SoC02 Utoaji wa dawa na vifaa tiba hospitalini kwa utaratibu wa OTT

SoC02 Utoaji wa dawa na vifaa tiba hospitalini kwa utaratibu wa OTT

Stories of Change - 2022 Competition

eam6476

New Member
Joined
Aug 24, 2021
Posts
2
Reaction score
1
Dawa na vifaa tiba ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha utoaji wa huduma bora za afya kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini na kuhakikisha kuwa jamii inakuwa na afya bora. Pamoja na umuhimu huo, sekta ya afya imekuwa na changamoto ya uhaba wa dawa na vifaa tiba. Hii inapelekea ugumu wa utoaji wa huduma bora za afya kwa wagonjwa hususani waliolazwa wodini, licha ya kuwa serikali imeongeza bajeti yake katika wizara ya afya kwa lengo la kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana.

Naipongeza serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya kwa jitihada mbalimbali zinazofanywa kuhakikisha kuna uwepo wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya licha ya changamoto ya ugonjwa wa virusi vya UVIKO-19. Hivyo kutokana na changamoto zilizopo za uhaba wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya, ni vyema tukaanza kufikiria njia nzuri zaidi ya kuzitumia rasilimali zilizopo ili kuhakikisha tunaokoa maisha ya ndugu zetu wagonjwa waliopo hospitalini. Moja ya njia hizi ni utoaji wa dawa na vifaa tiba kwa utaratibu wa OTT.

Kirefu cha OTT ni “One Time Taking”. Huu ni utaratibu ambao dawa na vifaa tiba hutolewa kwa mara moja na kwa siku husika. Utaratibu huu wa OTT utamsaidia mgonjwa kupata dawa zake za siku hiyo atakazokuwa ameandikiwa na daktari wodini na kwa wakati unaofaa. Pia utaratibu huu utawasaidia wauguzi kutoa huduma kwa wakati na kwa ufanisi zaidi kwa wagonjwa kwa kuwa utawawezesha kupata vifaa tiba vinavyohitajika kuwahudumia wagonjwa waliolazwa wodini.

Utaratibu huu wa OTT una faida mbalimbali kwa wagonjwa, kwa wahudumu wa afya hospitalini na kwa serikali kwa ujumla. Hizi ni faida kadhaa za kututumia utaratibu wa OTT.

Utapunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini. Mara nyingi wagonjwa waliolazwa wanakabiliwa na gharama kubwa za matibabu katika vituo ya afya. Sehemu kubwa ya gharama hizo ni gharama za dawa na vifaa tiba wanavyovitumia wanapokuwa wakiuguzwa. Kwa kutumia utaratibu wa OTT, utapunguza gharama za matibabu zinazotokana na dawa na vifaa tiba kwa sababu mgonjwa atapatiwa dawa na atahudumiwa kwa vifaa tiba sawa na idadi ya siku atakazokuwa amelazwa hospitalini.

Utaratibu wa OTT utamsaidia mgonjwa kupata dawa alizoandikiwa na daktari na muda sahihi wa kupatiwa hizo dawa. Yaani dawa za kutumia asubuhi, mchana, jioni na usiku. Hivyo mgonjwa atalipia gharama za idadi ya vidonge au dawa za sindano atakazokuwa ametumia kwa siku husika na hiyo kumfanya awe na weledi wa gharama za matibabu anazozilipia.

Utapunguza mlundikano wa dawa na vifaa tiba wodini. Utaratibu wa OTT utapunguza mlundikano wa dawa na vifaa tiba visivyokuwa na matumizi wodini na hiyo kufanya mazingira ya kufanyia kazi kwa wauguzi waliopo wodini kuwa mazingira safi, salama na rafiki kwa kuwa watakuwa wanapatiwa vifaa tiba vinayohitajika kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa kwa hiyo siku moja husika.

Hii pia itasaidia kuhakikisha matumizi sahihi ya malighafi zilizo duni kwa mfano mipira ya mikono yaani ‘gloves’ na vifaa vingine vingi. Hii pia itawasaidia wauguzi kuweka rekodi sahihi ya vifaa tiba pamoja na makadirio sahihi ya vifaa tiba vilivyotumika kwa mgonjwa husika wakati wa kufunga mahesabu ya gharama za matibabu za wagonjwa baada ya kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Utaratibu wa OTT utasaidia sana katika kupunguza upotevu wa dawa wodini. Upotevu wa dawa wodini hutokea wakati ambapo mgonjwa amefariki au mgonjwa alikuwa akitumia dawa fulani na kabla hajamaliza kutumia dawa hizo, ikamlazimu daktari kumbadilishia dawa kutokana na sababu mbalimbali za kitabibu. Kwa hivyo vile vidonge vilivyobaki alivyokuwa akivituia mgonjwa hapo awali, vinakuwa havina matumizi tena kwa sababu daktari amebadilishia dawa. Lakini zile dawa zilizobaki bado pia ni rasilimali ambayo ikitunzwa itaweza kumsaidia mgonjwa mwingine na kumtibu hususani kwa dawa za vidonge.

Utasaidia ufuatiliaji wa karibu wa madhara yatokanayo na matumizi ya dawa ‘Adverse Drug Reaction’ kwa wagonjwa. Hili ni jukumu muhimu hasa kwa wafamasia ili kuweza kuisaidia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba ‘TMDA’ kuifuatilia dawa husika kwa ukaribu kulingana na madhara yatakayokuwa yametolewa ripoti kuhusu matumizi ya dawa husika kwa wagonjwa.

Utaratibu wa OTT utawasaidia sana wafamasia kufahamu na kuchunguza zaidi madhara yatokanayo na matumizi ya dawa na kuweza kuzuia na kutibu madhara yatokanayo na matuizi ya dawa hizo kwa wagonjwa. Hili litawezekana kwa sababu mgonjwa atapatiwa dawa moja baada ya nyingine kwa nyakati tofauti na hivyo itawezesha kufahamu ni wakati gani amepata madhara kutokana na dawa alizopewa na kuweza kutoa taarifa kwa TMDA kwa kutumia fomu ya njano.

Utawasogeza wafamasia karibu na wahudumu wengine wa afya katika utoaji wa huduma za afya kwa wagonjwa. OTT itamfanya mfamasia awe karibu na madaktari na wauguzi wakati wa kuwaona wagonjwa wodini na kuweza kushauriana katika matibabu ya mgonjwa husika. Hii pia itamsaidia mfamasia kuongeza maarifa zaidi kutoka kwa wataalamu wengine wa afya kama madaktari bingwa na wauguzi na kuongeza wigo wa wanataaluma bobezi katika kada ya Famasia.

Pia kwa uwepo wa mfamasia wodini itawasaidia madaktari kufahamu dawa zilizopo kwenye kituo husika na kuepusha gharama za ziada za matibabu kwa mgonjwa kuandikiwa dawa ambayo haipo katika kituo anachotibiwa. Pia kwa uwepo wa wafamasia wodini utakuza matumizi sahihi ya dawa za vijiua sumu ‘Antibiotics’ na kuzuia usugu wa dawa utokanao na matumizi yasiyo sahihi ya dawa za Antibiotics.

Utaongeza nafasi za ajira kwa wafamasia: Utaratibu wa OTT utaiwezesha serikali kupitia wizara ya afya pamoja na hospitali za umma na binafsi kuongeza nafasi za ajira kwa wafamasia na pia kusogeza huduma za kifamasia karibu zaidi na wagonjwa. Hii itapunguza dhana potofu kuwa wafamasia ni watu wa kukaa dirishani na kugawa dawa au wezi wa dawa.

Hii ni kwa sababu huduma za wafamasia na umahiri wao utaonekana zaidi pale wanapowahudumia wagonjwa hosptalini katika wodi walizolazwa. Hivyo kutakuwa na wafamasia wengi zaidi watakaokuwa wanahudumia wagonjwa kwa kuwapatia dawa sahihi kwa matumizi na kwa wakati sahihi kwa utaratibu wa OTT, pamoja na kufuatilia kwa ukaribu zaidi maendeleo yao na kuzuia madhara yatokanayo na dawa.

Imeandaliwa na:

ERICK A. MINJA.

Mfamasia.

Email: minjaerick7@gmail.com
 
Upvote 0
Back
Top Bottom