Utoaji wa elimu bila malipo uendane na uboreshaji wa stahiki za watumishi ili kuhakikisha elimu bora

Utoaji wa elimu bila malipo uendane na uboreshaji wa stahiki za watumishi ili kuhakikisha elimu bora

DolphinT

JF-Expert Member
Joined
Mar 9, 2016
Posts
2,014
Reaction score
2,979
Nitumie ukurasa huu kuipongeza serikali ya awamu ya tano katika suala zima la kuendelea kupambana na umaskini kwa kujikita katika kujenga Tanzania ya viwanda ambapo kwa matarajio makubwa ni dhahiri kwamba siku za mbeleni suala la ukosefu wa ajira kwa kiasi kikubwa litakua limepungua. Hii inatokana na ukweli kwamba uwekezaji katika viwanda hupanua fursa za kiuchumi katika biashara na kilimo pamoja na ajira za kudumu na za muda mfupi.

Hali kadhalika niipongeze serikali kwa juhudi inazofanya katika suala la kupambana na ujinga kwa kuhakikisha kuwa watanzania wanaotakiwa kupata elimu wanaipata. Hii ni dhamira nzuri inayotekelezwa chini ya mpango wa elimu bila malipo katika shule za umma kuanzia elimu ya awali mpaka kidato cha nne. Ni kiu yangu kuona kwamba elimu inatolewa kama huduma muhimu na sio bidhaa. Kwa kuwa Rais wetu amekua akitueleza kuwa nchi yetu ni tajiri na ina rasilimali za kutosha ni vyema serikali yetu ikawekeza katika sio tu elimu ya sekondari mwisho kidato cha nne bali hata ngazi ya vyuo vikuu vya umma ambavyo ni kimbilio kubwa la Watanzania walio wengi.

Nchi zote zilizopiga hatua katika maendeleo zilihakikisha kwamba pamoja na mambo mengine watu wake wanapata elimu ya kutosha, bora, sawia na yenye kuendana na vipaumbele vya taifa katika maswala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Ni wakati sasa kwa Tanzania yetu kujenga mfumo imara zaidi wa elimu ambao kwa namna moja au nyingine itazifanya shule zetu za umma kuwa kimbilio la watanzania walio wengi huku wakiziamini na kutambua kwamba huko ndiko kunakotolewa elimu iliyo bora. Kwakua Rais wetu amejipambanua kuwa yeye ni mtetezi wa wanyonge ni dhahiri kwamba watanzania walio wengi ni wa kipato cha chini na hivyo hawana uwezo wa kupeleka wanafunzi wao katika shule tunazoamini kuwa ni bora na zitoa elimu bora.

Hali kadhalika watumishi katika wizara ya elimu hasa waalimu wa shule za sekondari na msingi katika shule za umma ni watu waliokata tamaa ukilinganisha na idara au wizara nyingine. Hii ni kutokana na taaluma ya ualimu kuonekana ni taaluma ya watu walioshindwa katika Nyanja zaote za maisha na kuamua kufanya ualimu kuwa chaguo lao la mwisho. Mtazamo huu katika jamii unaakisiwa na aina ya maisha wanayoishi ambayo hata hayalingani na elimu zao. Umefika wakati sasa serikali kuijengea heshima taaluma ya ualimu ili iheshimike na kuchukuliwa kwa mtazamo chanya na jamii kwa ujumla.

Mishahara wanayolipwa kwa kiasi kikubwa na midogo na haiwewazeshi kukidhi mahitaji yao ya msingi na ya kimaendeleo. Suala la nyongeza ya mishahara hata linapokuwa kisheria limeonekana kama ni hisani kutoka serikalini, Walimu hawapandiswhi madaraja kwa wakati na hivyo kijikuta haki zao zinapotea bila maelezo ya kueleweka. Katika vyuo vingi hapa Tanzania fani ya elimu inaonekana kuwa na wahitimu wengi Zaidi kuliko kada nyingine; kwakuwa wanafunzi wengi hutegemea bodi ya mikopo ni dhahiri kwamba walimu wengi walipunguzwa mishara yao kwa kipindi cha mwaka 2015/2016 kwani sheria mpya ya bodi ya mikopo ilifanya kazi kurudi nyuma badala ya kuanzia pale iliposainiwa kwenda mbele. Yaani kutoka asilimia nane ya mshahara kama ilivyokua katika mkataba mpaka asilimia kumi na tano kwa wanufaika wote. Suala hili limesababisha athari kubwa sana kwa watumishi hasa waalimu.

Stahili za likizo pamoja na malimbikizo ya mishahara pamoja na madai mbalimbali kutokulipwa kwa wakati imikua pia ni changamoto kubwa kwa tasnia ya ualimu sanjari na urasimu katika kuhama au kubadilisha vituo vya kazi hasa pale walimu wanapohitaji kujumuika na familia zao.

Mafunzo kazini pia imekua ni changamoto kubwa hasa kwa walimu ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia ulimwenguni kote. Ni ajabu sana kumkuta mwalimu aliyehudumu kwa takribani miaka mitano au kumi bila kupata mafunzo yoyote juu ya uboresha wa njia za kujifunza na kufundisha wanafunzi ili kuhakikisha kuwa wanapata elimu bora.

Suala la makazi au nyumba za walimu limekua bado ni tatizo kubwa katika kada ya elimu; ingawa serikali inajitahidi kuchukua hatua kukabiliana nalo lakini upepo umeelekea upande mmoja kwa kiasi kikubwa kwa mana ya kwamba nguvu kubwa imeelekezwa katika ujenzi wa vyumba vya madarasa na kutatua changamoto za madawati na kusahau kwamba wanafunzi hawa wanahitaji pia waalimu kwa ajili ya kuwafundisha ambao pia wanakaa katika makazi bora,

Wito wangu kwa serikali na watunga sera wetu; Linapokuja suala la elimu ni vyema mfumo mzima wa utoaji wa elimu pamoja na rasilimali watu wake wakahusika au kuhusishwa tena kwa utafiti yakinifu unaohusisha makundi yote. Katika bajeti ya serikali ya kugharimia elimu bila malipo ni vyema suala la motisha, maslahi na mahitaji ya walimu yakazingatiwa pia ili kuhakikisha kuwa watu hawa wanafanya kazi kwa utulivu na kuhakikisha kuwa vijana wetu wanapata elimu bora na sio bora elimu.

Mamlaka ya udhibiti ubora wa elimu; badala tu ya kukagua masuala yanayohusu ufundishaji na ujifunzaji na kutoa taarifa ni vyema pia wakahusika katika kuzisikiliza changamoto zinazowakabili watumishi wa idara hii ili kwa akushirikiana na serikali ziweze kutatuliwa kwa haraka, hii huongeza ari ya watumishi kufanya kazi kwa kujituma Zaidi.

Nihitimishe kwa kuandika kwamba maendeleo shirikishi pia ni jambo la muhimu kama sio la lazima. Katika maeneo ya nchi ambayo huduma za elimu ni hafifu ni vyema serikali kuu kupitia serikali za mitaa kuwashirikisha wananchi ili wahusuike katika kujenga miundombinu rafiki kwa ajili ya watumishi wa elimu hasa waalimu badala ya kutegemea tu serikali. Lengo kubwa ni kuhakikisha kuwa thamani ya fedha inayotolewa na serikali katika kugharimia elimu inaonekana baada ya muda fulani. Ni jambo la kuishangaza sana fedha za walipa kodi zinapotumika kugharimia elimu ambapo matokeo yatokanayo hayaakisi thamani ya fedha iliyowekezwa. Ifike mahala elimu bila malipo kutoka kwa wazazi au wananchi itafsiriwe kama uwekezaji mkubwa unaofanywa na taifa, Fedha hizi zioneshe matokeo chanya katika matokeo ya mitihani na mwisho wa siku wataalamu watakanao na elimu hii sanjari na kuondokana na taifa tegemezi katika Nyanja zote ambao naamini watatoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya Tanzania ya viawanda.

Ni matumaini yangu makubwa tamko ka Mheshimiwa Rais alipohutubia walimu Dodoma litatekelezwa kwa haraka ili kuzitatua changamoto hizi zinazoikabili elimu yetu.

(angalizo: makala hii niliandika kwa mara ya kwanza katika gazeti moja la kila siku na pia katika ukuraza wa facebook)​
 
Back
Top Bottom