Usimdharau Mtu

Usimdharau Mtu

tamu 3

Member
Joined
Dec 11, 2024
Posts
63
Reaction score
122
USIMDHARAU MTU

1.
Za kale hapo zamani, hadithi inaanzia,
Yamhusu Yasmini, binti aliyevutia,
Mnene wa wastani, watu aliwazuzua,
Usimdharau mtu, ungali humfahamu.

2.
Juma mwana mtulivu, wa familya masikini,
Alikuwa si muovu, mwerevu pia makini,
Hakuwa mwenye uchovu, kumwendea Yasmini,
Usimdharau mtu, ungali humfahamu.

3.
Juma limpenda sana, huyo binti Yasmini,
Mara alipomuona, akaripuka moyoni,
Akaomba kuoana, waishi kwake nyumbani,
Usimdharau mtu, ungali humfahamu.

4.
Yasmini alicheka, alicheka alicheka,
Sababu ana viraka, nguo zimemraruka,
Juma alikasirika, machozi yakamtoka,
Usimdharau mtu, ungali humfahamu.

5.
Yasmini hakupenda, Juma kwao masikini,
Wanashindia mlenda, mkali kama kwinini,
Juma mwili ukakonda, mawazo mengi kichwani,
Usimdharau mtu, ungali humfahamu.

6
Ilipita myaka mingi, Juma anahangaika,
Akiujenga msingi, maisha yakijengeka,
Limpenda watu wengi, viunzi akivivuka,
Usimdharau mtu, ungali humfahamu.

7.
Upande wa Yasmini, liolewa nae pia,
Mwanaume mwenye dini, kijijini metokea,
Ana chache mfukoni, hela ukihesabia,
Usimdharau mtu, ungali humfahamu.

8.
Juma alishafungua, kubwa sana kampuni,
Nchini ikaenea, matawi ni ishirini,
Watu walijivunia, bidhaa zake sokoni,
Usimdharau mtu, ungali humfahamu.

9.
Mume naye Yasmini, maisha lienda kombo,
Hawana chakula ndani, hawawezi kwimba wimbo,
Wakawaza kwa makini, walifanyaje moja jambo,
Usimdharau mtu, ungali humfahamu.

10.
Mumewe wa Yasmini, mwishowe lipata jibu,
Alienda kampuni, komba jambo ajaribu,
Juma aso hayawani, Akalijibu jawabu,
Usimdharau mtu, ungali humfahamu.

11.
Siku moja Yasmini, memtembelea Juma,
Kule kwake kampuni, kwake nguvu alihema,
Kijilaumu moyoni, kujikosea heshima,
Usimdharau mtu, ungali humfahamu.

12.
Yasmini alilia, kwa kumpuuza Juma,
Aliishi kijutia, lipuuza huko nyuma,
Juma kimkumbukia, kwa werevu na hekima,
Usimdharau mtu, ungali humfahamu.

13.
Mwisho wake Yasmini, mmewe walitengana,
Kisa ni maisha duni, kila siku kulumbana,
Machozi ya mashavuni, hakika yalipishana,
Usimdharau mtu, ungali humfahamu.

Denny Jeremias kitumbika
Mtunzi wa mashairi na ngano za Kiafrika
Mufindi Tanzania 10.3.2025
 

Attachments

  • 1737824204161.jpg
    1737824204161.jpg
    178.7 KB · Views: 1
Hongera kwa kipaji .wana jf tunakubali kukusapoti kwa hali na mali na karibu sana tena na tena
 
Back
Top Bottom