SoC03 Utaratibu wa malipo ya fidia itokanayo na wanyama waharibifu

SoC03 Utaratibu wa malipo ya fidia itokanayo na wanyama waharibifu

Stories of Change - 2023 Competition

Finley

New Member
Joined
Aug 31, 2022
Posts
2
Reaction score
2
UTANGULIZI
Katika kuhakikisha kwamba wananchi wake (hasa wale ambao wanaishi Jirani na hifadhi za wanyamapori) wanaishi kwa furaha na amani, jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia wizara ya mali asili na utalii katika kitengo cha wanyamapori walitunga sheria, kanuni na taratibu zinazohusu uhifadhi wa wanyamapori ili kufikia lengo kuu la kuzuia migogoro ambayo inaweza kutokea baina ya Wanyamapori na binadamu. Miongoni mwa sheria na kanuni hizo ni Pamoja na ile sheria ya uhifadhi wa wanyamapori ya mwaka 2011 ambayo inasimamia utoaji wa fidia na kifuta machozi kwa waathirika wa Wanyama hatari na waharibifu. Miongoni mwa Wanyama hao ni Pamoja na simba, chui, fisi, nguruwe, Nyati, kiboko Pamoja na tembo.

Miongoni mwa vipengele vya sheria hii inayosimamia utoaji wa fidia na kifuta machozi kwa waathirika wa moja kwa moja kutokana na migogoro hiyo baina ya wanyamapori na binadamu; ni kipengele cha pili cha sheria hii kinachofahamika kama “malipo ya fidia”. Katika kifungu cha 3(1) cha sheria hii kinataja namna na utaratibu ambao unatakiwa kufanyika kwa waathirika ambao wamepatwa na uharibifu wa mazao yao au Wanyama wao kutokana na Wanyama waharibifu au Wanyama wakali. Pia katika kipengele hichohicho cha pili, kimetaja zuio la kupata haki ya fidia ambapo katika kifungu cha 4(1) (a) kimetaja zuio la haki ya kupata fidia kwa waathirika wa migogoro baina ya wanyamapori na binadamu kwa waathirka ambao uharibifu wa mazao umetokea katika eneo la shamba linalozidi hekari tano (5); pia kifungu cha 4(1) (b) kimetaja zuio la haki ya kupata fidia kwa waathirika wa migogoro baina ya wanyamapori na binadamu kwa wathirika ambao uharibifu umetokea kwenye eneo la shamba ambalo mazao yake hayakua katika hali mzuri ya ukuaji na hakukua na matarajio ya kupata mavuno.

Pia, katika sheria hiyo ambayo inaratibu utoaji wa fidia kwa waathirika wa migogoro baina ya wanyamapori na binadamu kuna kipengele ambacho kinaonyesha na kutaja kiasi cha malipo ya fidia na kifuta machozi kwa waathirika kama ifuatavyo:

  • Fidia inayohusu kifuta machozi kwa wafiwa ambao wamempoteza mpendwa wao kutokana na Wanyama hatari ni pesa taslimu milioni moja (1,000,000/=).
  • Fidia inayohusu madhara yatokanayo na wanyamapori na kupelekea ulemavu wa kudumu kwa muathirka ni pesa taslimu laki tano (500,000/=).
  • Fidia ya kumfariji muathirika aliyepata maumivu au majeraha ya muda mfupi kutokana na mnyama hatari ni pesa taslimu laki mbili (200,000/=).
  • Fidia kwa kifo cha mifugo mikubwa (hasa ng’ombe) ni elfu hamsini (50,000/=)
  • Fidia kwa kifo cha mifugo midogo (hasa mbuzi, kondoo, nguruwe na punda) ni pesa taslimu elfu ishirini na tano (25,000/=).
  • Kifo cha Wanyama wafugwao (kama mbwa na paka) ni pesa taslimu elfu kumi tu (10,000/=).
  • Pia fidia kwa uharibifu wa mazao (kwa eneo la shamba lisilozidi hekari tano (5)) ni kama ifuatavyo:
  • Hakuna malipo ya fidia kwa uharibifu wa mazao kwa shamba ambalo lipo chini ya nusu kilomita kutokea eneo la uhifadhi.
  • Fidia kwa shamba ambalo lipo umbali wa kuanzia nusu kilomita hadi kilomita moja (1km) kutoka eneo la uhifadhi ni pesa taslimu elfu ishirini na tano (25,000/=).
  • Kwa uharibifu uliofanyika kwenye shamba lililopo umbali wa kuanzia kilomita moja (1km) hadi kilomita nne (4km) kutokea eneo la uhifadhi ni pesa taslimu elfu hamsini (50,000/=).
  • Fidia kwa shamba ambalo lipo umbali wa kuanzia kilomita nne (4km) hadi kilomita tano (5km) kutoka eneo la uhifadhi ni pesa taslimu elfu sabini na tano (75,000/=)
  • Pia, kwa uharibifu wa mazao uliotokea kwenye shamba lililopo umbali zaidi ya kilomita tano (5 km) ni pesa taslimu laki moja tu (100,000/=).

Mapungufu yanayoathiri utekelezwaji wa sheria hii:
  • Ucheleweshwaji au hata kutotolewa kabisa kwa fidia kwa waathirka.
  • Matumizi ya lugha ngeni (lugha ya kiingereza) ambayo ni ngumu sana kueleweka na wahusika wakuu ambao ni wanakijiji waishio maeneo Jirani na hifadhi za Wanyamapori.
  • Kukosekana kwa usaidizi wa kisheria na kitaalamu wa kuelewa vipengele na vifungu vya sheria hiyo kutokana na ufinyu wa uelewa wa lugha ngeni na lugha za kisheria zilizotumika.
  • Kukosekana kwa ufafanuzi wa kutofautisha aina ya mazao; mazao yote yamepewa hadhi sawa katika utoaji wa fidia bila kujari thamani halisi ya mazao yaliyoharibiwa.
  • Kwa mfano, kimetajwa kiwango cha fidia kwa kuzingatia umbali ambapo uharibifu umetokea kutoka eneo la uhifadhi bila kuangalia aina ya mazao (kama ni zao la chakula au biashara).
  • Kifungu cha 4(1) (b) kimetaja zuio la haki ya kupata fidia kwa waathirika wa migogoro baina ya wanyamapori na binadamu kwa waathirika ambao uharibifu umetokea kwenye eneo la shamba ambalo mazao yake hayakua katika hali mzuri ya ukuaji na hakukua na matarajio ya kupata mavuno. Lakini haijabainishwa ni kwa kiasi gani muathirika angepata pungufu ya mavuno kama ilivyotarajiwa kulingana na hali ya ukuaji wa mazao hayo.
  • Kukosekana kwa watoa elimu inayohusu ufuatiliaji wa fidia kwa waathirka; hii hupelekea kukosekana kwa uelewa wa namna na utaratibu wa kufuata pindi uharibifu au hata kifo kimetokea.

Nini kifanyike?
  • Kuzingatia utolewaji wa fidia kwa wakati.
  • Kufanyike mabadiliko ya baadhi ya vipengele/vifungu vya sheria hiyo ambavyo vinaleta mkanganyiko kama ilivyoainishwa, Pamoja na kuongeza vipengele ambavyo havikuwekwa kulingana na wakati ambao sheria ilitungwa ili utekelezaji wa sheria hii uendane na wakati wa sasa. Hii ni Pamoja na:
  • Kuongeza kiasi cha fidia ili kuendana na hali halisi ya Maisha ya sasa tofauti na kipindi ambacho sheria ilitungwa (mwaka 2011).
  • Kutambua utofauti wa thamani ya mazao; hasa kati ya mazao ya chakula na mazao ya biashara.
  • Kuwatambua waathirika ambao wamepatwa na uharibifu kwa kuzingatia ukubwa wa shamba bila kuwaacha wale ambao wana mashamba makubwa Zaidi ya hekari tano (5) kama sheria ya sasa inavyotaja.
  • Kuweka nguvu katika utoaji wa elimu na uelewa kwa wanakijiji waishio Jirani na maeneo ya uhifadhi. Hii ni Pamoja na kutafasiri vifungu vya sheria husika kulingana na lugha ya taifa hata kabila husika.
  • Kubwa Zaidi ni kuhakikisha uhifadhi wa wanyamapori unazingatia ustawi wa Maisha ya binadamu Pamoja na mali zake.
Uhifadhi kwa ustawi wetu!
 
Upvote 3
Back
Top Bottom