SoC02 Uwajibikaji

SoC02 Uwajibikaji

Stories of Change - 2022 Competition

PENIELSJ

New Member
Joined
Sep 14, 2022
Posts
1
Reaction score
1
UWAJIBIKAJI

Uwajibikaji ni hali ya mtu kuyakabili majukumu yake ipasavyo bila kusukumwa, kuwajibika pia nia hali ya mtu kutimiza vilivyo majukumu alionayo. Uwajibikaji umegawanyika katika nyanja mbalimbali, nyanja hizo ni kijamii, kisiasa, na kiuchumi. Kila mtu katika jamii anawajibu ambao anatakiwa kuutimiza kwa nafasi yake, wajibu hutofautiana kutoka mtu mmoja na mtu mwingine, kwa kuzingatia nafasi ya mtu huyo katika jamii husika na umri wake.

Uwajibikaji unaanzia ngazi ya familia kwa mwanafamilia mmoja mmoja, jamii na hatimaye taifa zima. Ili kujenga jamii bora yenye mifumo imara ya maisha na maendeleo katika nyanja zote za maisha ni lazima kila mmoja katika jamii husika kuwajibika ipasavyo. Uwajibikaji unafaida nyingi katika jamii zetu vivyo hivyo kutokuwajibika kuna madhara makubwa katika jamii zetu. Zifuatazo ni faida za uwajibikaji na hasara za kutokuwajibika.

Uwajibikaji humsaidia mtu kutimiza malengo yake kwa wakati. Mtu anayewajibika ni dhahiri kwamba atafanya kazi kwa bidii na nidhamu ya hali ya juu ili kufikia maono aliyonayo kwa wakati muafaka, hivyo kuishi maisha ya ndoto zake. Mtu asiyewajibika hawezi kufikia malengo yake kwa kukosa bidii, uwajibikaji na nidhamu ya kazi mtu huyu huishia kupanga malengo lakini hushindwa kutimiza malengo hayo.

Pia uwajibikaji huchochea maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla. Kuwajibika humuwezesha mtu kujikimu mahitaji yake ya msingi kama: chakula, malazi, mavazi na mahitaji mengine ya ziada kama elimu, mawasiliano na usafiri ambayo nayo ni muhimu kwa maisha ya mwanadamu. Kuwajibika pia kunawezesha mtu kuwahudumia watu wanao mtegemea kwa kuwapatia maitaji yao muhimu, mfano mtu aliyeajiriwa serikalini au katika sekta binafsi anapowajibika ipasavyo atajipatia kipato kupitia mshahara na atalipa kodi inayo wezesha shughuli mbalimbali za maendeleo ya taifa. Kutokuwajibika kunakwamisha maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Uwajibikaji unasaidia kuokoa maisha ya watu. Yapo makundi ya watu mbalimbali ambayo kwa mujibu wa majukumu yao wanagusa maisha ya watu moja kwa moja, mfano madaktari wanapotimiza majukumu yao ipasavyo wataokoa maisha ya watu dhidi ya vifo vinavyoweza kuzuilika. Vivyo hivyo kwa madereva na askari wa barabarani wanapowajibika wanaokoa maisha ya maelfu ya watu dhidi ya ajali zinazoweza kuzuilika. Kutokuwajibika kwa makundi haya husababisha watu wengi kupoteza maisha hii pia inaathiri nguvu kazi ya taifa.

Uwajibikaji unasaidia kulinda haki za binadamu katika makundi tofauti tofauti, haki za msingi za binadamu ni pamoja na haki ya kuishi, kuheshimiwa, uhuru wa kuabudu na kuwa na kinga kisheria dhidi ya uonevu wa aina yoyete. Kuwajibika kunasaidia serikali kupitia vyombo vya dola kama mahakama, asasi za kiraia na jamii kwa ujumla kulinda haki za binadamu, mfano katika ngazi ya familia wazazi wana haki ya kulinda haki za watoto ambazo ni: haki ya kuishi, haki ya kulindwa, haki ya kushiriki, haki ya kuendelezwa na haki ya kutokubaguliwa (www.sematanzania.org). Haki za binadamu zinapolindwa huchochea ustawi wa taifa na haki hizi zisipolindwa hupelekea kupoteza maisha, uonevu chuki na visasi ambavyo huathiri ushiriki wa watu katika ujenzi wa taifa.

Uwajibikaji hupunguza mmomonyoko wa maadili au vitendo viovu katika jamii, mfano wa vitendo viovu ni: ubadhirifu wa mali za umma, rushwa, uuzaji wa madawa ya kulevya, biashara ya ngono na wizi. Watu wengi wanojihusisha na vitendo hivi viovu ni watu ambao wameshindwa kuyakabili majukumu yao kikamilifu hivyo huamua kutafuta njia za haraka za kujipatia mafanikio kwa njia hizo zisizo rasmi. Jamii zetu zinazokabiliwa na changamoto kubwa ya watu kutamani mafanikio ya haraka na wengi wao kutokuwa tayari kuvumilia mchakato wa kupata mafanikio halali hivyo wameishia kujihusisha na vitendo viovu ili kujipatia mafanikio ya haraka.

Uwajibikaji unalinda utu wa mtu, jamii inaheshimu na kuthamini mchango wa mtu mwajibikaji katika kuyatekeleza majukumu yake kwa ustawi wake binafsi na ustawi wa jamii. Hivyo ni muhimu kwa watu wote kuwajibika ili kulinda hadhi na utu wetu katika jamii zetu. Mtu asiyewajibika hujishushia heshima yake kwa jamii inayo mzunguka, jamii humchukulia mtu huyu kuwa ni mtu asiye jitambua na mzembe, mfano, mzazi au mlezi hutarajiwa kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuhudumia watoto wake au familia yake kushindwa kufanya hivyo heshima yake katika jamii hushuka.

Uwajibikaji unaimarisha mahusiano mazuri baina ya wanajamii katika jamii husika. Watu katika jamii wanapowajibika au wanapokuwa katika shuguli zao za kila siku hukutana wakati wengine hufanya kazi pamoja katika maeneo mbalimbali, hii huboresha mahusiano mazuri baina yao kama wanajamii pia hujifunza umuhimu wa ushirikiano, uchapakazi (bidii) na uadilifu kutoka kwa wengine. Mfano kupitia shuguli mbalimbali wanazofanya watu wameanzisha mifuko ya kijamii katika maeneo yao ya kazi yenye lengo la kusaidiana katika matukio ya huzuni na furaha, wanajamii wengi kupitia mifuko hii wameendelea kunufaika na kushirikiana hivyo kuwa na mahusiano bora kijamii. Kutokuwajibika kunaathiri mahusiano ya wanajamii hii hupelekea kuzorota kwa maendeleo ya jamii husika.

Uwajibikaji unaboresha misingi ya utawala bora. Viongozi bora ni wale wanaotekeleza majukumu yao kwa kuzingatia utawala wa sheria, demokrasia, uwajibikaji na uwazi ambao ni nyenzo muhimu za utawala bora kwa ustawi wa taifa. (www.policyforum-tz.org). Mfano kiongozi anapo tekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kufuata misingi ya utawala bora ni dhahiri kuwa kutakuwa na matumizi sahihi ya dola na kutambua mipaka ya madaraka kulingana na katiba ya taifa husika, hivyo kuchochea ustawi wa taifa kwa ujumla. Kiongozi asiye wajibika hazingatii utawala wa sheria hali ambayo hupelekea kuwepo na changamoto nyingi za kiutawala, mfano matumizi mabaya ya madaraka na mali za umma, rushwa na ukiukwaji wa haki za binadamu hii husababisha machafuko ya kisiasa ambayo huathiri ustawi wa wananchi na taifa.

Kwa kuhitimisha uwajibikaji ni muhimu sana kwa ustawi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Jamii inapaswa kusisitiza uwajibikaji kuanzia ngazi ya familia kwa kila mwanafamilia kwa nafasi yake, wanajamii na taifa zima ili kuleta maendeleo. Vilevile jamii inapaswa kukemea kutokuwajibika katika makundi mbalimbali ya wanajamii kujenga misingi imara ya uwajibikaji, ili kuwa jamii na taifa lenye misingi bora ya maadili mema katika nyanja zote za maisha.
 

Attachments

Upvote 2
Back
Top Bottom