SoC04 Uwanja wa michezo tambarare: Pedali za kuifikia Tanzania tuitakayo

SoC04 Uwanja wa michezo tambarare: Pedali za kuifikia Tanzania tuitakayo

Tanzania Tuitakayo competition threads

i_denyc

New Member
Joined
Jun 6, 2023
Posts
4
Reaction score
8
UTANGULIZI
Wengi tunajua uwanja wa michezo ni eneo la uwazi, na mara nyingi huwa tambarare. Mashindano tofauti hufanyika, kama vile mchezo wa mpira wa miguu, mpira wa kikapu na hata mbio za riadha. Ni katika sehemu hii wachezaji hunadi ujuzi na uwezo unaoweza kuwafanya waibuke kidedea kwenye mchezo wanaoshindania. Matokeo ya michezo huwa ni ya aina tatu yaani, kuna kushinda, kushindwa na kwa nadra sana washindani hutoka suluhu. Lahasha! Huu sio aina ya uwanja wa michezo ninaolenga kukujuza ndugu msomaji. Karibu uwaze kuwazua ni uwanja gani ninaokujuza.

KIINI
Uwanja wetu unamteremko mkali kwa sasa hadi pale hatua stahiki zitakapo chukuliwa kuufanya tambarare. Katika uwanja huu kuna wachezaji wanacheza kupandisha mlima huku wengine wakicheza wakishuka mlima. Matokeo huwa ni ya aina mbili, kuna kushinda na kushindwa na wala hakujawahi kutokea suluhu. Kama ilivyo kwenye uwanja wa michezo ya kawaida, huu uwanja pia una aina mbalimbali ya michezo. Michezo michache iliyopo kwenye uwanja huu ni pamoja lakini sio tu na: Siasa, Elimu,Haki, Kazi na Ajira.

Siasa. Sheria na kanuni za mchezo huu zipo bayana lakini husimama kama pazia huku marefa hupenda kuwabeba mabingwa watetezi kwa kuwa ndio wenye nguvu zaidi, rasilimali, miundo imara na ushirikiano wa karibu na serikali ambayo inaweza kuwapa faida na uwezo wa kudumisha ushindi katika mchezo huu. Ili uwanja wa mchezo wa siasa uwe tambarare na kupata Tanzania tuitakayo ni muhimu kuzingatia mambo machache;-​
  • Usawa na Uwazi. Ni vyema kila mchezaji akawekewa mazingira wezeshi bila ubaguzi wala upendeleo. Mfano, sio mchezaji mmoja wa chama flani anaruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara huku mchezaji mwingine akikataliwa kwa madai ya uvunjifu wa amani. Uwazi kwenye karne hii unafikiwa hasa kwa njia ya mtandao na sioni sababu za kuzima Intaneti kipindi cha uchaguzi. Kama vipi tuige mfumo wa majirani zetu.​
  • Kutokomeza Ufisadi na Rushwa. Mchezo unapaswa kuwa safi na wenye kuaminika. Katika kuhakikisha hili mchezo unapaswa kuchezwa kwa maslahi ya umma na si kwa manufaa ya watu binafsi. Ufisadi na rushwa kwenye siasa husababisha kutokuwepo kwa haki katika kugawanya rasilimali za nchi, na hivyo kusababisha madhara kwa maendeleo ya jamii. Mfano, sio mchezaji mmoja wa chama flani chenye madaraka atumie fedha za umma kufanyia kampeni zake na kupotosha matokeo ya uchaguzi ilihali washindani wenzake wakiwa hawana bajeti shindani.​
  • Kuboresha Sheria na Kanuni za mchezo, Waswahili wanasema "Mwacha mila ni mtumwa". Kuna umuhimu wa kubadilika na kuboresha mifumo na taratibu zilizopitwa na wakati ili kukidhi mahitaji na changamoto za sasa. Katika uboreshaji huo sio tuu kuboresha majina ya Sheria husika kama tunavyoona danganya toto zinazoendelea saivi za kuboresha jina la sheria ili kuwapa uhuru marefa wa mchezo huu, bali tunataka kuboreshwa kwa utekelezwaji wa yaliyomo ndani ya sheria husika.​
Elimu. Jamii huunadi mchezo huu kama ufunguo wa maisha japo uwanja wake haupo tambarare. Nikiangalia tofauti iliopo kati ya wanafunzi wa "mabasi ya njano" na "kidumu na mfagio" ni kubwa sana. Natambua hatua kubwa tuliopiga katika kutoa elimu bure kwa shule za msingi hadi sekondari, lakini kutoa elimu bure iliopitwa na wakati mashuleni ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu (Kinjekitile Ngwale tutamsoma hadi lini?). Dunia inabadilika kila iitwapo leo na hivyo elimu inapaswa kubadilika ili kukidhi matakwa ya mabadiliko ya jamii lasivyo inakua bora elimu na sio elimu bora. Ni heri wananchi wakavuja jasho ili watoto wao wacheze mchezo huu kwa usawa na kwa manufaa yao ya baadae. Kuusawazisha mchezo huu na kuipata Tanzania tuitakayo ni muhimu kuzingatia haya;-​
  • Kuboreshwa kwa mtaala, Elimu yetu inahamasisha ukumbukaji na sio ufikiriajii. Dunia inashuhudia mapinduzi ya nne ya viwanda ikiwa bado mtaala wetu umeshikilia mfumo wa elimu ya mapinduzi ya kwanza ya viwanda. Kwa hali hii, kwakujua na kwa kukusudia tunaandaa watumwa wa baadae.​
  • Kuboreshwa kwa viwango vya kitaaluma, hivi inawezekanaje mwanafunzi anaepelekwa shule na "school bus" akapimwa ufaulu na yule anaetembea kilomita 10 kufika shule? mwanafunzi anaelipiwa “tuition” na yule anaemuona mwalimu mara mbili kwa muhula. Tukiliangalia hili tutajua mizani haina usawa. Albert Einstein alisema “Kila mtu ni mwerevu, lakini ukimpima samaki kwa uwezo wake wa kupanda mti ataishi maisha yake yote akiamini yeye ni mjinga”. Viwango vya kitaaluma visivyo na usawa huipa jamii hasara ya kupoteza nguvu kazi na vipaji vyenye tija.​
Haki. Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Ni muhimu kuheshimu na kutoa haki kwa kila mtu bila kujali hadhi au uwezo aliokuwa nao. Uwanja wa utoaji haki una mteremko mkali sana, hivyo kufanya wachezaji kupoteza imani na vyombo husika vya mchezo huu. Tambarare itapatikana ikiwa Sheria zinazoipa mahakama zetu uhuru wa kweli (judicial independence) zitaboreshwa na vyombo husika vitajitathmini na kutekeleza majukumu yake kwa uaminifu kwa kufuata viwango vya maadili.​


Mdau akilalamika kukosa imani na mfumo wa upatikanaji haki (Chanzo, Jambo tv)

Kazi na Ajira. Asie fanya kazi na asile. Tutafanya kazi gani ilihali uwanja haupo tambarare?. Ndani ya mchezo huu haijalishi unachokijua, cha muhimu ni yule unaemjua. Wahanga wakubwa wa mchezo huu wakiwa vijana hasa wale waliomaliza vyuo vikuu ambao bila "connection" ya kazi na ajira hulazimika kuwa madalali ingawa walisomea uhandisi. Sekretarieti ya ajira isiwe tuu refa wa kuchuja pia itafute "green pastures" na kututengenezea mafunzo yanayoendana na masoko ya ajira. Kuboreshwa kwa mifumo ya sekretarieti ya ajira katika mchakato wa kuajiri ni mwarobaini wa kuufanya uwanja huu kuwa tambarare.
MWISHO
Yote tisa, la kumi na la mwisho nchi ya ahadi haiko mbali, ikaribu. Naiona Tanzania yenye mabawa endapo kila mchezaji atashiriki kikamilifu kwenye kuusawazisha uwanja wetu ili historia isituhukumu kwa kutojishughulisha na ustawi wa kizazi kijacho. Hatujachelewa, rasilimali tunazo, wajenzi tunao na nguvu tunazo hivyo kazi iendelee.​
 
Upvote 2
Back
Top Bottom