu ya kifo cha Yesu?
1. Torati ya Nabii Musa:
Hesabu 21:8 Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka wa
shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa , atazamapo ataishi.
Utabiri huu ulikuja kuthibitishwa na Yesu mwenyewe katika
Yohana 3: 14 anasema Na kama vile Musa alivyomwinua Yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa ili kila mtu amwaminiye awe na uzima wa milele katika yeye.
Kwa hiyo kitendo cha Nabii Musa kumuinua Yule nyoka katika mti jangwani, kitendo kile
kilikuwa kinaashiria kuinuliwa kwa Bwana Yesu juu ya mti wa msalaba.
2. Isaya:
Yeye anatabiri pia kifo cha Yesu katika Isaya 53:9 inasema:Wakamfanyia pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.
Nabii Isaya anatabiri kwamba Yesu atasurubiwa na wabaya, Hili lilitimia baada ya Yesu kusurubiwa katikati ya waharifu wawili, Biblia Inasema:
Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto.Luka 23:33
3. Nabii Daudi:
Katika kifo cha Yesu msalabani Daudi alitabiri kilio cha mwisho cha Yesu akiwa juu ya masalaba; Zaburi 22:1 Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?
Kauli hii ilikuja kutimizwa na Yesu katika Mathayo 27:46 . “’Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha”’
4. Nabii Yona:
Kitendo cha nabii Yona kuwa ndani ya tumbo la nyangumi kwa siku tatu, ilikuwa ni ishara ya kifo cha Yesu kukaa siku tatu ndani ya kaburi,
Mathayo 12:40 Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi.
JE YESU ALITABIRI KUHUSU KIFO CHAKE?
Mathayo 20:17-18 Hata Yesu alipokuwa akipanda kwenda Yerusaremu, aliwachukuwa wale wanafunzi kumi na wawili faraghani; na njiani akawaambia, Anglieni, tunapanda kwenda Yerusaremu; na mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi; nao watamhukumu afe; kisha watampeleka kwa mataifa wapate kumdhihaki, na kumpiga mijeredi, na kumsulibisha; na siku ya tatu atafufuka. Pia soma Luka 9:22, 18:32-33
JE QURANI TUKUFU INASEMAJE KUHUSU KIFO CHA YESU?
Sema: walikufikieni mitume kabla yangu kwa hoja zilizo wazi na kwa haya mnayoyasema. Basi mbona mliwaua kama mlikuwa wakweli? AALI IMLAN 3:183
Quran inasema Mitume waliokuwa na HOJA zilizo wazi WALIUAWA, na miongoni mwa mitume waliokuwa na HOJA zilizo wazi ni Pamoja na Issa
Na tukampa Isa, mwana wa Mariamu, HOJA waziwazi, na kumtia nguvu kwa Roho Mtakatifu. AL BAQARAH 2:87
Bila shaka Isa naye alikufa maana alikuwa na HOJA zilizo waziwazi.
MARYAM 19:33 “Na amani iko juu yangu siku niliyozaliwa na siku nitakayokufa na siku nitakayofufuliwa kuwa hai” Aya hii ipo wazi kabisa Yesu mwenyewe ndiye anasema ATAKUFA na ATAFUFULIWA;
AAL IMRAN 3:45, inasema
“Na (Kumbukeni) Mwenyezi Mungu aliposema: “Ewe Isa! Mimi nitakutimizia muda wako wa kuishi(hawatakuua hao maadui). Na Nitakuleta kwangu, na Nitakutakasa na wale waliokufuru,(hawataweza kukudhuru) na Nitawaweka wale waliokufuata, juu ya wale waliokufuru, mpaka siku ya Kiama.
Ayah hii haisemi Yesu hata kufa, hapana!!
bali inasema Maadui zake waliokuwa wakimuwinda ndio hawata weza KUMUUA, . Lakini pia Allah anasema NITAKUTIMIZIA MUDA WAKO WA KUISHI akimaanisha atakufa maana kutimiza muda wa kuishi ni KUFA. Sasa maadui wa Yesu walikuwa ni Mayahudi na sasa hebu tuone mayahudi walimuua Yesu au walishindwa? Mayahudi walipoambiwa wamuue Yesu walisemaje.?
Yohana 18:31-32
Basi Pilato akawaambia, Haya! Mtwaeni ninyi, mkamhukumu kwa ile torati yenu! Wayahudi wakamwambia, Sisi hatuna ruhusa ya kuua mtu.
Ili litimie lile neno lake Yesu alilolisema, akionyesha ni mauti gani atakayokufa.
Wayahudi walipoambiwa suala la kumuua Yesu walikataa kwamba wao hawana ruksa ya kuua, na hivyo Wayahudi kama maadui wa Yesu hawakumuua Yesu., wala hawakumsurubisha, Bali walio msurubisha Yesu ni Askari wa Kirumi, lakini Wayahudi wao walimsaliti Yesu kwa Warumi.
Yohana 19:23-24 inasema:
Nao askari walipomsulibisha Yesu, waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa kila askari fungu lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa imefumwa yote pia tangu juu.
Basi wakaambiana, Tusiipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani. Ili litimie andiko lile linenalo, Waligawanya nguo zangu, Na vazi langu wakalipigia kura. Basi ndivyo walivyofanya wale askari
Na wakati Yesu yupo msalabani ilibidi watu wote walioangikwa msalabani wauawe kwa kuvunjwa miguu maana ilikuwa ni jioni na haikuwa ruksa kwa Wayahudi miili ya watu ikae msalabani siku ya Sabato, na hivyo Askari wa Kirumi ilibidi wafanye hivyo, lakini walipofika kwa Yesu hawakumuua kwa kumvunja miguu maana yeye alikufa mapema.
Yohana 19:32-34
Basi askari wakaenda, wakamvunja miguu wa kwanza, na wa pili, aliyesulibiwa pamoja naye.
Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu;
lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji.
Mayahudi ni kweli walifanya jitihada za kumwua Yesu kwa siri, lakini ilishindikana kama ambavyo Qurani tukufu inasema kwamba Maadui zake hawatamuua wala kumsurubu. Kwa hiyo AAL IMRAN 3:45 haikatai kwamba Yesu hatakufa msalabani, bali inakataa kwamba maadui zake Yesu ambao ni Mayahudi ndio hawawezi kumsulubu wala kumuua. Walichokifanya Mayahudi ni kumsaliti Yesu kwa Warumi, maana kwa kipindi hicho Wayahudi walikuwa chini ya utawala wa Kirumi.
Na Yesu mwenyewe anasema hivi juu ya kifo chake.
Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungajimwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.
Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena. Yohana 10:11,17
AN NISAA 4:158“ Na kwa(ajili ya) kusema kwao: “Sisi tumememuua Masihi Isa, mwana wa Maryamu Mtume wa Mungu,” hali hawakumuua wala hawakumsulubu, bali walibabaishiwa(mtu mwengine wakadhani Nabii Isa…..
Baadhi ya watu hutumia aya hii kudai kwamba aliyekufa msalabani sio Isa, bali ni mtu mwingine. Ukweli ni kwamba kauli hii sio ya Allah , maana inasema “kwa kusema kwao” sio Allah amesema, Bali Wanadamu ndio walisema kwamba walibabaishiwa mtu mwingine. Kauli hii ni Indirect speech (Allah ananukuu kauli ya wanadamu jinsi walivyo sema na wala sio yeye katoa hiyo kauli) kauli hii pia ina fanana na kauli ya Mungu katika Biblia.
Malaki 3:14 Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za Bwana wa majeshi?
Vile vile hapa Mungu ananukuu kauli ya wanadamu, na sio yeye kasema kumtumikia Mungu hakuna faida, bali wanadamu ndio waliotoa hiyo kauli.
Kauli ya Allah ni kwamba Isa atakufa.
CHIMBUKO LA KUPINGA KUFA NA KUFUFUKA KWA YESU:
Mwanzilishi wa kupinga kifo cha Yesu msalabani ni shetani, lakini akitumia wanadamu wa kawaida. Mfano siku moja Yesu alikuwa akiwaambia wanafunzi wake kwamba atakufa, lakini Petro akaanza kupinga kwamba Yesu hawezi kufa, Yesu alipomgeukia Petro alimwambia hivi katika
Mathayo 16:23-24…, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.
Kwa hiyo suala la kupinga kwamba Yesu hakufa msalabani ni kwenda kinyume na mpango wa Mungu, lakini pia ni kazi ya Shetani kupinga kwamba Yesu hakufa .
Baada ya Yesu kuzikwa Mafarisayo walimwendea Pilato na kumwambi
“’Wakasema, Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa akali hai, Baada ya siku tatu nitafufuka.
64 Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza.
65 Pilato akawaambia, Mna askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo.
66 Wakaenda, wakalilinda kaburi salama, kwa kulitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi.” Mathayo 27:63-66
Lakini jitihada zao hazikuzaa matunda maana ilipofika siku ya tatu kama ilivyotabiriwa Yesu alifufuka katika wafu, Mathayo 28:1-10. Sasa baada ya kuona wameshindwa kulinda kaburi na Yesu kafufuka wakaweka mikakati ya kueneza uwongo. Mathayo 28:12-15 inasema: Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi, wakisema, Semeni ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala.Na neno hili likisikilikana kwa liwali, sisi tutasema naye, nanyi tutawaondolea wasiwasi. Basi wakazitwaa zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Na neno hilo likaenea kati ya Wayahudi hadi leo”
Askari hawa baada ya kupewa fedha kazi yao kubwa ilikuwa ni kueneza uwongo kila mahali kwamba Yesu hakufufuka, na hili ndilo chimbuko la kupinga kwamba Yesu hakufa wala hakufufuka.
YUNUS 10:94 Na kama unayo shaka juu ya haya tuliyokuteremshia, basi waulize wale wasomao vitabu kabla yako.
………………………………………………………………………