JE, kwa nini Waislamu wanafunga? Kufunga ni kutekeleza Amri ya Mwenyezi Mungu ambaye anasema katika Kurani: “Enyi mlioamini, mmeamrishwa (mmelazimshwa) kufunga (swaumu) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mwenyezi Mungu (Kurani 2:183).
Kwa hiyo utaona ibada hii kwa mujibu wa Kurani, hawakulazimishwa Waislamu wa leo pekee bali hata jamii zilizotangulia. Kwa kufunga mtu anapata nini? Mwenyezi Mungu anajibu kwenye aya hiyo anaposema: Fungeni ili mpate kuwa wachamungu.
Tafsiri pana ya hapa ni kwamba kufunga ni kambi ama darasa ambamo Waislamu wanapaswa kuingia na watakapotoka humo wawe wameiva kiuchamungu na siyo kushinda na njaa kwa maana ya kufunga kwa mazoea au kufuata mkumbo. Yaani, kila mwaka Waislamu wanapata wasaa wa mwezi mzima wa ‘kujifua’ katika suala zima la uchamungu wao na inatazamiwa kwamba wanapotoka kwenye chuo hiki cha funga waendelee na uchamungu hadi kwenye chuo kingine, yaani Ramadhani nyingine kwa wale watakaojaliwa kufika.
UCHAMUNGU NI NINI?
Uchamungu ni sentensi fupi yenye maelezo marefu. Lakini kwa kifupi uchamungu ni kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kujiepusha na makatazo yake. Yaani kila anachokifanya mfungaji kinapaswa kiwe kinachunga mipaka aliyoelekeza Mwenyezi Mungu.
Mwanazuoni mmoja anaeleza mambo manne yanayohusu uchamungu ambayo ni; kuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu, kufanya kila linalomridhisha Mwenyezi Mungu, kuchuma au kula vya halali na mwisho ni kuishi kwa kujiandaa kila wakati kwamba utaondoka duniani muda wowote na hivyo ukutane na mola wako ukiwa salama.
Kwa hiyo mfungaji anapaswa kujipima kwa kujiuliza haya maswali: Je, yale ambayo Mwenyezi Mungu aliyoamrisha kufanya anayafanya? Yale aliyotaka yaachwe mfungaji anayaacha?
Kama mfungaji atafunga ama kumaliza mfungo na hajaacha maasi sambamba na kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu basi kwa mafundisho hayo ajue anafunga kwa mazoea na lile lengo la kufunga linakuwa halijatimia kwake.
Ni vyema kila anayefunga akajiangalia nafsi yake na kama alikuwa anafunga kwa mazoea abadilike sasa. Mafundisho yanaonesha kwamba maswahaba wa Mtume (SAW) na wema waliotangulia walifahamu sababu ya kuumbwa kwao.
Walijitambua kwa nini wako duniani na nini kitakuwa mwisho wa maisha yao hapa duniani na kisha wakatekeleza yale waliotakiwa kufanya na kuachana na yale waliyokatazwa. Hawa walikuwa wanafikia lengo la uchamungu.
FAIDA ZA UCHAMUNGU
Faida za uchamungu pia zipo nyingi na hapa zinatajwa chache. Kubwa ni kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kumuingiza mja kwenye pepo yake. Mwenyezi Mungu anasema kwamba fanyeni haraka kukimbilia msamaha wake na mfanye haraka kuipata pepo yake.
(Kurani 3:133). Ili kupata pepo ya Mwenyezi Mungu na msamaha wake lazima Muislamu ajipinde sana hususan katika mwezi huu mtukufu. Kadhalika Mwenyezi Mungu anasema kwamba pepo imeandaliwa wachamungu (na moto kwa wanaomuasi).
Hivyo, Muislamu anapofanya ibada, kuswali, kufunga, kutoa zaka, kwenda kuhiji na ibada zingine huwa matarajio ni kupata pepo ambayo ni maisha ya milele na siyo kufanya hayo kwa ajili ya kujionesha kwa wanadamu.
Kwa hiyo ni vyema mfungaji na kila anayemuamini Mwenyezi Mungu ajue kwamba kupata pepo si jambo rahisi. Ni lazima ajitahidi kumcha Mwenyezi Mungu kwa kutimiza maamrisho yake. Kwa mantiki hiyo, mtu asione kuamrishwa kufunga ya Ramadhanini kama Mwenyezi Mungu kampa uzito.
Anayedhani hivyo, huyo hajajijua na wala hajajitambua. Ni kwamba mfugaji anaumia leo lakini kesho atapata pepo na bila shaka hakuna Muislamu ambaye anajitambua halafu hataki pepo.
Mwenyezi Mungu anasema hakika vipenzi vyake hawatakuwa na hofu katika maisha ya dunia wala ahera. Hawa hawatamuogopa yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu tu na wala hawatahuzunika siku ya kiama.
(Kurani 10:63) Leo hii ukikutana na watu wengi utaona wana hofu za kidunia ambazo si Mwenyezi Mungu. Mtu anakuwa na hofu ya kufukuzwa kazi, hofu ya kuzaa watoto wengi, hofu ya kuoa wake wengi (wanaume), lakini yote hii ni kukosa uchamungu kwa maana ya kumtegemea Mwenyezi Mungu mtukufu ukweli wa kumtegemea.
Mchamungu hata akipata matatizo ama maradhi anajua ni sehemu ya mitihani tu ya Mwenyezi Mungu na ndipo anakuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu kwa sababu anajua ni mtihani. Mchamungu pia huwa na huruma na mwema kwa wenzake na hivyo pia hupata manufaa ya kidunia kutokana na wema wake.
YA KUFANYA MFUNGAJI
Katika mwezi huu ambao bado uko katika kumi la kwanza, kila aliyefunga anatakiwa kuzidisha ibada kwa maneno na vitendo. Walioghafilika huko nyuma wazinduke na kuifanye Ramadhani hii kama kitu cha kuwabadilisha.
Walete toba kwa wingi, wasimame sana usiku kwa kufanya ibada na kumtaja sana Mwenyezi Mungu kwa sababu huu ndio mwezi wa kuchuma thawabu kwa wingi. Wakati miezi ya kawaida mtu akifanya jambo jema moja analipwa hadi thawabu 10, mwezi huu thawabu zinafika hadi zaidi ya 700 kwa jambo moja la heri.
Kadhalika kila mwenye chochote ajitahidi katika kutoa sadaka, kusaidia wenye shida, kusalimia wagonjwa na kila jambo lenye heri. Ni vizuri ifikie matendo ya kila aliyefunga mwezi huu yawavute hata wasio Waislamu. Kwa kifupi mfungaji anatakiwa kuwa mwema na huruma kwa binadamu wenzake bila kujali dini zao.
MAMBO YA KUEPUKA
Kufunga hakuna maana ya kuacha kula na kunywa pekee, bali pia mfungaji anatakiwa kuacha maasi yote.
Aache kusema uongo, kusengenya, kuiba, kudhulumu, kuzidi baada ya kufuturu na kadhalika. Matendo hayo hayafai siku zote lakini katika mwezi wa Ramadhani anayeyafanya huandikiwa madhambi maradufu.
KUFUNGA BILA SWALA
Waislamu wengi wanaipa heshima ibada ya funga na kuitekeleza ibada ya swala. Hili ni kosa kubwa kwa mfungaji, na ingawa hizi ni ibada mbili tofauti lakini huenda funga ya asiyeswali ikawa ya mashaka kukubaliwa.
Marehemu Sheikh Nassoro Bachu aliwahi kuulizwa kuhusu kufunga bila kuswali akajibu: “Kwani funga kaamrisha nani na swala kaamrisha nani? Itakuwaje uchupe nguzo ya pili uende nguzo ya nne halafu useme eti Mwenyezi Mungu anaikubali swaumu yako kwa kuwa umekaa na njaa sana (huku ukiwa huswali). Hili haliwezekani.”
KURUDIA MAASI
Anayefanya ibada ya Ramadhani pekee na ikiisha anarudi kwenye maasi huyo hajajua lengo la kuumbwa kwake na kufanya ibada. Kimsingi, kama ilivyoelezwa hapo juu, Ramadhani ni kambi au chuo ambacho humfanya mtu abaki mchamungu.
Ramadhani ni sawa na msimu wa kulima kwa matarajio ya kuvuna baadaye. Kuna watu wanadhani wamekuja hapa duniani, kula, kunywa na kustarehe. Hawajiulizi wale waliotangulia mbele ya haki; babu zao, bibi zao na hata wazazi wao wako wapi na kule walikotangulia kuna nini kinachoendelea.
Mwezi huu unatakiwa umsaidie kila aliyefunga kuhuisha moyo wake kwa mema. Anayerudi kwenye maasi baada ya Ramadhani, ni sawa na mkulima anayechoma shamba lake baada ya kustawi vyema na hivyo wakati wa mavuno (kiyama) atakuwa na majuto mkubwa.
Sababu kubwa ya watu kurejea kwenye maasi baada ya Ramadhani ni kukosa hofu ya Mwenyezi Mungu. Mtu wa aina hiyo hajui nafasi ya Ramadhani na ndio hao wanaofunga kwa kwa mazoea.
Tena utaona siku hizi za mwanzo za Ramadhani, watu watajaa misikitini lakini kadri siku zinavyokwenda watakuwa wanapungua. Hii ni tofauti na waliotangulia ambao kadri mwezi ulivyokuwa unayoyoma ndivyo wanavyojifunga kibwebwe na kusikitika kwa nini unaisha mapema.
DHIMA YA MAIMAMU
Katika mwezi huu ni vyema maimamu na wahadhiri wakajitahidi kuwafanya Waislamu wabaki misikitini. Moja ya mbinu ni kuwafanya waujue ukubwa wa Mwenyezi Mungu sambamba kuwatia hofu kuhusu yeye. Wajue kwa uhakika hapa duniani ni sehemu ya kupimwa matendo yetu.
Hilo lifanyike si kwa maneno makali kwani Mwenyezi Mungu anataka watu walinganiwe dini kwa hekima na mawaidha mazuri kwa sababu baadhi ya watu nyoyo zao ni dhaifu.