Ojuolegbha
JF-Expert Member
- Sep 6, 2020
- 1,278
- 797
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewasili jijini Budapest, Hungary kwa ziara ya kikazi ya siku nne (4) inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya Tanzania na Hungary.
Baada ya kuwasili, Waziri Kombo amefanya kikao cha ndani cha maandalizi na timu ya Tanzania kwa lengo la kutathimini maeneo ya kipaumbele ya ushirikiano baina ya Tanzania na Hungary katika sekta ya maji, elimu na kujengeana uwezo, afya, biashara na uwekezaji, utalii, nishati na mazingira, michezo na utamaduni.
Ziara hiyo ya siku nne (4) inafuatia mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Hungary, Mhe. Péter Szijjártó kufuatia kuendelea kuimarika kwa ushirikiano kati ya Nchi hizo mbili.
Aidha, Mhe. Kombo ameongozana na Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb.); Balozi wa Tanzania nchini Hungary Mhe. Hassan Mwamweta; Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri na viongozi wengine waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.