Ushairi

Mwosha Maiti

New Member
Joined
Oct 11, 2018
Posts
3
Reaction score
1
ZIMWI LA DAR!

Kwanza naanza kwa dua, Yarabi nisimamie,
Moyo nakuinulia, roho wako nivuvie
Hekima busara pia, nazo unikirimie
Pamwe na Watanzania, yao nchi watetee
Zimwi limeteka Dar, limejivika fahari.

Liwalo sasa na liwe, leo nabwaga manyanga
Nimechoka kuwa mwewe, kutwa ubawa kukinga
Kisa naogopa jiwe, mbawa kuzitia janga
Wallahi sina kiwewe, tayari nimejipanga
Zimwi limeteka Dar, limejivika fahari.

Limemeza waandishi, hawana tena habari
Hawatoi matamshi, wameshatiwa kiburi
Hawatumii utashi, walopewa na Kahari
Wanaeneza ucheshi, na wa zimwi uhodari
Zimwi limeteka Dar, limejivika fahari.

Limemeza wasanii, hawana tena sanaa
Isadifuyo jamii, madhila kujinasua
Hawana tena bidii, weledi umepotea
Sheria wanazitii, zimwi linazozitoa
Zimwi limeteka Dar, limejivika fahari.

Limemeza wanadini, hakuna tena nabii
Mwenye huria lisani, asokipofu utii
Anenaye fuadini, pasi kujali uhai
Faraghani hadharani, asiye na jitimai
Zimwi limeteka Dar, limejivika fahari.

Zimwi ‘memeza siasa, siwaoni wapinzani
Wameshageuka kasa, wamerejea mtoni
Ijapo hawajasusa, watamia mateteni
Wasije yote kukosa, nchi kavu na majini.
Zimwi limeteka Dar, limejivika fahari.

Halaiki wanahanya, kwa mambo linayofanya
Uhuru limeuminya, haki limeikusanya
Wazee linawasonya, huku linawatekenya
Matakwa yake kupenya, taifa lake kunyonya
Zimwi limeteka Dar, limejivika fahari.

Zimwi lavunja sheria, hakuna wa kulisema
Damu linajinyonyea, pasi hata na huruma
Tumboni linawatia, hata wasiotuhuma
Ni nani asiyejua, Bongo zima yazizima
Zimwi limeteka Dar, limejivika fahari.

Zimwi watu linateka, wakwasi na makabwela
Umma unatiribuka, likinya yake risala
Hakuna wakupulika, kama pono wanalala
Wamegeuka mateka, si watu nyangarakala
Zimwi limeteka Dar, limejivika fahari.

Zimwi linajulikana, na wasiojulikana
Nao wasojulikana, kwa zimwi wajulikana
Sio baba sio nina, si mzee si kijana
Zimwi halina hiyana, lamtwaa na mnuna
Zimwi limeteka Dar, limejivika fahari.
.
.
~ Eric F. Eric Fortunatus Ndumbaro
Mwenge Catholic University (MWECAU)
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…