Habari Mkuu
Kuna vitu muhimu vya kufahamu hasa linapokuja swala la talaka kwani watu wengi hudhani talaka ni jambo la wanandoa pekee, si kweli.
1. Talaka hutolewa na Mahakama, hivyo ili kupata talaka ni lazima ukafanye maombi Mahakamani na si kila Mahakama bali itakupasa kuzingatia maelekezo ya sheria kulingana na aina ya ndoa yenu
2. Talaka hutolewa kwa kuionesha Mahakama sababu za msingi za kuifanya iamini kuwa ndoa yenu hioyo hairekebishiki tena. Fahamu kuwa Mahakama yenyewe haipendi kutoa talaka/kuvunja ndoa za wapendanao.
3. Talaka itakupa uwezo wa kutambulika kama mtu asiye ndani ya ndoa, hii ina maana kuwa kwa wakristu wataweza kuoa/kuolewa tena na kwa waislamu itahesabu ongezeko la idadi ya nafasi ya kuoa mke mwingine, kwa watamaduni vivyo hivyo pia.
4. Talaka hutolewa kwa ndoa inayotambulika kisheria na ili kuthibitisha uwepo wa hiyo ndoa ni sharti pawepo cheti cha ndoa hiyo. Hii ni kwa ndoa za aina zote, kidini, kiserikali na kimila, ni sharti ndoa iwe imesajiliwa kwa msajili wa ndoa.
5. Kabla ya kufanya maombi ya talaka Mahakamani ni sharti muwe mmeshapita kwenye usuluhishi wa ndoa, na ikashindikana kusuluhishwa hivyo mkapatiwa hati ya kushindwa kwa usuluhishi. Usuluhishi unaweza kufanywa na Baraza la kata au mabaraza ya kidini ya usuluhishi wa ndoa, ila sharti Baraza hilo liwe linatambulika kisheria.
6. Baada ya talaka kinachofuata ni mgawanyo wa mali mlizochuma pamoja, hapa ni lazima ijulikane kuwa huu mgawanyo una wahusu watalaka pekee na wala hauwahusu watoto wao. Kumekuwa na mazoea na dhana kwamba mali tutawapa watoto, hii ni kinyume na sheria. Zipo kesi za Mahakama Kuu zilizopinga hili swala/mtazamo.
Mwisho kabisa, pole kwa maswahibu Mkuu, pima uzani wa unayopitia kisha tafakari vizuri kama kweli talaka ndjo suluhisho la hayo maswahibu. Ukiona ndio basi fuata utaratibu, ukikwama unaweza niuliza siku yoyote nitakupa mwanga pindi nitakapoona swali lako.
Kila la kheri.