SoC02 Usimdharau binadamu mwenzio

SoC02 Usimdharau binadamu mwenzio

Stories of Change - 2022 Competition

Kasiano Muyenzi

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2018
Posts
13,858
Reaction score
22,729
Mimi ni kijana niliyelelewa na kukulia chini ya malezi ya mama ,baba yangu alifariki nikiwa bado mdogo mama alinilea vyema akiwa ni mwajiriwa wa serikali, alinisomesha nami nikasoma kwa bidii nikamaliza elimu ya msingi na nilichaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari hadi kidato cha sita na kufaulu.

Baadae nilijiunga na chuo cha usimamizi wa fedha na baada ya masomo nilipata kazi katika Halmashauri ya jiji la Dar kitengo cha uhasibu.

Mama alifurahishwa sana na matokeo hayo, aliniambia kuwa nijiepushe na ndugu wengine hasa ndugu zake wasio na elimu na ambao huja Dar kuomba msaada wakitokea Simiyu (nyumbani kwao na mama) sikupenda kuwa karibu na ndugu 'maskini ' wa huko Simiyu.

Pamoja na kupata kazi nzuri niliendelea kuishi kwa mama na niliishi hapo kwa ushauri wa mama mwenyewe ambaye alikuwa sasa anajiandaa kustaafu serikalini na alipenda niishi naye nami nilipenda pia kuishi na mama yangu nimpendaye sana na tuliishi kwa furaha mno.

Kuna wakati mama aliwahi kunisimulia kuhusu kaka yake aitwaye Koroboi kuwa ni mtu anayemnyimaga usingizi. Sikuwahi kufatilia anamnyimaje usingizi maana mjomba aliishi huko Simiyu.

Ilitokea siku moja nikiwa nje ya mkoa kikazi mama alinipigia simu kuwa mjomba koroboi kaja na rafiki zake 2. Mama alitafuta namna ya kuwafukuza akashindwa pa kuanzia hivyo akanipigia kunipa taarifa nirudi haraka niwaondoe ili apate 'usingizi'

Nilistuka kwa taarifa hiyo na nilimjibu kuwa kesho nakuja nitamalizana nao. Nilikuwa na jazba nyingi juu ya mjomba Koroboi, kulingana na masimulizi ya mama sikuwahi kumpenda kabisa huyu mjomba amnyimae usingizi mama yangu kipenzi.

Mjomba Koroboi, alikuwa na tabia ambayo mama hakuipenda, kila ajapo nyumbani kwa mama huufanya huo mjengo kuwa kanisa kwa kuanzisha maombi ya kukemea mapepo kwa sauti ya juu, akisema nyumba hiyo ni kijiwe cha washirikina! lakini cha ajabu hana hela, hana nyumba, hana gari yaani ni maskini wa kutupwa ajiitae nabii, mara mchungaji yaani ni kero tupu, hivyo hawakuwa wakipatana kabisa na mama.

"Nikitua tu Dar nitakata tiketi kabisa kisha niwapelekee waondoke kesho yake tu." nilimjibu mama na akanisisitiza nisikawie.

Nilitua Dar kesho yake jioni , nikapitilizia kwenda kukata tiketi na kisha nikaelekea nyumbani kwa mama

Nilifika nyumbani saa 2 usiku nikakuta makelele mengi pale sebuleni mjomba Koroboi alikuwa akiomba huku anatembea kila kona akisema kwa sauti kubwa "ninaagiza moto ulao ushuke ndani ya hili jengo, uteketeze madhabahu zote za kichawi ndani ya hii nyumba , nabatilisha maagano yote ya kichawi aliyoyafanya dada Mbuke na mapepo , katika Jina la Yesu Kristo wa Nazareth yashindwee ,,,,,,,,"

Nilishikwa na hasira kusikia mama anatajwa na mjomba kuwa alifanya maagano ya kichawi! sikumuona mama hapo sebuleni, ni mjomba tu pamoja na hao watu wake ndio pekee walikuwepo hapo sebuleni wakikemea kwa sauti za juu kabisa , sikusubiri wamalize hayo makemeo yao, nilimvaa mjomba na kumkwida shati na kuanza kumtoa nje kisha nikamwambia "mjomba kama anataka kuhubiri na kukemea mapepo nenda sokoni au gerezani na sio nyumbani kwa mama yangu!"

Mjomba alinikazia uso kisha akasema "kijana usishindane na Mungu,,,,," kabla hajamaliza nilimkatisha kwa kumuuliza kwa kebehi "wewe ni Mungu? huna hela, gari, umekaa kichizi chizi tu halafu unaleta umungu hapa , una akili kweli ?" alipotaka kusema nilimkatisha kwa kumwambia "chukua vitu vyako na watu wako muondoke haraka tiketi zenu hizi hapa na iwe mwanzo na mwisho kuja hapa!

Niliita bajaj ikaja ikawabeba na kuwapeleka stendi.

Mara tu baada ya mjomba na watu wake kuondoka nilimtafuta mama huko chumbani kwake na kumkuta akiwa amelala sakafuni anatoa povu hana fahamu, sikujua ni nini kimesababisha awe hivyo, haraka nilipiga simu kuita ambulance ije kumpeleka hospitali kwa uchunguzi zaidi.

Matokeo ya uchunguzi yalionesha hana tatizo lolote!

Nikiwa nashangaa shangaa kuhusu hayo matokeo, ujumbe uliingia katika simu yangu mtumaji akiwa ni mjomba Koroboi , sms ilisomeka hivi;

"Mami umefanya kosa kubwa sana kwa kukatisha maombezi ya kumkomboa mama yako, we hujui lolote kuhusu mama yako ni mchawi na hutumika kichawi kila siku kuroga watu , Mungu alinituma nije hapo kumtoa katika maagano ya kichawi na kumkomboa aokolewe, lakini wewe umetufukuza tena kwa dharau kubwa, sawa, tumeondoka Ila nikuambie tu kitakacho tokea hapo nyumbani usihangaike kutafuta dawa za hospital wala za mitishamba maana hazitaleta ahueni yoyote kwake , Ila ukiona shida inazidi tafuta mtumishi mwenye nguvu za Mungu akusaidie kumrejesha mama yako na wewe pia katika hali ya kawaida. "

Niliusoma huo ujumbe mara tatu kisha nikarejea katika majibu ya uchunguzi aliofanyiwa mama nikachoka kabisa Ila nikasimama kiume na kumjibu mjomba kwamba asinitishe na hayo maunabii yake ya kimchongo, kisha nikafuta sms zake na kublock namba yake!
Swala la mama kuwa mchawi sikulikubali kabisa!

Usiku huo mama alilala hapo hospitali na asubuhi aliruhusiwa kurudi nyumbani.

Huu ni mwezi wa sita sasa tangu tukio hilo litokee , hali ya mama haijawahi kuwa nzuri kabisa , nimetumia fedha nyingi ili kumrejesha mama katika hali yake ya kawaida lakini wapi! Elimu yangu hainishawishi nikubali kuwa mama ni mshirikina na ili kumuokoa nahitaji nimpeleke kwa mtumishi mwenye nguvu za Mungu akaombewe. Kinachonipa shida ni hiki "sijui ameroga ama amerogwa" Ila hali unazidi kuwa mbaya kila siku.


Niliota ndoto siku moja kuwa nanyang'anywa tonge la ugali na mjomba, nilishindana naye Ila mwisho wa ushindani huo mjomba alitwaa hilo tonge kisha akalitupa mbali wala sikujua lilipo angukia kisha ndoto ikapotea.

Mwezi mmoja baada kuota hiyo ndoto nilipokea barua ya kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa hela za halmashauri! Miezi 3 imetimia bila kuwepo kazini sina hela za kumtibu mama, gari ya mama na gari langu zote zimepaki hakuna hela ya kununulia mafuta, najiona kabisa nipo njiani kupelekwa kifungoni japo siku haijafika maana upande wa mashtaka wapo sahihi na nafsi inanisuta , Ila najiuliza sana mjomba Koroboi ndiye kanisababishia haya?

Kuna wakati nawaza kuwa ni ndoto tu niliota Ila mjomba hawezi kunifanyia hivi. Kuna wakati pia huwaza kuwa nilimkosea adabu kipindi kile ,yaani mawazo ni mengi mno

Natamani kumtafuta mjomba nimuombe msamaha lakini moyo unasita kwa kuona aibu.

Kila siku ule ujumbe wa sms kutoka kwa mjomba hunijia kwa sauti Ila huwa nakosa majibu badala yake nabaki najiuliza nifanyeje sasa?

Nadhani kumdharau mtu yeyote haifai.
 
Upvote 5
vunja ukimya ongea na mjomba...... lakini kabla ya kuongea na mjomba embu tafuta ukweli juu ya jambo hili kwa ndugu wengine( kwa upande wa baba na mama) huwenda ukapata ukweli juu ya jambo hili.
Nalifanyia kazi wazo lako ndugu, asante kwa ushauri.
 
Dah pole sana nenda kwenye maombi usisubiri mpaka maji yafike shingoni
 
Haya yametokea kwenye familia yetu mwaka jana,mjomba alimtishia atampiga mama risasi kwani amekuwa akimuona mama na wenzie wanaenda kumchawia nyumban kwake ingawaje mama na mjomba wapo mikoa tofaut

Ndugu karibia wote wa mama wanasema mama yetu ni mshirikina kumbe sijui kuna mizimu anayo ndo inamtumia na hao ndugu zake waliwah mpeleka mpaka kwa mganga ili kumtenganisha na mizimu hyo ingawaje mama hajaw kutueleza hicho kitu sie wanae

Wadogo zangu walipanik sana na kufuta namba za ndugu wa mama
Mama yeye husema kuwa hajui chochote
 
Haya yametokea kwenye familia yetu mwaka jana,mjomba alimtishia atampiga mama risasi kwani amekuwa akimuona mama na wenzie wanaenda kumchawia nyumban kwake ingawaje mama na mjomba wapo mikoa tofaut

Ndugu karibia wote wa mama wanasema mama yetu ni mshirikina kumbe sijui kuna mizimu anayo ndo inamtumia na hao ndugu zake waliwah mpeleka mpaka kwa mganga ili kumtenganisha na mizimu hyo ingawaje mama hajaw kutueleza hicho kitu sie wanae

Wadogo zangu walipanik sana na kufuta namba za ndugu wa mama
Mama yeye husema kuwa hajui chochote
Dawa ni kuokoka tu yaani kumwamini Yesu ndio njia iliyosahihi.
 
Kaka Yesu yupo kwa ajili yako mwamini leo utatoka kwenye hizo shida.Tafuta kanisa zuri la kiroho linalosimamia Neno la Mungu kwa weledi na onana na mchungaji wa Hilo kanisa .
Pia wasiliana na mjomba umuombe msamaha na akupedetails kuhusu mama yako.Asante
 
Back
Top Bottom