- Awali ya yote nimshukuru Mungu aliyetupatia uzima na afya mpaka tulipofika sasa. Pia, niwapongeze wanajamii kwa kuendelea kufuatilia machapisho mbalimbali katika ukurasa wetu huu pendwa.
- Naomba nianze kwa kuangalia takwimu za maambukizi ya VVU na UKIMWI duniani kote na kwa Tanzania
- Takwimu kutoka shirika la kupamba na maambukizi ya VVU na UKIMWI duniani zinaonesha kuwa mapaka sasa takribani watu wapatao milioni 38 (38,000,000) duniani wanaishi na virusi vya ukimwi (VVU) au UKIMWI. Kati yao, milioni 35.9 wakiwa ni watu wazima walio na zaidi ya umri wa miaka 15 na takribani watu milioni 1.7 wakiwa ni watoto wenye umri chini ya miaka 15 (taarifa ya mwaka 2020 kutoka UNAIDS)
- Takwimu kuhusu vipimo: Takriban asilimia 84 (84%) ya watu wenye maambukizi ya VVU wameshapima VVU na kujua hali zao za kiafya. Hivyo takribani asilimia16% ya watu bado wanauhitaji wa vipimo vya VVU
- Takwimu Kuhusu dawa za kupambana na VVU- ARV: Mpaka kufikia mwisho wa mwaka 2020, watu wenye maambukizi ya VVU wapatao milioni 27.4 (73%) walikuwa na uwezo wa kupata dawa za ARV. Hivyo watu wapatao milioni 10.2 bado hawajaanza kutumia dawa za ARV. Kotokana na taarifa za UNAIDS, upatikanaji dawa na matumizi ni chachu au ufunguo katika kupambana na kutokomeza UKIMWI.
Je, takwimu kutoka Tanzania zinasemaje?
- UKIMWI ni miongoni mwa magonjwa 10 yanayoongoza kwa kusababisha idadi kubwa ya vifo nchini Tanzania.
- Taarifa kutoka shirika la kupambana na UKIMWI nchini Tanzania zinaonesha kuwa takribani watu milioni 1.7 wanaishi na VVU
- 77, 000 ni idadi ya maambukizi mapya ya VVU kwa mwaka 2019
- 27, 000 ni idadi ya vifo vilitovyotokana na UKIMWI kwa mwaka 2019
- Asilimia 75 (75%) ni idadi ya watu wazima wanaotumia madawa ya ARV kati ya watu wazima wenye maambukizi ya VVU
- Asilimia 66 (66%) ni asilimia za watoto wanaotumia madawa ya ARV kati ya watoto wenye maambukizi ya VVU
Je, mpango wa 95-95-95 ni nini?
- 95-95-95 ni mpango ulioandaliwa na shirika la kupambana na maambukizi ya VVU na UKIMWI, (UNAIDS) ukiwa na jina la 2025 AIDS TARGET ukiwa ni moja ya mipango ya kutokomeza kabisa UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
- Huu mpango unahusisha zaidi katika kuondoa vikwazo vya kisheria na kijamii katika upatikanaji wa huduma zinazohusiana na maambukizi ya VVU na UKIMWI. Pia, kuunganisha na kusaidia upatikanaji wa pamoja kwa huduma za VVU na huduma nyinginezo muhimu zinazohitajika kwa watu wenye maambukizi ya VVU pamoja na jamii zilizoko kwenye hatari kwa ujumla ili kuendeleza upatikanaji wa afya bora.
Zijue sehemu kuu za mpango wa 95-95-95:
- Chini ya asilimia 10 (10%) za nchi zote duniani ziondoe vikwazo vya kisheria na sera zinazozuia upatikanaji wa huduma zihusianazo na VVU na UKIMWI
- Chini ya asilimia 10 (10%) ya unyanyapaa na kutengwa kwa watu wenye maambukizi ya VVU kutoka kwa wanafamilia, jamii zao n.k
- Chini ya asilimia 10 (10%) ya unyanyapaa na mateso ya kijinsia dhidi ya watu waishio na VVU kama vile kubak(w)a, ukeketaji, n.k
- Asilimia 95 (95%) ya watu walioko kwenye hatari ya kuambukizwa VVU watumie njia mbalimbali za kujikinga dhidi ya VVU
- Asilimia 95 (95%) ya watu waishio na VVU watambue hali zao za kiafya. Kwa kuwa kuna baadhi ya watu wenye maambukizi ya VVU pasipo kujua hali zao za kiafya kuwa wana maambukizi hayo, huu mpango wa 95-95-95 unajikita zaidi pia katika kuhamasisha upatikanaji wa vipimo vya VVU hususa ni kwa jamii au watu ambao ni vigumu kufikiwa.
- Asilimia 95 (95%) ya watu waishio na maambukizi ya VVU na wanafahamu hali zao za kiafya juu ya VVU wanaanza matumizi ya madawa ya ARV. Hili pia inalenga zaidi makundi ya watu ambayo hayakufikiwa katika kampeni/mipango iliyopita
- Asilimia 95 (95%) ya watu wanaotumia madawa ya kupambana na VVU (ARV), viwango vya VVU katika damu vinadhibitiwa. Hili ni kwa kuwepo kwa matumizi sahihi ya dawa za ARV
- Asilimia 95 (95%) za upatikanaji wa huduma za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Hili ni kwa kuhakikisha asilimia 95 (95%) ya mahitaji ya kijinsia na afya ya uzazi kwa wanawake wenye umri kati ya miaka 15-49 yanatimizwa, 95% ya wanawake waishio na VVU wenye mimba na wanaonyonyesha viwango vya VVU kwenye damu vimedhibitiwa ipasavyo, 95% walioko kwenye hatari ya maambukizi ya VVU wanapata vipimo ifikapoa 2025
- Asilimia 90% ya watu waishio na VVU na walioko kwenye hatari ya kuambukizwa VVU wanaunganishwa katika mipango ya huduma kulingana na hali zao za kiafya.
Asanteni wanajamii kwa muda wenu, karibuni jukwaani
Call: +25578015660