SoC03 Uwajibikaji ni maisha yetu

SoC03 Uwajibikaji ni maisha yetu

Stories of Change - 2023 Competition

Irecondrito

New Member
Joined
Jul 23, 2023
Posts
1
Reaction score
0
Uwajibikaji ni ile hali ya kukubali majukumu kwa ukweli, uwazi na kuzingatia maadili kwa ajili ya wengine.

Uwajibikaji ni dhana pana, ikianza na mtu mmoja mmoja hadi kufikia jamii nzima. Ni kitu bora, ni jambo la kujivunia, kila mtu inabidi apende na aishi akijua maisha yake yeye yanaamuliwa na yeye mwenyewe kwa kuwajibika ipasavyo. Uwajibikaji haupendi lawama na kunyoosheana vidole bali unataka matokeo. Uwajibikaji ni tunu na ni urithi ambao inabidi turithishe kizazi na kizazi, tuwaeleze kwamba uwajibikaji ni maisha yetu na inabidi wayaishi.

Jamii/taasisi iliyojengwa katika misingi ya uwajibikaji, nidhamu, ustadi, na taaluma huwa ni vipaumbele vya kila mmoja katika utekelezaji wa majukumu yao, ila jamii ambayo haina misingi ya uwajibikaji, majungu, lawama, unafki, na migogoro huwa ni sehemu ya maisha yao ya kila siku.

Nikipita mitaa mbalimbali katika majiji yetu imejaa kila aina ya uchafu na uvundo. Ukiuliza wakaaji kwa nini kuna adha hii ya uchafu wa mazingira, wote wataelekeza lawama sehemu zingine, ama serikali ama taasisi flani. Wanasahau kwamba na wao ni sehemu ya ule uchafu, na wao wanachangia pakubwa maeneo yao kuwa kama yalivyo, na wana uwezo wa kubadili historia hiyo ya uchafu na uvundo kwa kufanya maamuzi sahihi ya "uwajibikaji."

Mkulima, mwalimu, mwanafunzi, daktari, mwanasiasa, mfanyabiashara, n.k., wote hawa wanajukumu la kuhakikisha wanawajibika katika nafasi zao kwa ustawi wa jamii yetu na taifa letu. Inabidi kila mtu kwa nafasi yake afanye maamuzi ya kuwajibika ipasavyo kwa kujenga jamii bora. Uwajibikaji inabidi uwe maisha yetu, uwajibikaji na maendeleo vinashabihiana. Maendeleo ya sehemu yoyote ni lazima maamuzi yafanyike kwa kila mmoja kuwajibika kwa nafasi yake.

Kila mmoja wetu akiwajibika kwa nafasi yake inapunguza uwezekano wa kukwazana makazini na katika ngazi mbalimbali katika maisha yetu. Pale mtu anapoaminiwa na kupewa majukumu na hayatekelezi ipasavyo inaleta migongano ndani ya jamii na kuwaumiza wengine. Uwajibikaji unaongeza furaha, mshikamano, kuaminiana, na kuongeza kasi ya maendeleo.

Kwa mtazamo wangu, uwajibikaji tunaweza kuuweka katika ngazi tatu kama ifuatavyo:

  1. Ngazi ya mtu binafsi:Hapa inahusisha utekelezaji kwa ukamilifu wa yale majukumu kwa ngazi ya mtu binafsi. Uwajibikaji kwa ngazi hii ni pamoja na kujali hisia za watu wengine na kuwa mkweli. Kama wewe ni mzazi, basi hakikisha unatoshea vema kwenye nafasi ya uzazi kwa kuchukua vema majukumu yako. Jamii/taifa hujengwa na muunganiko wa jamii za watu waliotoka kwenye familia mbalimbali. Hivyo kila mtu ana nafasi kubwa sana katika kujenga jamii bora endapo atachukua vema majukumu yake na kuyatekeleza kama inavyopasa. Kwa hapa, ni muhimu kuhakikisha tunakuza watoto katika njia bora, kuweka mikakati ya malezi bora ili kuzalisha taifa bora lenye misingi imara kuanzia ngazi ya familia. Tunu na misingi ya jamii yoyote ile hujengwa ndani ya familia zetu, hivyo hata uwajibikaji unajengwa katika familia zetu kwa watoto kujifunza kwa vitendo kupitia kwa wazazi na jamii inayomzunguka. Kwa muktadha huo, ni vema jamii ikazalisha watu wengi ambao watakua ni kioo na mfano wa kuigwa kwa watoto.
Zipo nukuu kadhaa zinazolenga uwajibikaji katika ngazi ya mtu binafsi:

  • Jeffery Gitomer anasema, "Kulaumu wengine kwa matatizo yetu ni kama, ni kama kuilamu donate kwa kuwa na amfuta huku tukisahau kwamba tatizo si donate tatizo ni maamuzi ya mtengenezaji."
  • George Washington Carver anasema, "Asilimia tisini na tisa ya kushindwa kwetu hutokana na kulaumu wengine badala ya sisi wenyewe."
  • Saidi Mdala anasema, "Kitu hatarishi kwa vijana ni kutokubali kukua na kutegemea wengine katika utatuzi wa changamoto zao."
  • Shelby Martin anasema, "Uwajibikaji binafsi unahitaji busara, kukubali, ukweli na udhubutu."

Ngazi ya jamii

Jamii ni muunganiko wa watu wanaoishi eneo moja. Katika jamii kuna watu wa aina tofauti na wenye tabia na mitazamo tofauti. Ni jukumu la jamii kukaa kwa pamoja katika amani na maridhiano pamoja na utofauti uliopo baina yao. Jamii isipowajibika ipasavyo katika kusimamia misingi waliojiwekea huweza kuleta mitafaruku na migongano baina yao. Kwa hiyo jukumu la jamii ni kuwajibika katika kuibua uovu unaotendeka katika jamii. Kwa kuibua viongozi ambao si waadilifu, kwa kuibua wananchi ambao hawana siha njema waharibifu wa mazingira na wavunjifu wa amani ni jukumu la jamii kuwaibua na kuhakikisha wanafikishwa katika vyombo vya kisheria.

Ngazi ya serikali

Serikali yoyote ipo kwa ajili ya kutetea maslahi ya wanachi wake, ipo katika kuhakikisha wanachi wake wanapata stahiki zao na wanafanya kazi zao katika mazingira rafiki na yenye amani. Serekali iliyoshindwa kuwajibika kwa wananchi wake haifai kuwepo madarakani, wanachi inabidi wajue kwamba wanao wajibu wa kuihoji na kuiwajibisha serikali pale inapoenda nje na matakwa yao. Katika nchi yoyote yenye demokrasia wenye mamlaka ni wanachi. Serikali inabidi itimize wajibu wake kwa wananchi na wananchi hivyo hivyo inabidi watimize wajibu wao kwa serikali yao.


Jinsi gani tunaweza kuongeza uwajibikaji kwa ngazi zote

Kuweka uwazi katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali

Kujenga jamii yenye maadili bora yenye kujali utu

Ugatuzi wa madaraka kwa kuwapa wananchi mamlaka ya kuwawajibisha viongozi wao

Tukumbuke tu kwamba uwajibikaji ni kiungo muhimu sana katika maendeleo yoyote, tunapokubali uwajibikaji tunajiweka katika mazingira ya sisi kubadilika ili kuendana na kile tunachokiendea.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom