Pre GE2025 Uwepo wa Dawati la Jinsia katika Vyama vya Siasa utasaidia kupunguza mazingira ya Rushwa ya Ngono

Pre GE2025 Uwepo wa Dawati la Jinsia katika Vyama vya Siasa utasaidia kupunguza mazingira ya Rushwa ya Ngono

Mijadala ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025 (Kabla, wakati na baada)

MeVSMe

JF-Expert Member
Joined
Mar 25, 2024
Posts
270
Reaction score
425
Zanzibar: Asha Bakar (40) mtoto wa mwisho kati ya watatu wa familia ya Bakari Juma, Asha ambaye pia ni mama wa Watoto watatu, anayeishi na mume wake kisiwani Unguja, anasimulia safari yake ya uongozi ilivyokatika hafla, baada ya kutakiwa kimapenzi na bossi wake.

“Bosi wangu aliniambia baada ya kutoka katika kikao cha kujadiliwa, nisijali kuhusu kuipata nafasi hiyo ya mjumbe wa Kamati ya Taifa, lakini nimfuate nyumbani kwake usiku wa saa moja, halafu mambo mengine nimuachie yeye,” Asha amesema kwa masikitiko na aibu.

Ule usemi wa ngombe wa masikini hazai ulimkuta Asha ambaye anaendelea kusema baada ya kutakiwa kimapenzi na bosi wake, hakujua wapi pa kukimbilia na uamuzi aliouchukuwa ni kujitoa katika kinyanganyiro hicho, ili kuepuka aibu na fedheha.

”Unasema wapi aibu hio nilitoka na kuendelea na maisha yangu mengine,” amemaliza Asha.

Kamati za Maadili zipo katika chama chake lakini mifumo dume ndio imetawala na asilimia kubwa ya Wajumbe na Wenyekiti katika kamati hizo ni Wanaume, hivyo ni suala la aibu kwenda kushtaki malalamiko yake ya rushwa ya ngono kwenye kamati husika.

Kupata Taarifa na Matukio ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kila mkoa ingia hapa: LGE2024 - Special Thread: Orodha ya Mijadala ya Mikoa yote Tanzania Bara inayoshiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 pamoja na Zanzibar

“Nafasi za Wanawake”
Takwimu kutoka Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini, Tanzania inaeleza kuwa kuna ina vyama 19 vyenye usajili kamili, kati ya hivyo ni vyama vitatu tu ndio wenyekiti wao ni Wanawake, kama Chama Cha Mapinduzi — CCM, ACT WAZALENDO na Chama cha Sauti ya Umma - SAU.

Vyama vitatu makatibu wao Wanawake ambavyo ni Chama cha Kijani - CCK, United Democracy Party -UDP na NCCR Mageuzi.

“Umuhimu wa Dawati”
Pili, Said Mohamed ni Diwani wa Wadi ya Mahonda Wilaya ya Kaskazini A Unguja amesema Dawati la Jinsia linasaidia kupunguza hali ya kuwepo kwa vitendo vingi vya udhalilishaji katika vyama vya siasa.

Anasema “Wanawake wamekuwa wakikumbwa na ukatili na udhalilishaji wa kijinsia katika vyama vyao kipindi cha uteuzi na kampeni, hawana sehemu rafiki ya kupeleka malalamiko yao ili yafanyiwe kazi.”

Pili ambaye anatokea CCM anasema “Kawaida Kamati za Maadili, Mwenyekiti ni Mwanamme na Katibu ni Mwanamke, Wajumbe ndio mchanganyiko, unafikiria mara mbili mbili nipeleke lalamiko langu pale na je yatafanyiwa kazi?”

Halima Ibrahimu Mohamed, Katibu wa Uenezi na Itikadi na Waziri katika Baraza Kivuli la Chama cha ACT WAZALENDO, aliwahi kugombea nafasi ya Uwakilishi katika Uchaguzi wa Mwaka 2020 katika Jimbo la Malindi Zanzibar lenye jumla ya wadi mbili na Shehi 11.

“Ni kweli upo umuhimu wa kuwekwa Dawati la Jinsia katika Vyama vya Siasa kwani Wanawake watapata sehemu ya kupeleka kero zao zinazowakumba katika kutafuta nafasi za uongozi na hilo dawati liwe na viongozi wanawake pia,” amemaliza Halima.

“Serikali na Wadau”
Anna Athanas Paul ni Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto amesema tathimini iliyofanywa na Wizara hiyo, imeonesha Wanawake bado wapo kidogo katika nafasi za uongozi ukilinganisha na Wanaume jambo ambalo linahitaji kuangaliwa.

”Takwimu zilizokusanywa na Wizara kutoka taasisi mbalimbali kwa mwezi Machi mwaka 2024, ni asilimia 30 tu ya wanawake ambao wako kwenye uongozi ukilinganisha na wanaume ambao ni asilimia 70,” amesema Naibu Waziri Anna.

Anna ameongeza kuwa Serikali inaendelea na jitihada katika kufikia malengo yaliyowekwa kupitia Dira ya 2050 na mpango wa maendeleo (ZADEP) 2021/2026 ambapo lengo katika nafasi za uongozi ni kufikia 50/50.

Ziko Mamlaka ambazo zinahusika na masuala ya Rushwa kwa ujumla wake na kwa Zanzibar, Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi —ZAECA kupitia Afisa Elimu Yussuf Juma Suleiman amesema: “Sheria ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar, Sheria namba 5 ya Mwaka 2023 Kifungu cha 52, itasaidia kupunguza kwa vitendo hivyo kwa kiasi kikubwa na kitawapa ari na hamasa wanawake wengi kuingia katika uongozi na kutoa taarifa na hizo taarifa sisi tutazichukulia hatua.”

Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar, (TAMWA ZNZ) ni taasisi isiyo ya kiserikali iliyopo Kisiwani Zanzibar inayojishuhulisha na maswala ya utetezi wa haki za Watoto na Wanawake, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA - Z Dkt Mzuri Issa, amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuanzishwa kwa Madawati ya Kijinsia katika vyama vya siasa ili kuondosha kadhia za rushwa ya ngono zinawapata hasa Wanawake.

Anaongeza “Wanawake wanaogombea nafasi za uongozi wanakumbwa na ukatili wa kijinsia na udhalilishaji katika vyama vya siasa, kutokana na kuwa hawana sehemu maalumu ya kupeleka malalamiko yao.”

Mohamed Ali Ahmed ni Naibu Msajili wa vyama vya siasa Tanzania kwa upande wa Zanzibar amesema kuwa, upo umuhimu wa kuanzishwa Dawati la Jinsia katika vyama vya siasa lakini huku akiwasihi viongozi wakike wasikubali kutoa rushwa kwa sababu ya kupata nafasi ya uongozi.

Anasema “Kuongezwa kwa kifungu kipya cha 10 c ndani ya Sheria ya Vyama vya Siasa nchini, kitatoa nafasi kwa Wanawake kuongezeka ushiriki wao na pia kuwajibika kwa kuwa na sera ya jinsia kwa muda wote, kwani hapo awali hali haikuwa hivyo kwenye Vyama vya Siasa.”
 
Back
Top Bottom