Mkutano wa Mawaziri wa Kundi la BRICS umefanyika kuanzia Juni 10 hadi 11 huko Nizhny Novgorod, nchini Russia. Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi alihudhuria mkutano pamoja na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za BRICS na wawakilishi kutoka Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na ASEAN. Pia wawakilishi kutoka Umoja wa Afrika na Umoja wa Nchi za Kiarabu pia walialikwa katika mkutano huo.
Katika wakati huu ambapo nguvu za mrengo wa kulia zinaathiri Bunge la Ulaya na vita kati ya Israel na Palestina vinagawa mitazamo ya dunia, BRICS inaendelea kuwa na umoja na kufanikiwa, na kuvutia ufuatiliaji wa kimataifa kutokana na utulivu wake.
Saudi Arabia, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Iran na Ethiopia zilijiunga rasmi na BRICS mwezi Jamuari mwaka huu, na kuwa alama kubwa ya maendeleo ya mfumo wa BRICS. Upanuzi wa familia ya BRICS inayojumuisha nchi za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini bado unaendelea, huku nchi nyingi zikionyesha kuvutiwa ama kuwasilisha maombi rasmi ya kujiunga na mfumo wa BRICS. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan alisema wakati akiwa ziarani hapa China Juni 3 kwamba, Uturuki inatarajia kujiunga na BRICS, na mwishoni mwa mwezi Mei, serikali ya Thailand iliridhia muswada wa barua rasmi inayoashiria nia ya nchi hiyo kuwa mwanachama wa BRICS. Jamii ya kimataifa inafuatilia sana utambulisho wa nchi hizo mbili kama ‘mwanachama wa NATO’ na ‘nchi ya ASEAN,’ hali ambayo sio tu inapanua fikira za familia ya BRICS lakini pia inatoa ujumbe wa kipekee wa ujumuishi kwa ajili ya ushirikiano mpana zaidi wa BRICS.
Kiuhalisia, ‘uwazi, ujumuishi, ushirikiano na kunufaishana’ daima vimekuwa ni moto ya mfumo wa BRICS. Tangu mwanzo, mfumo huu umejiwekea kanuni ya kutojihusisha na masuala ya kisiasa, kutoegemea upande wowote katika migogoro, na kutotaka kuondoa mtu yoyote. Kanuni hizi hazijabadilika kabla na hata baada ya kundi hilo kuongeza nchi wanachama. Nchi zinazoendelea zinatambua kabisa moyo wa BRICS na kutambua mfumo wa ushirikiano wa kundi hilo. Mshauri wa Rais wa Nicaragua, Laureano Ortega Murillo anazifananisha nchi za BRICS na familia kubwa inayojitahidi kujenga dunia ya usawa zaidi. Kwa jamii ya kimataifa, hii haimaanishi tu kwamba ushirikiano zaidi katika Nyanja ya fedha, kutoa msukumo kwa uchumi wa dunia kukabiliana na changamoto, lakini muhimu zaidi, ina maana kuwa idadi kubwa ya watu watapata fursa ya kuwa na sauti ambayo kwa hakika wanastahili, jambo ambalo ni kiini cha kutimiza usawa na haki katika utaratibu wa kimataifa.
Wakati huohuo, Kundi la Nchi 7 (G7) nalo linafanya mkutano wake kuanzia Juni 13 hadi 15 nchini Italia, na kabla ya mkutano huo, ajenda ya kulazimisha vikwazo kwa upande mmoja na kuchochea mivutano kati ya kambi imewekwa wazi na vyombo vya habari. Imeripotiwa kuwa, Kundi hilo linatarajiwa sio tu kuendelea kuegemea upande mmoja katika vita kati ya Russia na Ukraine, bali pia kuichafua China kwa ‘kuisaidia Russia kukwepa vikwazi vya nchi za Magharibi.’ G7, linalojumuisha Marekani na wenza wake wakuu, linawakilisha kundi la nchi tajiri zaidi duniani lakini mara nyingi linaonyesha upekee na kulenga maslahi katika mtazamo wake finyu. Mtindo huu wa ‘kurusha ngumi’ ili kudumisha mamlaka yake duniani kwa kweli hauvutii, na pia si ajabu kwamba ufahari na ushawishi wa G7 si mkubwa kama ilivyokuwa awali.
Tofauti na G7, mfumo wa BRICS unatetea tabia ya ‘kukumbatia’ kuliko ‘kurusha ngumi.’ Mfumo huu unazingatia kuanzisha uaminifu wa kisiasa kwa msingi wa kuheshimu mamlaka na maslahi muhimu ya kila nchi, kushughulika na mabadilishano ya kitamaduni kwa udhati kwa msingi wa kuheshimu staarabu tofauti, historia, na njia za maendeleo, na kukumbatisha ushirikiano wa kiuchumi na kifedha kwa mtazamo wa usawa na kunufaishana bila ya kujihusisha na mazingira yoyote ya kisiasa.
Wakati likivutia nchi nyingi zinazoibuka kiuchumi, BRICS haijazitenga nchi zinazoendelea. Taasisi kama Benki Mpya ya Maendeleo ya BRICS zinakaribisha ushiriki wa nchi zinazoendelea. Wakati Dunia ya Kusini inaendelea kuonyesha kujiamini na haiko tena tayari kushiriki bila ya sauti katika mfumo wa kimataifa, ushirikiano mpana wa BRICS unajibu wito wa maendeleo ya kihistoria.
Katika siku za baadaye, BRICS, itakayokuwa na wanachama zaidi na wenzi, itakuwa kituo cha nguvu ya pande nyingi inayojizatiti katika kujenga utaratibu wa kimataifa ambao ni wa haki, usawa, na jumuishi, na kuifanya hatma ya jamii ya binadamu kuwa bora zaidi.