beth
JF-Expert Member
- Aug 19, 2012
- 3,880
- 6,368
Utafiti wa vipimo vya awali vya Virusi vya Ukimwi(VVU) kwa vichanga waliozaliwa na akinamama wenye maambukizi umeonesha vipimo vipya vimefanya vizuri asilimia 100.
Utafiti wa ‘BABY’ uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kwa kipimo cha Early Infant Diagnosis(EID) ikitumia mashine za GeneXpert unabaini maambukizo ndani ya saa mbili.
Upimaji wa kawaida kwa maambukizi ya Ukimwi kwa watoto wachanga unafanywa kwa watoto wachanga wenye wiki nne hadi sita na majibu yake yalikuwa yakichukua wiki mbili.
Mkurugenzi wa NIMR Mbeya, Dk Nyanda Ntinginya aliwaambia wanahabari wa kampeni ya ‘Tumeboresha sekta ya afya’ kipimo hicho kwa mtoto kinachukua siku mbili kutoa majibu.
Utafiti uliofanyika Julai 2015 hadi Novemba 2016 NIMR Mbeya kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Munich cha Ujerumani ulilenga kutathimini vipimo vya awali vya VVU kwa vichanga ambao wazazi wao wameathirika.
Alisema utafiti huo ulilenga kutathmini vipimo vya awali vya VVU kituo cha kutolea huduma ambapo vipimo hufanywa na wauguzi tofauti na sasa ambao huhitaji wataalamu wa maabara hivyo kuhusisha usafirishaji sampuli za damu.
Alisema matokeo ya utafiti yameonesha vipimo hivyo vilifanya vizuri kwa asilimia 100 na vinatoa majibu ndani ya saa mbili na hivyo mgonjwa kupewa majibu yake siku hiyo hiyo ukilinganisha na upimaji wa kawaida ambapo huchukua wiki mbili au zaidi kupata majibu.
Matokeo ya utafiti huo uliofanywa pia Afrika ya Kusini na Msumbiji umepelekea Shirika laAfya Duniani(WHO) kutoa miongozo ya upimaji wa VVU kwa vichanga muongozo wa utoaji wa huduma za VVU wa mwaka 2016.
Kuhusu chanjo ya UKIMWI, Mkurugenzi huyo alisema miaka minne NIMR Mbeya imefanya tafiti za chanjo ya VVU kuiwezeza Tanzania kuwa kati ya nchi chache duniani zilizoshiriki tafiti kubwa tatu za majaribio ya chanjo hiyo.
“Majaribio hayo yamefanywa kwa kushirikiana na Mtandao wa Chanjo za UKIMWI duniani na Serikali ya Marekani. Zinaangalia usalama wa chanjo kwa matumizi ya binadamu na ubora wa kusisimua kinga ya mwili kwa VVU,”alisema.
Chanzo: Habari Leo