Utajiri wa rafiki yangu ulivyofanya nikamuamini Shetani - 25
Mimi "Nashukuru sana kaka"
Ally Mpemba "Usijali brother,haya ni maisha tu ila unapaswa uwe makini"
Aliendelea "Tatizo lako master huwa unajisahahu sana hadi kuepelekea kunisababishia matatizo,kuna muda napenda tufanye mambo makubwa sana ila naona bado una changamoto zako!"
Mimi "Lakini kaka nishajifunza na sitorudia kufanya makosa "
Ally Mpemba "Ngoja tuone "
Baada ya mazungumzo na Ally niliondoka zangu kuelekea maskani huku nikiwa nafuraha kwssababu jamaa alikuwa amenipatia laki tano.Mambo yalianza kurudi kwenye mstari baada ya kupitia matatizo ya kiuchumi kwa siku kadhaa.
Kila ulipokuwa ukifika mwisho wa mwezi kama kawaida ile bangiri niliyokuwa nimeivaa ilikuwa ikibana sana na damu zikinitoka lakini mwisho wa siku sikuwa napata fedha kabisa na nilipokuwa nikimuuliza Ally Mpemba yeye aliniambia ni kwasababu nimekiuka masharti,sasa ile hali kiukweli iliendelea kunitesa sana na nisingeweza kuishi na kitu ambacho kinaendelea kunitesa na manufaa siyaoni.
Nilimuomba sana Ally Mpemba aweze kuniombea kwa Sheikh yule wa Chumbe kama kuna jambo lolote niweze kufanya ili ikiwezekana nitolewe ile bangiri ambayo iliendelea kunitesa,Ally Mpemba alionekana kama kuwa mbishi lakini alipoona nakomaa sana aliniambia atanirudisha tena kwa mzee lakini ni baada ya Mwezi utakaofatia.Sikuelewa ni kwanini jamaa alikuwa anakomalia mimi kuendelea kuivaa bangiri ambayo ilikuwa ikiendelea kuniumiza na haikunipa chochote zaidi ya kunitoa damu zangu.
Sasa nakumbuka jamaa aliniambia kabla ya kunipeleka kwa Mzee inapaswa kwanza nianze kutafuta wafanyakazi wa ile hotel/mgahawa wake.Kweli,sikutaka kabisa kupoteza muda kwasababu alikuwa ameniahidi atakuwa ananilipa kila mwezi kama msimamizi,yeye alijiweka kando kabisa ingawaje watu walikuwa wakifahamu ni mgahawa wa jamaa.
Niliwashirikisha mademu na washikaji tuliokuwa tukifanya nao kazi ya usajili wa line kila nilipokuwa nikienda ofisini pale buguruni,niliwapata mademu 3 na mshikaji mmoja ambao wao walikubali,kikichofanya wakubali pia ni kwasababu mauzo ya line kwa wakati huo yalianza kupungua,pia wale mademu ni kama walikuwa wamechoka na ishu za kusajili line maana waliona ni kama ilikuwa ikiwadharirisha.Pamoja na hao lakini nakumbuka jamaa aliongea na yule Mama aliyekuwa mpishi wa ile Catering yake akawa amemtafutia wafanyakazi wengine.Jumla mara ya kwanza kulikuwa na wafanyakazi 6,wakike 4 na wakiume wawili.
Baada ya kuanza kazi kwa ule mgahawa mimi pia nikawa nimeacha kazi rasmi ya usajili wa line nikaanza kusimamia ule mgahawa,mimi nilikuwa nakusanya mauzo yote kwa siku na ndiye nilikuwa msimamizi mkuu wa ule mgahawa.Mgahawa huu ulikuwa mtaa wa mkunguni nyuma ya Big bon jirani kabisa na Soko kuu la Kkoo.
Kiukweli tulikuwa tunauza sana na hatukuuza kama ujuavyo wewe bali ilikuwa ni nguvu za kishirikina.Nakumbuka kuna siku Ally Mpemba alipoona mgahawa unachanganyia sana aliinita nyumbani kwake,nilipofika tukawa tumejadili namna ya utoaji wa kafara maana alikuwa ameniambia tangu mwanzo ni kazi ambayo ningekuwa naifanya mimi.
Mimi "Niambie kaka namna ya kufanya"
Ally Mpemba "Kabla ya kufanya chochote orodhesha majina ya wafanyakazi wote kisha mimi nitayatuma kwa Sheikh Unguja"
Nilianza kumuorodheshea majina ya wafanyakazi wote wa ule mgahawa na kweli nilipompatia aliwasiliana na Sheikh akawa anamtajia,sasa baada ya muda kupita kuna majina Sheikh akawa ameyataja pale ambayo yote yalikuwa ya wanawake,walikuwa takribani 3,sasa wale wengine waliobaki hawakuwa na maana,Ally Mpemba aliniambia ikiwezekana niwafukuze waondoke kwasababu hawakuwa na umuhimu wowote kwenye ule mgahawa.
Kiukweli ilinipatia taabu sana kuwafukuza kwasababu hakukuwa na sababu maalumu ambayo ningewaeleza,nilianza kuwafanyia visa na nilikuwa mkali sana,niliamua kufanya uaminifu kwa Ally Mpemba ili kumridhisha kwasababu hapo nyuma nilikuwa nimemkwaza,sasa nilichokifanya ni kuwatafutia sababu wale wafanyakazi ambao Ally Mpemba aliniambia hawakuwa na faida na niliwalipa fedha zao na kuwaondoa,japo walinisihi sana nisiwafukuze lakini kiukweli sikuwa na namna,nilikuwa naumia sana lakini ndugu zangu sikuwa na jinsi.Sasa wale waliobaki nilijaribu kuwapeti peti kwa marupurupu na kuwasifia ya kwamba wao wanapiga sana kazi kuliko wale niliowaondoa,kiukqeli hawakuelewa jambo lolote na wao walifurahi wakawa wanajipa kichwa kama kweli walikuwa wanafanya kazi kumbe ilikuwa ni mtego wa panya,kupitia wale wale wafanyakazi niliwaomba wanitafutie wafanyakazi waliokuwa wanajituma kama wao ili kujaza nafasi zilizokuwa wazi.Walifurahia sana na wakasema watawashitua ndugu zao ili waje wapambane.
Lile zoezi la kuwatimua halikuchukua siku moja bali ilikuwa ni prosesi ambayo ilichukua muda kwa takribani majuma mawili ili kuwatafutia sababu,hivyo nilivyomaliza hilo zoezi nilimwambia Ally Mpemba ya kwamba nimemaliza na nilikuwa natafuta wafanyakazi wengine wa kujaza nafasi,Ally Mpemba alinipongeza sana kwakupiga kazi na akaniambia mwisho wa Mwezi tutaondoka kulekea Unguja mara moja halafu tuwahi kugeuka.
Kweli,mwisho wa mwezi baada ya kuwa nimetoa damu kupitia bangiri langu la mkononi tukawa tumeondoka kuelekea Unguja kwa Sheikh,tulivyofika nakumbuka yule mzee alimwambia Ally Mpemba wale wafanyakazi itabidi kila baada ya miezi 6 awe anakufa mmoja kwasababu akisema iwe kila mwaka itakuwa mbali sana na majini yake aliyokuwa akiyafuga hayakutaka iwe mwaka,ndipo nikaja kugundua kwamba kumbe jamaa alikuwa akifuga majini na ndiyo yalikuwa yakimpa utajiri ule wote.
Yule mzee alimwambia Ally Mpemba ampatie shilingi milioni moja na Ally alifanya hivyo,baada ya kuipokea ile hela alianza kuifanyia dawa na baada ya kumaliza alimrudishia ile hela Ally Mpemba kisha akawa amemwambia ya kwamba.
Mzee "Hiyo hela hakikisha utakapokuwa unataka kuwalipa mshahara,utakuwa unachukuwa elfu kumi hapa na kisha unachanganya na fedha nyingine ndiyo unawalipa"
Ally Mpemba "Sawa Sheikh"
Mzee "Usiwalipe wewe,huyu kijana ndiye anapaswa kulifanya hilo jukumu"
Ally Mpemba "Hizi pesa anapaswa kukaa nazo yeye?"
Mzee "Siyo lazima akae nazo huyu,ila kama yakiwa yanafanyika malipo hakikisha ni lazima elfu kumi moja inatoka hapa kwenye hizo hela nilizokupatia"
Aliendelea "Na itakuwa kwa mmoja wapo wa mfanyakazi mliyemkusudia"
Ally Mpemba "Sawa nimekuelewa vema"
Kilichokuwa kinafanyika ni kwamba,kama kuna mfanyakazi ambaye tulikusudia afe baada ya miezi sita kutimia,nilikuwa nachukua elfu kumi moja kwenye ile milioni nachanganya na mshahara wake kisha nampatia,kwa mfano kama mshahara ilikuwa laki tatu basi ilikuwa namuandalia mfanyakazi laki mbili na tisini ambayo ilikuwa fedha ya kawaida na baada ya hapo nachukua na elfu kumi kutoka kwenye ile milioni moja kisha inakuwa laki tatu halafu ndipo namlipa mfanyakazi tuliyekusudia.
Baada ya maelekezo yale,Ally Mpemba alimwambia yule mzee afanye namna sasa ile bangiri iweze kunipatia fedha kwasababu tayari nishakuwa mwema kwake,lakini nilimuomba pia yule mzee anibadilishie ile bangiri kwasababu haikuwa na muonekano mzuri hata kidogo,kuna muda nilikuwa naonekana kama mganga wa kienyeji kwasababu tu ya mbangiri ule.
Yule mzee alinipatia Pete ndogo sana ambayo aliniambia niivae kwenye kidole cha kati na akasisitiza itafanya shughuli kama iliyokuwa ikifanya ile bangiri;kiukweli niliipenda sana ile pete kimuonekano kwasababu ilikuwa nzuri na ndogo pia,ingekuwa ngumu sana mtu kugundua,sasa lakini yule mzee akasisitiza sana ya kwamba nisije nikathubutu kuivua ile Pete kama ilivyokuwa kwa bangiri tu.
Baada ya kupata kilichotupeleka hatimaye tukarudi Dar es salaam,tulipofika Dar es salaam Ally Mpemba aliniambia zile fedha atakaa nazo na itakapofika mwisho wa mwezi ule wa sita atanipatia elfu kumi ili nijumlishe na fedha ya malipo ya mfanyakazi tutakayemkusudia.
Kiukweli ile Pete ilipokuwa ikifika mwisho wa mwezi ilikuwa ikibana kama ilivyokuwa bangiri na nilikuwa nikifanya kuituliza kama mwanzo,baada ya damu kumwagika nilikuwa nikipata fedha kama kawaida na zilikuwa nyingi kushinda mara ya kwanza,baada ya kupata zile fedha nilikuwa nikizihifadhi benki nikiwa na lengo la kuanza tena ujenzi upya.Niliendelea kupiga kazi kwenye mgahawa wa Ally Mpemba kwa uaminifu mkubwa na wale wafanyakazi wakawa wamewaleta wafanyakazi wengine,lakini kabla ya kuwaajiri Ally Mpemba akapendekeza kwanza majina yatumwe kwa Sheikh kule Unguja na majibu yakitoka vizuri tuwaajiri,majina yalirudi na kuonekana baadhi wanafaa na wengine hawafai(Hii ilikuwa inahusisha nyota ya bahati) wale waliofaa tuliwaajiri na wale ambao hawakufaa niliwatafutia sababu.
Ilipofika mwezi wa sita mwishoni kuna mdada ndiye tukawa tumekubaliana na Ally Mpemba nilimlipe pesa kupitia ile prosesi na kiukweli majibu yalikuwa mazuri,baada ya kumlipa ile fedha mkononi yule mdada aliipokea na mambo mengine ya kawaida yaliendelea,ingawa wote niliwalipa mkononi kila mmoja na fedha yake lakini yule mdada yeye ndiye tulikubaliana mwisho wa mwezi huo wa sita awe kitoweo kwa biashara ya Ally Mpemba.Taarifa tulizopata ni kwamba alipofika kwao aliugua ghafla na wakati anakimbizwa hospitali alifia njiani,ilikuwa ni huzuni kwa wafanyakazi wenzake waliokuwa wamezoeana lakini hakuna aliyefahamu ule mchezo,mambo yalikaa sawa hatimaye wakasahau na kazi ikaendelea kama kawaida.
Ally Mpemba yeye aliendelea kuingiza fedha nyingi sana na kwakuwa nilikuwa mshirika wake mkubwa nilikuwa naelewa kila kitu.
Baada ya muda kuwa umepita nakumbuka mwanamke wangu Rehema alipata likizo akawa amekuja kwao kisha akawa amekuja kunisalimu.
Itaendelea..............