SoC02 Urasimu mamboleo

Stories of Change - 2022 Competition

Maestro_06

Member
Joined
Sep 9, 2021
Posts
11
Reaction score
1
Maendeleo ya kiteknolojia yametoa msaada mkubwa sana katika jamii ya sasa. Teknolojia haijarahisisha kazi tu bali imeboresha utunzaji wa takwimu na kuondoa mlolongo mrefu na wenye kuchosha katika kutoa huduma. Mtu anaweza kukamilisha maombi ya udahili wa chuo kiganjani mwake bila kupita katika ofisi nyingi na kutumia nakala ngumu ambazo zinaweza kupotezwa kirahisi. Uchakataji mzuri wa taarifa na utenganishaji wa taarifa umeweza kufanywa kwa urahisi na muda mfupi. Lakini je, matumizi haya ya teknolojia yameondoa urasimu kabisa?

Mifumo hii ilitengenezwa ili kupunguza urasimu na kuondoa kabisa myanya ya rushwa na kwa asilimia kubwa imefanikiwa. Pamoja na mafanikio hayo makubwa lakini mifumo hii imeleta urasimu mpya, kandamizi na uliofumbiwa macho katika kivuli cha ‘usasa’. Changamoto nyingi zimekuwa zikiwapata watumiaji wa mifumo hii.

Mifumo mingi inayotumiwa na serikali Pamoja na baadhi ya taasisi binafsi imekuwa ikianzishwa bila kukaguliwa na kujaribiwa vizuri. Mifumo mingi imekuwa ikishindwa kufanya majukumu yake ipasavyo na kusababisha usumbufu usio wa lazima kwa watumiaji. Mifumo ya malipo kuchelewesha malipo, mifumo ya utambuzi kushindwa kutambua, mifumo ya kutunza taarifa kupoteza taarifa muhimu na mifumo ya maombi kukwamakwama yamekuwa malalamiko ya kawaida miongoni mwa watumizi wa mifumo ya kidijitali.

Pamoja na hayo, usumbufu wa kimtandao pia umekua hoja kubwa kwa watumiaji wa mifumo hii. Hatua chache ambazo zingehitaji muda mfupi kukamilika zimekuwa zikitumia muda mrefu na kusababisha kero miongoni mwa watumiaji.

Urasimu huu mamboleo umekuwa ukipewa majina mengi kama kufeli kwa mfumo, kuzidiwa kwa mfumo na kadhalika. Cha kushangaza ni kwamba endapo utatembelea wahusika na kuwaona ana kwa ana shida yako inaweza kutatuliwa. Hali hii imekuwa ikiibua maswali mengi sana. Je, wataalamu hawa wanakosea makusudi ili wapate kujitengenezea masega ya kulamba asali, au je, wataalamu wanaopewa kazi hizi hawana vigezo stahiki, au labda tumekurupuka kuvamia mifumo ambayo bado hatujajiandaa kuitumia?

Hoja hizi zimekuwa zikuzua mitazamo mbalimbali miongoni mwa watu wa kawaida. Wengine wameanza kuamini kuwa hata katika mifumo hii ya kisasa bado kuna wizi. Wengine hudai ya kuwa katika mifumo hii bado kuna namna ya kukosa usiri wa taarifa binafsi na muhimu.

Matatizo haya yamekuwa yakiwaongezea gharama zisizo za muhimu watumiaji. Makosa mengi yanayojitokeza katika mifumo hii hayana dhamana. Taarifa nyingi muhimu hupotea, pesa, haki ya watu wote kuhudumiwa kwa usawa na hata muda wa watumiaji hupotezwa. Cha kusikitisha bado swala hili limefumbiwa macho.

Hata dalili ndogo sana inaweza ashiria ugonjwa mkubwa sana, tena unaoweza kugharimu maisha. Swala hili lina mwarubaini wake. Yapo mambo mengi ambaya yanaweze kufanywa na wahusika ili kuweza kutatua matatizo haya.

Mifumo yote ambayo inatengenezwa yapaswa kufanyiwa majaribio ya kutosha kabla ya kufikishwa kwa watumiaji. Hii itapunguza hasara na usumbufu usiokuwa wa lazima kwa watumiaji na wamiliki. Kukaguliwa kwa mifumo hii kutasaidia kupunguza makandokando yoyote ambayo yalijitokeza katika utengenezwaji wa mifumo hii.

Wataalamu wanaotengeneza mifumo hii wanatakiwa kuwa na weledi na utaalamu wa kutosha ili kupunguza makosa ya kizembe. Pale ambapo watatumika wataalamu wabobezi usalama wa taarifa na ufanisi wa mifumo utakuwa wa kiwango cha juu.

Watunga sera wanatakiwa kutunga sheria inayolazimu mifumo yote ya kidijitali yenye kusudi la kutoa huduma iwe ya umma au ya binafsi kuhakikiwa. Hili liambatane na adhabu kali kwa wahusika au taasisi yoyote ambayo kwa makusudi kabisa inatumia mifumo ambayo haikuhakikiwa vizuri.

Watumiaji waliolengwa kutumia mifumo hii ya kidijitali wanatakiwa kupewa elimu ya kutosha juu ya mifumo hii ya kisasa ili kuwasaidia kuitumia mifumo hii kwa ufanisi mkubwa na kwa weledi. Hili pia litapunguza makosa ya kawaida yanayofanywa na watumiaji. Jambo hili ni la muhimu sana kwa sababu, baadhi ya mifumo hii inawalenga watumiaji wenye uelewa mdogo juu ya maswala ya tehama. Kuanzisha mfumo bila kuelewesha watumiaji kutasababisha mfumo kutokufukia malengo yaliyo kusudiwa.

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa teknolojia wanapaswa kuhakikisha kuwa watu wote wanaweza kupata huduma za kimtandao kiurahisi. Mifumo hii hailengi tu watu wenye kiwango cha juu cha kipato bali hata wale walio na kiwango cha kati na cha chini kabisa. Kama huduma ya mtandao inaweza kupatikana kwa bei nafuu zaidi itaweza kusaidia utendaji mzuri wa mifumo hii na kupunguza misururu mirefu ya watu maofisini wanaohitaji huduma. Pia itawaokoa wengi ,watumishi Pamoja na wananchi katika mtego wa rushwa ya namna yoyote.

Wasimamizi wa mifumo hii wanatakiwa kuwekwa kwenye uangalizi ili kuziba namna yoyote ya upendeleo, rushwa na wizi wa taarifa ili kuweza kuilinda mifumo hii.

Pia mifumo hii iwe na dhamana kwa ajili ya watumiaji wake. Hii itasaidia kufidia pale ambapo matatizo ya kimfumo yasiyohusiana kabisa na mtumiaji yataposababisha upotevu wa taarifa au hata pesa. Dhamana hii pia itawapa watu uhuru na Imani katika kutumia mifumo hii ya kiteknolojia. Serikali, wadau wa teknolojia pamoja na mashirika ya bima wanaweza kushirikiana ili kuweza kuhakikisha swala hili linawekwa katika utekelezaji.

Penye nia pana njia. Kama jamii kwa ujumla itaweza kusimama na kupaza sauti kulizungumzia swala hili, wahusika watafikiwa na ujumbe huu na marekebisho muhimu yatafanyika ili kutuepusha na urasimu huu mamboleo. Ni Fahari ilioje kumuona mtu aliopo Karagwe Bukoba kufanya malipo ya ushuru wa forodha wa bandari ya Dar es salaam akiwa ametulia nyumbani kwake?, au ni habari gani kwa muhitimu wa chuo aliopo Misungwi, Mwanza anapofanikiwa kutuma maombi ya ajira Uyole, Mbeya kwa wakati bila kupitia mikononi mwa madalali matapeli au kusafiri na barua zaidi ya kilomita 900?. Swala hili likivaliwa njuga urasimu huu mpya unaweza kutokomezwa kabisa. Tukiamua tunaweza.
 
Upvote 1
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…