Mwananchi laongoza kwa kutopendelea-Utafiti
Wednesday, 15 September 2010
Nora Damian
WAKATI kampeni za uchaguzi mkuu zikigonga vichwa vya habari vya vyombo mbalimbali vya habari nchini, gazeti la Mwananchi linaongoza kwa kuandika asilimia 97 ya habari za uchaguzi bila ya upendeleo, kwa mujibu wa utafiti wa Synovate.
Meneja wa huduma kwa wateja wa taasisi hiyo ya utafiti ya Synovate, Jane Meela alisema mchakato huo ulioanza kati ya Agosti mosi na 31 mwaka huu, uliangalia habari za uchaguzi zilizokuwa zikiandikwa kwenye vyombo vya habari tangu kuzinduliwa kwa kampeni hizo.
CCM ndiyo ilikuwa ya kwanza kuzindua kampeni zake Agosti 21, na kufuatiwa na CUF Agosti 27 na Chadema Agosti 28.
Utafiti huo wa Synovate, kwa mujibu wa Meela, unaonyesha kuwa Mwananchi limekuwa likiandika habari za uchaguzi bila ya kuipendelea Chadema kwa kiwango cha asilimia 97 na CCM asilimia asilimia 95.
Meneja huyo alifafanua kwamba, taasisi yake ilifanya utafiti wa kufuatilia vyombo vya habari jinsi vinavyoripoti uchaguzi mkuu na kuongeza kwamba, katika utafiti huo kulikuwa na timu maalumu.
"Tulibaini kuwa viko vyombo vya habari ambavyo vinalalia upande mmoja katika kuchapisha ama kutangaza habari za uchaguzi mkuu na tunadhani ipo haja ya kuliangalia suala hilo kwa kina zaidi," alitahadharisha Meela.
Kwa mujibu wa Meela, utafiti huo ulihusisha magazeti ya kila siku, ya wiki, redio na televisheni mbalimbali.
Utafiti huo ulihusisha magazeti 36, vituo 28 vya redio na vituo 10 vya televisheni na kuangalia habari katika makundi ya habari zilizoandikwa ama kutangazwa kwa upendeleo, bila upendeleo na zile ambazo hazikuegemea upande wowote.
Mbinu waliyotumia katika utafiti huo kwa magazeti ya kila siku na yale ya wiki ni kwa kuyasoma na redio na televisheni ilikuwa ni kusikiliza na kutazama, kufuatilia habari zote zinazohusiana na uchaguzi, kuandaa muhtasari wa muktadha wa kihabari na kuchambua habari kwa ubora na kwa idadi yake.
Katika matokeo hayo, meneja huyo alifafanua kwamba Mwananchi iliongoza kwa kuandika habari za uchaguzi ambazo ni sawa kwa sentimita 41,060, likifuatiwa na Tanzania Daima sentimita 40,393, Nipashe 38,951, Uhuru 33,413, Majira 28,267, Habari Leo 28,455, The Guardian 22,171, Daily News 19,654, The Citizen 19,460 na Rai sentimita 15,256.
Meela alisema magazeti mengine yaliandika habari hizo kwa sentimita 149, 407 wakati kwa upande wa televisheni, TBC 1 iliongoza kwa kutoa sekunde 79,035 ikifuatiwa na ITV 40,553, Star TV 37,096, Mlimani TV 34,190, Channel Ten 30,902, Tanga TV 8,880, Abood TV 4,320 na TVZ 4,260.
Meela alifafanua kuwa Radio One ilirusha kwa sekunde 42,990, ikifuatiwa na TBC Taifa 39,225, Times FM 15,855, Redio Free Africa 14,190, Magic FM 7,698 na redio nyingine zilitangaza habari hizo kwa sekunde 44,280.
Kwa upande wa mambo yaliyopewa kipaumbele baada ya uzinduzi wa kampeni mnamo Agosti , Meela aliyataja kuwa ni pamoja na amani asilimia 28, rushwa 21, uchumi 15, kilimo 7, afya 6, haki za binadamu 3, ajira na utalii 1 na mengineyo 6.
Hata hivyo, alisema katika utafiti huo hawakuangalia vyama ambavyo vilikuwa havijaanza kampeni na kwamba walichokuwa wanaangalia ni habari zinazohusiana na uchaguzi mkuu.
NCCR Mageuzi ni moja ya vyama ambavyo hadi mapema mwezi huu kilikuwa bado hakijaanza kampeni kutokana na kuamua kuanza harakati zake baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Kwa upande wa chama kilichoongoza kupewa nafasi kubwa, Meela aliitaja CCM kuwa iliandikwa kwa wingi na kufuatiwa na Chadema.
Kwa mujibu wa matokeo hayo ya utafiti, chama hicho tawala kiliongoza kwa kupata asilimia 51, ikifuatiwa na Chadema 21, CUF 14, NCCR- Mageuzi 6, TLP 4, SAU 2 na DP 2.
Kwa upande wa televisheni, CCM bado iliongoza kwa asilimia 59, Chadema 19, Cuf 16, Nccr-Mageuzi 3, SAU 2 na TLP 2.
Kwa upande wa redio CCM, iliongoza kwa asilimia 55, Chadema 20, CUF 14, Nccr 5, SAU 4 na TLP 2.
Alifafanua kwamba, Chadema ilianza kuandikwa na kutangazwa kwa wingi baada ya kumtangaza Dk Willibrod Slaa kuwa mgombea wake wa urais. Slaa alikuwa mbunge wa Karatu na kwa sasa ni katibu mkuu wa Chadema.
"Katika utafiti wetu tumebaini kuwa televisheni nyingi zimekuwa haziegemei upande wowote katika kutangaza habari zinazohusiana na uchaguzi mkuu," alisema Meela.
Synovate ni taasisi ambayo imekuwa ikiheshimika nchini kutokana na tafiti zake mbalimbali katika mambo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.