The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 747
- 2,112
Uwekezaji katika elimu ya msichana unaweza kubadilisha jamii, nchi na dunia nzima. Wasichana wanaopata elimu wana uwezekano mdogo wa kuolewa wakiwa chini ya umri na wana uwezekano mkubwa wa kuishi maisha yenye afya na yenye mchango mkubwa kwa jamii.
Elimu kwa binti ni suala kubwa zaidi ya kumpeleka tu shuleni. Pia inahusu kuhakikisha kwamba wasichana wanajihisi salama wakiwa shuleni; kuwa na fursa ya kukamilisha ngazi zote za elimu, kupata ujuzi wa kushindana katika soko la ajira; kupata ujuzi wa maisha unaohitajika ili kukabiliana na dunia inayobadilika; kufanya maamuzi juu ya maisha yao wenyewe; na kuchangia kwa jamii zao na dunia.
Kuhakikisha kwamba wasichana wote wanapata elimu bora ni haki yao ya kibinadamu, lakini pia ni kipaumbele cha maendeleo ya kimataifa.
Watu binafsi na nchi zote zinaweza kunufaika na elimu ya wasichana. Wanawake wenye elimu bora huwa na ufahamu zaidi kuhusu lishe na huduma za afya, wana watoto wachache, wanaolewa katika umri sahihi, na watoto wao kwa kawaida huwa na afya bora, ikiwa wataamua kuwa mama.
Wasichana wakielimika wanakuwa na uwezekano mkubwa wa kushiriki katika soko rasmi la ajira na kupata mapato ya juu. Utafiti wa Benki ya Dunia wa mwaka 2018 unakadiria kwamba fursa finyu za elimu kwa wasichana, na vikwazo vya kumaliza miaka 12 ya elimu, vilizigharimu nchi duniani kati ya dola trilioni 15 za Marekani na trilioni 30 kwa kupoteza ujuzi na mapato ambayo yangeweza kuletwa na idadi kubwa ya wasichana waliokosa fursa za elimu.
Makadirio yanasema duniani kote, wasichana milioni 129 hawako shuleni, ikiwa ni pamoja na milioni 32 wa umri wa shule ya msingi, na milioni 97 wa umri wa shule ya sekondari.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa umaskini ni mojawapo ya mambo yanayoweza kuamua kama msichana anaweza kupata na kumaliza elimu yake au la. Tafiti zinasisitiza kwamba wasichana wanaokabiliwa na matatizo mengi – kama vile kipato cha chini cha familia, wanaoishi katika maeneo ya mbali au ambao wana ulemavu – wako nyuma zaidi katika kufikia na kuhitimu elimu.
Ukatili pia huzuia wasichana kupata na kumaliza elimu. Mara nyingi wasichana wanaolazimika kutembea umbali mrefu kwenda shuleni huwa katika hatari kubwa ya kufanyiwa ukatili na wengi hukumbana na ukatili hata wanapokuwa shuleni.
Kwa mujibu wa shirika la Global Women Institute, inakadiriwa kuwa takriban wasichana milioni 60 wananyanyaswa kingono walipokuwa wakienda au shuleni kila mwaka. Hii huwaletea madhara makubwa kwa afya yao ya akili na kimwili na ustawi wa jumla huku pia ikisababisha mahudhurio ya chini na viwango vya juu vya kuacha shule.
Ndoa za utotoni pia ni changamoto kubwa. Wasichana wanaoolewa wakiwa wachanga wana uwezekano mkubwa wa kuacha shule. Pia wana uwezekano mkubwa wa kupata watoto katika umri mdogo na wanakabiliwa na viwango vya juu vya ukatili unaofanywa na wenzi wao. Hii inaathiri elimu na afya ya watoto wao, pamoja na uwezo wao wa kupata riziki.
Kulingana na ripoti ya Benki ya Dunia na wadau ya mwaka 2017, zaidi ya wasichana 41,000 walio chini ya umri wa miaka 18 huozwa kila siku. Kukomesha tabia hii kungeongeza ufaulu wa elimu unaotarajiwa wa wanawake, na pamoja na hayo, mapato yao yanayoweza kutokea. Kulingana na makadirio ya ripoti hiyo, kukomesha ndoa za utotoni kunaweza kuzalisha faida zaidi ya dola bilioni 500 kila mwaka kila mwaka.
Uwezeshaji wa mtoto wa kike unapaswa kuanza katika ngazi ya familia. Ni muhimu kuwafanya wajisikie kuwa wa thamani na sawa na kila mtu mwingine.
Ukiweka maadili sahihi na kumpa huduma stahiki mtoto wa kike, anakuwa na nafasi ya kuja kuwa mwanamke imara. Elimu kwa msichana inaweza kuleta mabadiliko ya maisha sio tu kwa maisha ya mtu binafsi bali kwa jamii kubwa zaidi.