SoC04 Utandawazi na changamoto ya Maadili

SoC04 Utandawazi na changamoto ya Maadili

Tanzania Tuitakayo competition threads

mtatasenior

New Member
Joined
May 11, 2014
Posts
1
Reaction score
0
SCOPE YA TATIZO: Tangu kuanza kwa karne ya 21 Taifa limekuwa katika mageuzi makubwa ya kuasili mifumo mbalimbali ya Tehama, lengo likiwa kuendana na ulimwengu. Mageuzi haya ya utandawazi yalipelekea kuhama kwa utamaduni wa kitanzania na kukaribisha mila na desturi za ulimwenguni.

Athari hii ilianza kwa watu wazima wa karne 19 ambao walipaswa kusimama na kuongoza muelekeo wa maadili na kurithisha tunu za Taifa katika kuhakikisha maadili yetu kama watanzania yanaendelea kuenziwa. Utandawazi ulianza kuwachukua na kuwafanya watumie muda mwingi kutafuta fedha ambayo kwa tafsiri ya utandawazi uchumi ulihesabika kuwa ni umiliki wa fedha sio umiliki wa vitu kama ilivyokuwa awali mfano: mashamba, mifugo na kuwa na familia kubwa.

Mtazamo huu ukabadili taswira na jukumu la malezi ambalo ndilo humuandaa mtanzania mwenye tunu ya maadili tuliyorithishwa na wazee wetu waliopigania uhuru wa Taifa hili. Malezi yakaanza kutekelezwa na wasaidizi wa kazi za nyumbani (house girl) ambao kwa kipindi hicho wengi wao walikuwa watu wazima, hivyo kufanya jukumu la malezi kwa Watoto wa waajiri wao kama lakwao. Kiwango cha umri wa wasaidizi hawa kiliendelea kushuka na kufikia hatua ya kufanywa na watoto wadogo, jambo ambalo hata serikali yetu tukufu ilianza kupiga vita ajira za utotoni kwa kuanzisha kampeni mbalimbali. Wakati huo jukumu la ulezi halikutizamwa kama inavyopaswa, mahitaji ya uchumi yaliendelea kuwalazimisha wazazi kutafuta mbadala wa kutekeleza jukumu hilo, ndipo zikaibuka zama za English medium na kupelekea kuonekana jukumu la malezi linapaswa kuwa chini ya shule kwani gharama za uendeshaji wa shule hizi ulikuwa juu na pia zilitoa ahadi ya kuhakikisha usalama wa mtoto kiakili, kiafya na kiroho (Imani).

Chagamoto ilianza kujitokeza pale ambapo idadi ya wanafunzi iliongezeka na kuzilazimisha shule kuhitaji walimu zaidi kukabili ongezeko la wanafunzi. Walimu waliopatikana walikuwa ni mazalia ya kizazi kilichokosa malezi ya wazazi hivyo kukosa uelewa wa kutafsiri maadili ya kitanzania, hivyo kuendelea kuzalishwa vijana wanaokosa muongozo wa kutafsiri nadharia na uhalisia wa maisha na kusababisha kumomonyoka kwa maadili.

WASHIRIKI WA TATIZO
  • Taifa kukosa mipango thabiti ya namna ya kukabiliana na athari za utandawazi katika tunu ya maadili ya mtanzania.
  • Wazazi kusahau jukumu la malezi na kudhani fedha inaweza kufanya kila kitu hata suala la malezi ya vijana wao.
  • Wizara ya elimu kushindwa kuwa na njia sahihi za udhibiti wa viwango vya elimu na utekelezaji sahihi wa mitaala, kaguzi nyingi zinazofanyika ni kutekeleza matakwa ya kikanuni jambo ambalo ni ukaguzi wa nyaraka za kitaaluma.
  • Vyuo vya ualimu ngazi zote vimeshindwa kuwaandaa wanazuoni ambao watakwenda kuleta suluhu ya changamoto zilizopo katika mazingira, hivyo kuzalisha wataalamu wenye ujuzi lakini wanakosa ukomavu wa kuziishi changamoto katika taaluma zao.
  • Kutokana na athari ya kimalezi na kukosa kujitambua, vijana wamekuwa wagumu kufundishika kutokana na kutoeleweka dhamira, kuthaminiwa na kutambuliwa nafasi yao kwa jamii. Kukosekana kwa mambo haya, wameanzisha vita baina yao na jamii kulipiza kisasi kwa kufanya mambo yanayokwenda kinyume na maadili yetu kama njia ya kudai haki yao iliyopotea.
NINI KIFANYIKE
  • Tume ya mipango ya Taifa ielekeze nguvu katika kuzishauri mamlaka na kuzisimamia katika utekelezaji mipango ya kuongeza maadili kwa Taifa ngazi zote. Mipango hii inaweza kutekelezwa kwa kuanzisha kampeni za elimu ya malezi chini ya wizara ya Ustawi wa Jamii, kama ilivyoanzishwa kampeni ya afya ya akili na mapambano dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza, elimu hii ipelekwe mahususi kwa watumishi, lengo likiwa kuwasaidia watumishi kukabiliana na mapungufu ya kimalezi waliyonayo, hii itasaidia utambuzi binafsi wa jamii na kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto za maadili.
Tume hii ihakikishe viongozi wa dini wanasomeshwa elimu ya saikolojia na iwe kigezo cha lazima kwani Taasisi hizi za kidini zimekuwa na mchango mkubwa katika kuilea jamii na kuirithisha maadili mema. Lakini kwakuwa inakabiliwa na wimbi kubwa la viongozi wanaotokana na mfumo mbovu wa malezi, wanashindwa kuwalea waumini wao na kusababisha mivutano ya kifikra kwa waumini na kuwaacha katika sintofahamu.​
  • Wizara ya Elimu kudhibiti uendeshwaji wa vituo vya elimu ya awali (Day care and Nursery). Wizara irejee katika muongozo wa uendeshaji wa vituo hivi kwani kwa sasa havitoi huduma bali vinafanya biashara. Vigezo vya uendeshaji ni vya muhimu sana, muongozo unaeleza shule za awali ni mahali mtoto anajiandaa na Maisha ya shule hivyo sehemu kubwa anapaswa kujengewa uwezo wa kushirikiana na mazingira na si kujifunza nadharia ya shule kwa ngazi ya elimu ya msingi. Ni ngumu kwa mwalimu aliyehitimu kidato cha nne na kwenda kusoma mwaka mmoja wa ualimu wa shule za awali akaenda kumfundisha mtoto, kiumri mwalimu huyu anahitaji kulelewa lakini anapewa jukumu la malezi (yaani mtoto analea mtoto). Kama tunaendelea na mfumo huu, basi wizara ivielekeze vyuo vinavyofundisha walimu hawa vifundishe elimu ya malezi kwa maana ya saikolojia ya makuzi na mabadiliko ya kitabia kwa mtoto kila hatua ya umri wake.
  • Serikali kupitia wizara ya elimu kama ambavyo imeboresha miundombinu ya elimu kwa madarasa ya awali, ianzishe vituo maalumu vya malezi katika ngazi ya kanda au mikoa kwa kuanzia, na kuonyesha kwa vitendo namna sahihi ya kumlea mtoto kitaaluma na kimaadili, hili likifanyika litaongeza thamani ya malezi na ukuaji wa kizazi salama na chenye maadili na uwezo wa kukabiliana na changamoto katika jamii. Vile vile itapelekea kupatikana/kuongezeka kwa ajira na kupunguza tatizo la ajira nchini.
  • Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kubeba jukumu la uelimishaji wa kubadili tabia ili kuweza kuongeza juhudi kwa serikali katika mapambano dhidi ya Rushwa ambayo ni matokeo ya mfumo mbovu wa malezi, waelimishaji wa TAKUKURU wajengewe uwezo wa elimu ya malezi ili kuendelea kupunguza gharama kwa serikali na kusaidia juhudi hizo za mapambano zinazidi kuwa na tija na kupelekea kubadili mitazamo katika jamii.
  • Sheria na kanuni zinazosimamia ASASI ZA KIRAIA ziboreshwe ili kuziwezesha kutekeleza jukumu la kuelimisha kuhusu elimu ya malezi ili mapambano haya ya kimaadili yatekelezwe haraka na kwa ushirikiano wa kila mdau katika jamii.
  • Vyombo vya Habari kuongeza vipindi vinavyohusiana na mabadiliko ya kitabia, serikali ifanye makubaliano na vyombo vya Habari katika kusimamia aina ya maudhui ambayo yatatoa nafasi kwa jamii kuwa na elimu ya utambuzi wa maadili ya mtanzania na maadili yasiyofaa katika jamii yetu ya Tanzania.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom