SoC04 Usalama wa nchi na Uboreshaji wa ukusanyaji mapato Sekta ya Utalii Kupitia Mfumo wa Kidigitali

SoC04 Usalama wa nchi na Uboreshaji wa ukusanyaji mapato Sekta ya Utalii Kupitia Mfumo wa Kidigitali

Tanzania Tuitakayo competition threads

flowbytes

New Member
Joined
Jun 5, 2024
Posts
1
Reaction score
0

Utangulizi

Sekta ya utalii nchini Tanzania ina changia pato la taifa kwa asilimia kumi na saba (17%) na mapato ya fedha za kigeni kwa asilimia hamsini na tano (55%). Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 - 2025/26 (Juni 2021 uk. 103)

Kwa takwimu hizi, sekta ya utalii inaendelea kuwa muhimu sana katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Hata hivyo, sekta hii inakabiliwa na changamoto mbalimbali. Katika andiko hili, nitajadili changamoto kuu mbili: Usalama wa nchi na Upotevu wa mapato.


Hali ilivyo sasa


Kwa sasa, mgeni anapohitaji kufanya utalii nchini, anawasiliana moja kwa moja na kampuni za utalii. Mawasiliano yote haya ya awali hakuna mamlaka za serikali zenye taarifa kamili kuhusu safari ya mgeni huyo. Hii ina maana kuwa mgeni anakwenda wapi, anafanya nini, na anakaa wapi, ni taarifa ambazo zinabaki mikononi mwa kampuni ya utalii. Kampuni hii ya utalii ndio inayotoa taarifa hizo baadae kwa mamlaka nyingine ikiwemo za kiserikali.

Changamoto Zilizopo

  • Usalama wa nchi
Kwa kuwa kampuni za utalii ndizo zinazoshikilia taarifa kamili kuhusu safari ya wageni, utaratibu huu unatoa mwanya wa kuhatarisha usalama wa nchi IKIWA kampuni husika itajishughulisha na vitendo vya uhalifu kama ugaidi, ujangili, wizi wa kuaminiwa n.k kupitia mlango wa utalii. Kwa kuwa hakuna mamlaka ya kiusalama iliyohusika kukagua mawasiliano haya tangu mwanzo, udhibiti wa aina hii ya matukio utakua mgumu na kupelekea kuharibu usalama wa nchi.​
Tukumbuke kua, jeshi la polisi liliripoti ongezeko la matukio ya uhalifu yaliyofanywa na raia wa kigeni kutoka matukio 5 mwaka 2019 hadi 17 mwaka 2020. Takwimu za hali ya uhalifu Januari - Disemba 2020 ( uk. 32).​
Ongezeko hili liliendana na kuongezeka kwa idadi ya raia wa kigeni nchini. Hivyo, kuna haja ya kuwa na mfumo bora wa usimamizi wa taarifa za wageni ili kuboresha usalama wa nchi.
  • Upotevu wa mapato
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Taifa wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26 unalenga kuongeza idadi ya watalii hadi milioni 5 na mapato ya dola za Marekani bilioni 6 ifikapo mwaka 2025. Mwaka 2023, watalii wa kimataifa waliofika Tanzania walikuwa 1,808,205, na kuingiza dola za Marekani bilioni 3.37. Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 - 2025/26 (Juni 2021 uk. 103)

Kwa takwimu hizi inaonyesha kua umebaki mwaka mmoja tu ili kupima kama malengo yaliyowekwa ya kufikia dola za Marekani bilioni 6 yametimia ikiwa kwa sasa ukusanyaji ni dola za Marekani 3.37 tu.​
Pamoja na changamoto zilizoikumba sekta hii kwenye janga la UVIKO-19, mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) ingeweza kufikia lengo kirahisi ikiwa ingeweza kuwa na taarifa sahihi kuhusu huduma zote za kifedha wanazofanya wageni wakiwa nchini. Mamlaka hii hutegema taarifa hizi kutoka kwa walipa kodi wenyewe, kampuni za utalii. Kampuni hizi zinaweza kutumia fursa hii kukwepa kodi kwa kutokutoa taarifa kamili au sahihi kuhusu huduma na gharama zote ambazo wageni wao watafanya wakiwa nchini.

Suluhisho

Kwa sasa kuna mifumo midogo midogo kama ya TANAPA na Ngorongoro Conservation inayohusika na uratibu wa taarifa za wageni wanaoingia kwenye hifadhi. Ila hii haitoshi. Maana hata mifumo hii miwili haisomani. Ili kuboresha sekta ya utalii na kuhakikisha usalama pamoja na ukusanyaji sahihi wa mapato, napendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa kidigitali utakao kuwa na uwezo wa kuunganisha taarifa zote zinazohusiana na utalii nchini, kuanzia hatua ya mwanzo ya mawasiliano kati ya mgeni na kampuni ya utalii hadi hatua ya mwisho ya safari ya mgeni.

Jinsi mfumo utakavyofanya Kazi​

Muundo wa mfumo
  • Mfumo huu utahitaji mamlaka, taasisi, bodi na kampuni zote zinazohusika na utalii kujiunga. Hapa nazungumzia Mamlaka za ndege (JNIA, KIA), TANAPA, NGORONGORO, TRA, TAWA Mamlaka husika ya usalama wa nchi, Kampuni za utalii n.k.
  • Mfumo utaruhusu kampuni za utalii kuweka huduma zao “Safari Packages” na kuweza kuonekana kwa wageni na kuzinunua. Mfano wa hii ni kama TripAdvisor, SafariBookings

Mchakato wa Kuanza Safari
  • Mgeni akitembelea Portal hii, anapata kila taarifa kuhusu utalii Tanzania. Anaweza kutafuta kampuni anayoitaka na kuanza kufanya nayo majadiliano kuhusu safari. Majadiliano yote huifadhiwa katika mfumo na mamlaka zinaweza kuyapitia na kujiridhisha.

Upatikanaji wa Namba ya Kipekee:
Baada ya kampuni kufikia makubaliano na mgeni, itapokea namba ya kipekee ya mgeni (Unique Tourist ID). Namba hii itakuwa na taarifa zote muhimu za mgeni, na bila namba hii, mgeni hatapokea huduma yoyote ya kitalii nchini. Namba itatambuliwa na mfumo tangu akiwasili katika uwanja wa ndege wa Tanzania.​

Kuanzia hapa sasa taasisi zote husika zitaanza kuona wanachostahili.​
  • Taasisi za kiusalama zinaweza kuona mawasiliano yote yaliyokua yalifanyika. Ikiwa kuna mawasiliano mengine yalifanyika kwa njia nyingine kama barua pepe, kampuni itahitajika kuweka attachment.
  • Mamlaka ya mapato nayo pia itaweza kuona huduma zote za kifedha mgeni huyo atakazofanya akiwa nchini na kuweza kujipatia mapato yake kwa njia ya urahisi.

Faida za Mfumo

Kulinda Usalama wa nchi
  • Mamlaka za usalama zitakuwa na uwezo wa kufuatilia mienendo ya wageni na kujiridhisha kuhusu usalama wa nchi.
  • Ikiwa kuna vitendo vyovyote vya kutiliwa shaka, mamlaka hizi zitaweza kuchukua hatua mapema.

Ukusanyaji wa Mapato
  • Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) itakuwa na uwezo wa kufuatilia huduma zote za kifedha mgeni atakazofanya akiwa nchini bila kutegema taarifa hizi kutoka kwa kampuni husika na kujipatia mapato stahiki.


Hasara Zinazoweza Kutokea


Gharama ya uendeshaji wa mfumo:
  • Uanzishaji wa mfumo huu utahitaji uwekezaji mkubwa wa awali katika teknolojia na mafunzo. Hata hivyo, faida za muda mrefu zitazidi gharama hizi za awali.

Mabadiliko ya Utendaji:
  • Kampuni na taasisi zitahitaji muda kuzoea mfumo mpya, na huenda kutakuwa na upinzani wa awali kutoka kwa baadhi ya wadau.
  • Mafunzo na uhamasishaji vitahitajika ili kuhakikisha mfumo unakubalika na kutumika ipasavyo.

Hitimisho

Kwa ujumla, kuanzishwa kwa mfumo huu kutaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya utalii nchini. Mfumo huu utaimarisha usalama, kuboresha ukusanyaji wa mapato, na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za kitalii. Kwa kuwa mimi ni mtaalam wa mifumo ya kompyuta na nina uzoefu katika sekta ya utalii, nipo tayari kusaidia katika kuandaa na kutekeleza mfumo huu. Tanzania inahitaji mfumo kama huu ili kuhakikisha kwamba sekta ya utalii inachangia ipasavyo katika uchumi wa nchi na inabaki kuwa salama na yenye kuvutia kwa wageni kutoka kote duniani.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom