..hii ni habari ya kwanza kuhusu kesi ya kina Zombe ambayo imeandikwa bila ushabiki wa upande wowote.
..kuna tabia miongoni mwa waandishi wa habari kuandika habari toka mahakamani ktk hali ya ushabiki-shabiki.
..habari toka mahakamani zinatakiwa kuandikwa bila dramatization ya aina yoyote ile.
..ufuatao ni utetezi wa mawakili wa Zombe na washitakiwa wengine.
..kuna tabia miongoni mwa waandishi wa habari kuandika habari toka mahakamani ktk hali ya ushabiki-shabiki.
..habari toka mahakamani zinatakiwa kuandikwa bila dramatization ya aina yoyote ile.
..ufuatao ni utetezi wa mawakili wa Zombe na washitakiwa wengine.
Habari Leo magazine said:Washitakiwa katika kesi ya mauaji inayomkabili Kamishna Msaidizi wa Polisi Abdallah Zombe na wenzake 12, wamedai kuwa wametolewa kama kafara kwa matakwa ya wakubwa wao.
Katika hoja zao za utetezi zilizotolewa na mawakili wao katika Mahakama Kuu ya Tanzania Dar es Salaam jana, washitakiwa hao walidai upande wa mashitaka uliibua ushahidi wa kupikwa ili kuwaharibia maisha, kazi na vyeo vyao.
Walidai kuwa hawana kesi ya kujibu, kwa vile upande wa mashitaka unaegemea zaidi katika ushahidi wa kimazingira ambao pia umeshindwa kuunganishwa ili waonekane wana kesi ya kujibu. Wakili Jerome Msemwa anayemtetea Zombe, alidai hakuna shahidi wa upande wa mashitaka aliyethibitisha kuwa mteja wake aliamuru kuuawa kwa wafanyabiashara hao.
Aliongeza kuwa hakuna shahidi aliyethibitisha kuwa mauaji hayo yalifanywa na Zombe mwenyewe. Alidai pia kuwa Zombe hajawahi kuhojiwa na mamlaka zozote kuhusu mauaji hayo. Wakili huyo alitamba kuwa hata Zombe akiamua kukaa kimya asijitetee katika kesi hiyo, hawezi kutiwa hatiani kwa vile upande wa mashitaka umeshindwa kuwasilisha ushahidi wa moja kwa moja, unaomfanya mteja wake aweze kutiwa hatiani.
Alisema hata Tume ya Polisi iliyoongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi Mgawe na Tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Kipenka Musa, iliona Zombe hana hatia katika mauaji hayo; badala yake ikapendekeza washitakiwe askari 15. Wakili huyo alidai hata shahidi kutoka kikosi cha 999 aliyekuwa zamu siku ya tukio la mauaji, alisema hakumsikia Zombe akitoa amri ya kuua.
Aliongeza kuwa aliyekuwa Mpelelezi Mkuu katika shauri hilo aliyemtaja kwa jina la Mkumbi, hakuwahi kushuhudia mawasiliano ya simu kati ya Zombe na Christopher Bageni anayedaiwa kusimamia mauaji hayo. Msemwa alidai kuwa upande wa mashitaka baada ya kukosa ushahidi katika kesi hiyo, sasa unategemea maelezo ya washitakiwa wa 11 na 12 ambao ni D 9321 Konstebo Rashid Lema, D. 4656 Koplo Rajab Bakari.
Washitakiwa hao ndio waliotoa maelezo yaliyomfanya Zombe akamatwe na kuhusishwa na mauaji hayo. Hata hivyo, wakili huyo aliiomba mahakama ikatae maelezo hayo kwani hakuna shahidi huru aliyeyaunga mkono. Msemwa alidai kuwa Zombe alishitakiwa bila kuchukuliwa maelezo, jambo alilolielezea kuwa ni kesi ya kipekee kwa mshitakiwa kufikishwa mahakamani bila kuchukuliwa maelezo yake.
Aliendelea kudai kuwa katika hali hiyo, Zombe hastahili kuwa mshitakiwa bali shahidi kwenye kesi hiyo. Aliongeza kuwa Zombe hakuwahi kuwaona wafanyabiashara kabla ya kuuawa na hata walipouawa hakuwahi kuona miili yao, hivyo akahoji iweje adaiwe kushiriki kwenye mauaji hayo?
Kwa upande wake, Wakili Majura Magafu anayewatetea washitakiwa saba katika kesi hiyo, alidai kuwa kesi hiyo ni ya kupika yenye lengo la kuwaharibia washitakiwa kazi, maisha na vyeo vyao. Alijenga hoja hiyo kwa maelezo kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kuunga ushahidi wa mazingira unaowafanya washitakiwa wasimame mbele ya mahakama hiyo na wajitetee.
Magafu aliungana na Msemwa kudai kuwa upande wa mashitaka unatumia maelezo ya mshitakiwa wa 11 na 12 ambaye pia alitaka mahakama ikubali ushahidi wa washitakiwa hao. Alidai kuwa ushahidi wote ni wa kusikia, kwani hakuna hata shahidi aliyeshuhudia tukio hilo. Alidai kuwa mashahidi muhimu wa mashitaka si mashahidi wazuri, kwa vile walishuhudia tu kukamatwa kwa wafanyabiashara hao eneo la Sinza.
Magafu aliomba mahakama iangalie nani alihusika na mauaji ya watu hao, kwani hata upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha na kutaja waliohusika katika tukio hilo. "Mheshimiwa sisi na mahakama bado tuko gizani." Alidai kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kueleza idadi ya askari waliokuwa katika tukio la mauaji. Alidai hata mpelelezi mkuu wa shauri hilo, alikiri kuwapo askari wengi kwenye tukio hilo.
Alidai kuwa mpelelezi huyo alionyesha kushangaa sababu ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuamuru askari wengine wasifikishwe mahakamani. "Kama hakukuwa na majungu kwa nini askari hao waachwe wakati wanajulikana? Alihoji Magafu na kuongeza: "Hii inaleta shaka, hivi ni kweli walioko hapa ndio waliohusika au walioachwa ndio walihusika na mauaji hayo?
"Tunaweza kusema kuwa walioletwa hapa mahakamani hawakuhusika na mauaji hayo, ila wametolewa kama kafara kwa matakwa ya wakubwa," alidai Magafu. Alidai baadhi ya wateja wake siku ya tukio walikuwa wamepangiwa kulinda kwenye tukio la dini na wengine waliokwenda kuwakamata washitakiwa, hawakuwa na silaha.
Aliongeza kuwa askari wa Chuo Kikuu (UDSM) walikuwa na silaha, ila zilirudishwa bila hata risasi moja kutumika. Wakili huyo alidai kuwa upande wa mashitaka baada ya kukosa ushahidi, ukaamua kutumia maelezo ya washitakiwa wa 11 na 12 ambao baada ya tukio hilo, walikuwa mafichoni hadi Machi 2006. "Je huu si ushahidi wa kupikwa?
Ni matumaini yetu kuwa ni ushahidi wa kupikwa," alidai Magafu na kutoa mfano wa mashahidi wa 25 na 26 ambao walikiri kuwa ndio waliofanya ujambazi wa BIDCO, lakini hawakukamatwa na kufikishwa mahakamani. Magafu katika hoja yake pia alidai kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kueleza ni eneo lipi mauaji hayo yalifanyika.
Alidai kuwa baadhi ya mashahidi wanadai ni Sinza lakini wengine wanadai ni katika msitu wa Pande. Aliongeza kuwa ni wajibu wa upande wa mashitaka kuondoa utata huo na shaka juu ya eneo ambako mauaji yalitokea. Alidai kuwa mahakama haiwezi kuwahukumu watu kwa hisia bali kwa ushahidi mzito ambao ungetolewa na upande wa mashitaka.
"Baadhi ya mashahidi wanadai pale Sinza kulikuwa na mapigano wengine wanasema hayakuwapo, sasa washitakiwa wajitetee juu ya lipi? Bado kuna utata na ushahidi wote ni wa kusikia," alidai Magafu. Aliendelea kudai kuwa kwa vile upande wa mashitaka hauwezi kupata dawa ya utata huo, washitakiwa hawana haja ya kupanda kizimbani kujitetea.
Naye Wakili Gaudence Ishengoma anayemtetea Bageni, alidai kuwa ushahidi dhidi ya mteja wake ni dhaifu na ambao umeshindwa kumuunganisha mteja wake na kosa la mauaji. Alidai kuwa mashahidi wa upande wa mashitaka wameshindwa kuthibitisha kuwa ni kweli polisi waliwaua watu hao kwa uroho wa fedha.
Pia alidai kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kueleza kuwa bastola aliyokuwa nayo mmoja wa waliouawa alikuwa anaimiliki kihalali au la, ili kujiridhisha kuwa watu hao hawakuwa majambazi kama inavyodaiwa na upande wa mashitaka. Wakili huyo alidai kati ya mashahidi 37 hakuna hata mmoja aliyethibitisha kumwona Bageni akisimamia mauaji hayo katika msitu wa Pande.
Alidai kuwa badala yake, upande wa mashitaka unatumia maelezo ya washitakiwa wa 11 na 12 kutaka kumtia hatiani mteja wake. Pia aliiomba Mahakama ikatae ushahidi wa washitakiwa hao kwa vile maelezo yao ni ya uzushi na hayaelezi kwa kina kama Bageni ndiye aliyesimamia mauaji hayo katika msitu wa Pande.
Lakini pia aliitaka Mahakama ikatae ushahidi uliotolewa na Feleshi ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai (DPP), kwa vile alitoa ushahidi huo unaomhusisha mteja wake na tukio hilo baada ya kusoma majalada yakiwamo maelezo ya washitakiwa wa 11 na 12.
Katika kesi hiyo, Zombe na wenzake wanashitakiwa kwa mauaji ya wafanyabiashara Ephrahim Chigumbi, Sabinus Chigumbi ‘Jongo', Mathias Lunkombe na Juma Ndugu, ambaye alikuwa dereva wa teksi iliyokuwa ikitumiwa na wafanyabiashara hao katika shughuli zao
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo namba 26/2006 ni Mrakibu wa Polisi Bageni, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Ahmed Makele, F. 5912 Konstebo Noel Leonard, WP. 4593 Konstebo Jane Andrew, D. 6440 Koplo Nyangelera Moris na D. 1406 Koplo Emmanuel Mabula.
Washitakiwa wengine ni E. 6712 Koplo Felic Sandsy Cedrick, D. 8289 Konstebo Michael Shonza, D. 2300 Koplo Abeneth Saro, D 9321 D/C. Rashid Lema, D. 4656 D/Koplo Rajab Bakari na D. 1367 D/Koplo Festus Gwabisabi. Baada ya upande wa utetezi kumaliza kutoa hoja zao za utetezi, upande wa mashitaka utajibu hoja hizo kabla ya Jaji Salum Masati kutoa uamuzi kutokana na hoja hizo.