SoC01 Uwepo mkakati wa kudhibiti wizi wa kutumia pikipiki

SoC01 Uwepo mkakati wa kudhibiti wizi wa kutumia pikipiki

Stories of Change - 2021 Competition

Noel Shao

Member
Joined
Jan 19, 2017
Posts
89
Reaction score
185
Tatizo la ajira nchini bado halijapata ufumbuzi wa kudumu hasa kwa rika la vijana. Ila kuanzia miaka ya 2005 ujio wa vyombo vya usafiri vya bei ya wastani kama bajaji na pikipiki vimekuwa msaada wa ajira kwa vijana walio walio wengi na wanaopenda kujitafutia ridhiki kwa njia ilio halali, hii si tu kwa wale waliokosa shule tu, bali hata kwa wahitimu wa ngazi tofauti.

Matumizi ya usafiri wa bajaji na pikipiki maarufu kama ‘bodaboda’, yamekuwa yakiongezeka kila kukicha. Kuna mengi ya kujivunia kwa matumizi ya vyombo hivi vya usafiri, kwani vimekuwa msaada katika maeneo mbambali ya nchi katika miji na vijijini. Katika maeneo ya mijini matumizi ya vyombo hivi hususani bodaboda ni makubwa ukilinganisha na maeneo mengine, kutokana na tatizo sugu la foleni za mara kwa mara.

Watumiaji wa bodaboda hupendelea vyombo hivi kwani huwawezesha kufika eneo lolote kusudiwa kwa wakati sahihi ama kazini, katika miadi tofauti nyakati za asubuhi, mchana hata usiku. Na maeneo ya nje ya mji yasiyofikaka kwa urahisi ndipo vyombo hivi hupendelewa zaidi

Fahari na uzuri wa vyombo hivi umeongezeka kwa kuwa vinatumiwa na watu wa kada mbalimabali wa kima cha chini na hata wa kima cha juu, wanaopenda kutunza muda na wazembe pia.

Kumekuwa na juhudi za mamlaka kutoruhusu vyombo hivi kuingia kiholela katikati ya miji mikubwa ili kuzuia uhalifu, na kuondoa kero kwa watumiaji wa barabara kwa lengo la kuifanya miji yetu ionekane safi kama miji ya mataifa mengine makubwa yaliyoendelea.

Aidha vyombo hivi hususani bodaboda vimekuwa vikilaumiwa kwa kutofuata sheria za barabarani, kama madereva kutokuwa na leseni za udereva na kofia ngumu “helementi”. Hivyo kuwa chanzo cha ajali nyingi zinazo pelekea vifo na ulemavu.

Kwa upande mwingine pikipiki hasa aina ya “boxer zimekuwa chanzo na sababu kubwa ya uhalifu nchini hasa katika jiji la Dar es salaam. Pikipiki zimekuwa zikitumiwa kufanya uhalifu wa aina tofauti kama uporaji, na mauwaji

Katika utekelezaji wa adhima yao, hutumia silaha mbalimbali za moto kama mabomu ya kurusha kwa mkono, bunduki, visu, mapanga, bisibisi au nondo, hivyo kuongeza hofu na taharuki kwa raia na mali zake. Walengwa wakubwa ni wateja wa mabenki wa kutoa au kupeleka fedha.

Vile vile hata ukwapuaji wa simu za mikononi, vito vya thamani au pochi za kike “vipima joto”, wahalifu wa kutumia pikipiki wamekuwa wakihusishwa navyo hivyo kupelekea usalama kuwa mdogo mijini.

Kila kukicha vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti matukio ya mara kwa mara ya uhalifu wa pikipiki, hivyo kuonyesha ni jinsi gani bado uhalifu unazidi kuenea na kuota mizizi.

Katika utekelezaji wa uhalifu huu, namba za usajili “plate number” hukunjwa au kutumia namba bandia kwa lengo la kuzuia kutotambulika kwa haraka.

Natoa rai kwa Jeshi la Polisi chini ya mkuu wa jeshi hilo, IGP Sulemani Siro kutumia weledi na mafunzo yao ya kazi kuhakikisha wanazima na kumaliza kabisa matukio haya ya uhalifu wa kutumia pikipiki, kwani yawezekana mtandao wa uhalifu ni mkubwa na unazidi kukua, hivyo juhudi za makusudi bado zinahitajika ili kurejesha usalama wa raia na mali zake.

Bado tuna imani na Jeshi la Polisi katika mapambano haya, na njia mbadala ambayo ikitiliwa mkazo na ikawa na watu waaminifu inaweza kuwa muarobaini, ni polisi shirikishi/jamii na kuweka Polisi wa siri katika maeneo mengi ya mijini.

Pia ni vema wamiliki halali wa bodaboda kuhakikisha kuwa kabla hawajafanya makabidhiano ni muhimu kusaini mkataba na kujiridhisha kuwa ni mtu mwamifu na ana miliki leseni ya kuendesha.

Mwisho, wananchi wamekuwa wanaishi na wahalifu katika maeneo yao, ni jukumu la kila raia mwema kuwa mzalendo kwa kuzuia uhalifu kwani naamini kila mmoja ameshaguswa kwa namna moja au nyingine na matumizi yasiyo halali ya bodaboda.

Kama si kuibiwa basi ni ajali. Wananchi tunawajibu wa kushiriki vita hii kwa kutoa taarifa ili kutokomeza uhalifu huu, ulinzi unaanzia kwetu.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom