Ushirikina unavyoharibu maendeleo elimu Simiyu

kbm

JF-Expert Member
Joined
Oct 5, 2012
Posts
5,224
Reaction score
1,677
Simiyu- Imani za kishirikina ni tabia kongwe ambayo imekuwa ikiendelea katika jamii mbalimbali nchini ikiwamo mkoa mpya wa Simiyu.
Kutokana na imani hizo, wazazi au walezi wameshindwa kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwamo elimu.
Matokeo yake, mkoa huo upo nyuma, kiasi kwamba maendeleo za elimu katika baadhi ya shule ni duni.
Baadhi ya wazazi katika wilaya ya Bariadi na Itilima mkoani humo wamekuwa wakipinga huduma ya chakula shuleni kwa hofu ya watoto wao kurogwa kupitia vyakula hivyo.
Juhudi za Serikali shakani
Hofu hiyo inapingana na juhudi za Serikali za kutoa huduma ya chakula shuleni ili kuwezesha wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani yao.
Zoezi la utoaji wa huduma ya uji shuleni ambayo lilianza mwaka 2010 baada ya maagizo ya Serikali ngazi ya mkoa kwamba shule zote zitoe huduma hiyo.
Serikali ya Mkoa iliagiza kila shule ilime ekari mbili za mazao ya chakula na nyingine mbili za mazao ya biashara, lakini agizo hilo limekutana na upinzani kwenye wilaya za Bariadi na Itilima.
Utafiti uliofanywa katika shule 11 kati ya 151 zilizomo katika wilaya hizo umebaini kuwa suala la imani za ushirikina zimewafanya wazazi wawazuie watoto wao kupata huduma hiyo kama njia ya kukwepa kuchangia.
Mbali ya uwezo walio nao, wazazi wamekuwa wakishindwa kuchangia Sh100 kwa ajili ya watoto wao kupatiwa huduma ya uji shuleni.
Anaongeza kuwa mwaka 2009, shule yake yenye wanafunzi 836 na walimu 12 ilianza kutoa huduma ya chakula cha mchana baada ya kulima viazi, na baada ya kumaliza viazi walilima mazao ya chakula kama mahindi na mtama.
“Zoezi hili hufanikiwa kipindi cha njaa wakati familia nyingi hazina chakula na siyo wakati wa mavuno ambapo wazazi huwazuia watoto wao wasile shule kwa hofu ya kurogwa”anasema Mwalimu Omary Ndogosa wa Shule ya Madilana.
Wazazi watishia walimu
Wazazi wengi walifikia mahali pa kumtishia maisha kwamba watoto wao wakipata madhara atakoma.
“Shule ya Msingi Madilana ilisitisha utoaji wa huduma ya chakula shuleni Machi 2010 baada ya wazazi kudai kuwa mtama umeharibika wakati umelimwa mwaka huo huo na shule yao,”anaeleza.
Hatua ya wazazi kuwazuia watoto wao kunywa uji shuleni ni kukwepa kuchangia fedha kwa ajili ya huduma hiyo.
Hali katika shule
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bumela, Andreycus Nyaki anasema shuleni kwake hali hiyo pia ipo. Anasema suala ya wazazi kuwazuia watoto wasipate huduma ya chakula shuleni ni tatizo kutokana na mwamko mdogo wa wazazi katika kuchangia maendeleo, achilia mbali shule nyingi kutokuwa na vitendea kazi kama vile madawati.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Laini A , Kata ya Sagata, Charles Misuko anasema shule yake haitoi huduma hiyo kutokana na tatizo hilo pamoja na wazazi kushindwa kuchangia fedha za malipo ya wapishi.
Athari za kutokula
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwaswale, Mabeja Masanja anasema kitaaluma kushinda na njaa shuleni kwa wanafunzi ni moja ya sababu ya kufanya vibaya katika mitihani na kushuka kwa kiwango cha elimu wilayani humo.
Aidha, James Peleke ambaye ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Laini B, anasema wao wanataka kupandishwa kiwango cha elimu, lakini jamii haielewi umuhimu wa elimu na lishe.
Wanasiasa nao wanaharibu mambo
Mratibu wa Elimu ya Msingi na Sekondari, Tarafa ya Bumela, Kidamli Sanangu anasema changamoto kubwa iliyopo ni shinikizo la wanasiasa.
Anadai wanasiasa wakishirikiana na wenyeviti wa kamati za shule wamekuwa wakichangia kushuka kiwango cha elimu.
Hao ni madiwani, wenyekiti wa kamati za shule ambao hata hivyo itikadi zao hazielezwi ingawa anaeleza kuwa wamekuwa wakidai kuwa wakichangia chakula shuleni, walimu ndio watajinufaisha , kitu ambacho si kweli.
Shule zimesitisha ulaji, wanafunzi wengine walia
Baadhi ya wanafunzi katika shule hizo wanasema kuwa, wanalazimika kusoma bila kupata uji kutokana na shule nyingi kusitisha huduma hiyo.
Sayi Masuka kutoka Madilana anasema tatizo hilo linawafanya washindwe kufanya vizuri darasani kutokana na wakati wa mchana watoto kuwa na njaa.
Masuka, mwanafunzi wa darasa la saba katika shule hiyo anasema ni kweli baadhi ya watoto shuleni kwao hawanywi uji baada ya kuzuiwa na wazazi.
Mwingine, Ganiyi Sinyangi anasema licha ya wazazi hao kuwazuia kunywa uji kipindi cha mavuno , wakati wa njaa huwaruhusu kufanya hivyo.
Mlo mbadala shuleni kwa wenye uwezo
Anasema uji unaopikwa katika shule nyingi hauna sukari, ila wanachokifanya wanafunzi ni kuja na juisi ya unga ambayo ipo katika pakiti ambayo huuzwa kati ya Sh100 mpaka Sh200 madukani na huchanganywa na uji ili kuufanya uwe na radha.
Tatizo ni uelewa mdogo wa wazazi
Sinyangi Minzi ambaye ni mzazi anasema tatizo hilo linatokana na uelewa mdogo wa baadhi yao kuhusu umuhimu wa elimu kwa watoto.
Anasema Serikali ilifanya jambo la maana la kuanzisha huduma hiyo katika mkoa huo unaokabiliwa njaa kwa kipindi cha kiangazi, viongozi wa Serikali wanapaswa kukemea tabia hiyo.
Kauli ya wataalamu wa elimu
Afisa Elimu, Sayansi Kimu wa Shule za Msingi Wilayani Bariadi na Itilima , Mihayo Magelle, anazitaja shule lukuki zenye tatizo hilo.
Hizo ni Madilana, Senani, Nangale, Migato, Mhunze, Shishani na Mwangwali Nyanguge ambazo hutoa huduma hiyo wakati wa njaa.
Anasema imani za ushirikina zimesababisha shule kadhaa za msingi katika wilaya ya Bariadi kushindwa kutoa huduma ya chakula kwa wanafunzi kwa kuhofia kurogwa katika kipindi cha mwaka jana. Shule hizo ni Madilana na Ndoleleji.
Anasema baada ya Bariadi kugawanywa na kuwa wilaya mbili mwishoni mwa mwaka jana, wilaya hiyo kwa sasa imebakiwa na shule 151 kati ya 190 za awali.
Ni shule 11 tu kati ya 151 ndizo zinazotoa huduma za chakula Shuleni
Anasema katika shule 151 zilizopo, ni 11 pekee ndizo zinatoa huduma ya chakula, ambazo ni Gaswa, Sagata,Nyawa, Nyanguge, Nguno, Migato, Kimali, Mhunze, Madilana, Nangale, Mwamigagani na Madilana.
George Momboja, Ofisa Elimu, Kilimo na Ufugaji Wilaya ya Bariadi anasema hakuna mtoto ambaye alipata madhara ya kurogwa baada ya kunywa uji shuleni.
Kwanini wanahisi kuna uchawi?
“Imani hizi potofu zilianza mwaka 2010 baada ya agizo la Serikali kutaka kila shule kutoa huduma ya uji shuleni, hadi sasa hakuna mwanafunzi wala walimu ambaye amepata madhara au kurogwa baada ya kunywa uji shuleni,”anasema.
Wazazi wapingana nae
Hata hivyo baadhi ya wananchi wanapingana na kauli hiyo wakisisitiza kuwa wao hawashindwi kulipia, bali ni kweli kwamba kupitia vyakula ni rahisi kumroga mtu, ndio sababu hawafurahii sana watoto kula shuleni.
Nini kifanyike
Anasema ni wajibu wa wanasiasa, wadau wa elimu na taasisi mbalimbali kwa ujumla kuhamasisha jamii katika kuchangia maendeleo ya lishe na elimu kwa watoto wa shule na sio kuiachia serikali pekee.
Anashauri jamii ishiriki kwa kuchangia maendeleo na siyo kusubiri misaada ya wahisani, kwani ili mtoto aweze kufaulu vizuri anahitaji kupata chakula shuleni.

Chanzo: MCL
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…